January 31, 2018



 Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, ameitaja mbinu kuu wanayoitumia katika michezo yao ya Ligi Kuu Bara kuwa ni kushambulia muda wote.

Mrundi huyo ambaye anasaidiana na kocha mkuu, Pierre Lechantre raia wa Ufaransa, wapo kwenye mikakati mizito ya kuipa ubingwa timu hiyo ambayo kwa sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 35.

Timu hiyo ikiwa imefikisha pointi 35, ndiyo yenye mabao mengi kwenye ligi hiyo mpaka sasa baada ya kufunga mabao 35.

Katika mabao hayo, 12 yamepatikana kwenye mechi nne zilizopita ambazo Simba ilikuwa bila ya Kocha Mcameroon, Joseph Omog aliyetimuliwa mwishoni mwa mwaka jana, huku mikoba yake ikichukuliwa na Mrundi huyo kabla ya ujio wa Lechantre.
Djuma amesema mbinu hiyo ya kushambulia anaamini kuwa itawapa ubingwa kirahisi.

 “Unajua mpira wa kisasa ukishambulia sana unampa wakati mgumu mpinzani wako kwani mara zote wewe unakuwa umetoka mbali ya goli lako, sasa mpaka mpinzani wako afike golini kwako inakuwa kazi kubwa.

“Lakini pia, tunapofanikiwa kupata bao basi tunashambulia tena kwa nguvu kwa kuwa morali inakuwa imepanda hali ambayo inatusaidia sana mpaka sasa kuwa na matokeo mazuri kwa kufunga mabao mengi.


“Mbinu hii itatusaidia kufunga mabao mengi sana kwani inamnyima mpinzani wetu kutushambulia kwa sababu tunapokuwa golini kwake, anakuwa na kazi mbili za kufanya, kwanza ni kulinda goli lake, pili kupanga mashambulizi kitu ambacho hakiwezekani kufanyika kwa wakati mmoja na kufanikiwa kwa usahihi,” alisema Djuma.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic