February 12, 2018




NA SALEH ALLY
UNAWEZA kujifunza jambo ambalo linaweza kukuondoa na kujua kuwa ulichokuwa unafanya si sahihi na huenda mihemko na kutojua mambo kunakufanya uwe mshamba.

Wengi hawakubali kwamba ni washamba, ushamba ni kutojua jambo. Inawezekana haulijui lakini kwa kuwa unapenda kuonekana unajua basi ukafikiri uko sahihi.

Mpira wa Tanzania unapungukiwa mambo mengi sana yakiwemo yale ya nje ya uwanja na mashabiki wamekuwa watu wanaohusika katika suala hilo.

Yanga na Simba ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika. Wote tayari wamecheza mechi zao za kwanza.

Tunaweza kusema tumeona uwezo wa timu zetu na hali ilivyo, wapi wanatakiwa kurekebisha na kipi wanatakiwa kufanya ili kufanikisha mambo.

Lakini ajabu kabisa kuna tabia ya kizamani ambayo hatutaki kubadilika na mashabiki wengi wamekuwa wakijiapiza kama vile ni jambo la msingi sana, huenda na wasitake kusikiliza hata kinachozungumzwa, huenda watajifunza.

Mfano, shabiki wa Simba, ataona ni fahari kubwa kuzungumza mbele ya watu aonekane mbele ya mashabiki wenzake wa Simba kwamba yeye ni mwiko na kamwe hawezi kuishangilia Yanga.

Shabiki huyo anaweza akaona ni ufahari mkubwa, kuvurumisha matusi au kebehi kwa Yanga mbele ya mashabiki wenzake wa Yanga, ili aonekane anaipenda sana timu yake.

Hali kadhalika, shabiki wa Yanga naye anaweza akafanya jambo lolote ilimradi aonekane anaipenda sana Yanga tena aonekane mbele ya watu bila ya kujali upenzi wake kwa timu anayoipenda ni wake na si kutaka watu waone ndiyo aonekane anaipenda.

Nani ni kiranja wa kukagua watu wanaozipenda Yanga au Simba, kama yuko ni kwa nini? Nani Yanga ni yake yeye bila ya wengine? Kaipata wapi? Hii ndiyo sehemu ya ulimbukeni wa mashabiki wengi.

Si vibaya, ulimbukeni huo ukaendelea kunapokuwa na mashindano ya Ligi Kuu Bara au mingine kama ile ya Kombe la Shirikisho. Lakini tunapoingia katika michuano ya kimataifa, basi tubadilike.

Yanga inacheza dhidi ya St Louis ya Shelisheli, wewe Mtanzania unajivika uraia wa Shelisheli na kuanza kuizomea timu ya Tanzania pale uwanjani, huu ni ujinga uliotukuka. Sawa na shabiki wa Yanga anayeizomea Simba ikipambana na Gendamarie ya Djibouti.

Hauwezi kuishangilia Yanga au Simba, una haki na hakuna anayeweza kukulazimisha. Ukiamua kuizomea Yanga au Simba za Tanzania pia una haki, hakuna anayeweza kukulazimisha. Lakini ninaamini kuna akili ndani ya ubongo wako inaweza kutengeneza kipimo cha mwenendo wa maisha sahihi kufikia kile kilicho sahihi.

Mtanzania anayetaka timu ya Tanzania ifungwe kwa kuwa hataki mafanikio ya Watanzania wengine na anafurahia bora timu ya Shelisheli au Djibouti ishinde dhidi timu ya Tanzania. Huu ni ulimbukeni wa kipimo cha juu kabisa unaopaswa kulaaniwa.

Unajiona hauwezi kuishabikia Simba kwa kuwa wewe ni Yanga kwelikweli, basi baki nyumbani, angalia kwenye runinga. Lakini ukienda uwanjani, moja kwa moja unakuwa upande wako ni timu ya Tanzania ambayo kama ikivuka itaendelea pia kukuletea burudani zaidi.

Wakati ukiwa njiani unakwenda kuiona Yanga au Simba inacheza dhidi ya wageni, jiulize isingefikia hapo ungewaonaje? Pia jikumbushe kwamba ikishinda, utaendelea kuona burudani zaidi na kujifunza zaidi.

Kuepuka kutokuwa mzalendo, ni kubaki nyumbani bahati nzuri siku hizi Azam TV wanaonyesha, basi unaweza kuangalia huko uliko mpira ukiisha, unaweza kuendeleza ushabiki wako unavyotaka wewe.


Nitie msisitizo, ushabiki ni furaha yako wewe lakini haukufanyi utende yasiyo sahihi. Pia kama ushabiki ni furaha yako, basi haina haja kushabikia kwa kutaka kuonekana unapenda sana ili usifiwe, furahisha nafsi yako na uendelee na maisha yako, maisha ya kutaka kujionyesha yanaonyesha uwezo mdogo wa kujitambua.

4 COMMENTS:

  1. Brother Saleh nadhani huu ujinga unaoukemea unaanzia kwa baadhi ya viongozi wa hivi vilabu hasa yanga kwani kabla ya match ya Yanga na st Louis Khaji Manara aliwaomba mashabiki wa Simba kutoizomea Yanga katika match yao lakini utaona jinsi gani watu wa yanga walivyomuwakia Manara. Wengine walifika mbali zaidi kwa kusema Manara anatafuta sapota ya yanga kinamna kwa timu yake kwani anahisi timu yake itakabiliwa na ushindani mkali zaidi kuliko ule wa yanga zidi ya st Louis lakini Mungu si Athumani kila mtu kashuhudia nini kimetokea pale taifa.

    ReplyDelete
  2. Yupo kiongozi mmoja wa Yanga ndiye alijitokeza wazi kuwa hakukubaliana kabisa na rai ya kiongozi wa Simba kuwataka mashabiki wao kutoizomea Yanga itapocheza na St. Louis jambo ambalo sio la kizalendo kabisa. Salehe wewe unamfahamu. Ingekuwa vema somo lako kuanzia kwake. Huyu ni tatizo mara zote.

    ReplyDelete
  3. Ujinga huo haukuanza leo! Ni kwamba wako waliouanza na sasa wajinga wenzao wanawajibu.
    Kumtetea mtu yeyote ambaye aliufanya ushamba huo bila kujitokeza kwanza akakiri kuwa ulikuwa ni ushamba kama si ulimbukeni na unapaswa kuachwa haitatusaidia kubadilika maana ni sanaa zilezile!
    Hivi kwanini hatujikumbushi tulikojikwaa tunataka kuangalia tulipoangukia?
    Ikumbukwe ni viongozi wa timu hizohizo tunazoita kubwa wanaowafanya mashabiki kuwa malimbukeni. Kuna wakati watu walipata kuimba "..Uzalendo umetushinda!!!"
    Tuache siasa kwenye michezo.

    ReplyDelete
  4. Salehe Jembe! Wewe na mashabiki wa simba wenzako ni wapumbavu kabisa yaani nyambafu. Waliokomenti hapa wote ni wa mbumbumbu fc. Article yako ni ya kujificha nyuma ya mbumbumbu fc kuwatukana mashabiki wa Yanga! Nakuheshimu sana Ila naomba ukome kuwatukana mashabiki wa timu ambao hawaendi uwanjani ambapo simba haichezi na timu yao! À ma unapenda tukupe jina?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic