February 28, 2018



Na Saleh Ally
UTAMU wa Ligi Kuu Bara unazidi kupanda kwa kasi kubwa kutokana na namna ambavyo timu kwa zaidi ya asilimia 70 zilivyojiandaa vizuri na kuongeza ugumu.

Ugumu wa ligi ndiyo burudani yenyewe kwa kuwa ushindani ni tofauti ya ubora wa kiwango na hii ndiyo ile niliyoeleza hivi karibuni kwamba kiwango kinaonekana kukua.
Wafungaji wengi wa Ligi Kuu Bara wamecharuka na inaonekana difensi nyingi zimezidiwa ujanja kutokana na kasi yao ya kupachika mabao.

Ingawa washambulizi wa timu kadhaa hasa Simba, Yanga, Azam FC na Singida United wanaonekana kufanya vizuri zaidi kuliko wale wa timu nyingi.

Simba wanaongoza kwa kuwa na mabao 46 ya kufunga kwa ujumla wakifuatiwa na watani wao Yanga waliokuwa na 30 kabla ya mechi yao ya leo dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.
Ukiachana na timu za juu, Mwadui FC ndiyo imeonyesha ukali wa ushambulizi kwa kuwa na mabao 21 licha ya kwamba iko katika nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi.

Walio katika nafasi ya tatu katika msimamo, Azam FC wao wamefunga mabao 20 sawa na Singida United na Prisons wana 18.
Kuna safu za ushambulizi ambazo ni kali na hazizidi timu sita kati ya 16 na utaona safu za ulinzi ambazo ni imara ni chache sana ambazo hazizidi tatu.

Simba wamefungwa mabao nane na Yanga na Azam kila mmoja ameruhusu tisa na timu hizo tatu pekee ndiyo zilikuwa zimefungwa mabao chini ya 10 kabla ya mechi ya Yanga dhidi ya Ndanda.

Utagundua safu nyingine za ulinzi zilizobaki hazikuwa imara kabisa au zimeshindwa kuhimiliki kasi ya ushambulizi. Mfano Majimaji imefungwa mabao 26 sawa na Mwadui FC lakini Mbao FC nayo wameruhusu milango yao kufunguliwa mara 25.
Baada ya mechi 19, Simba inaonekana kuwa na safu kali zaidi ya ushambulizi kutokana na kupata wastani wa kufunga mabao 2.42 katika kila mchezo. Maana yake unapokutana na Simba, uhakika wa kufungwa mabao mawili ni jambo la kawaida kabisa.

Wastani huu unatokana na idadi ya mabao yaliyofungwa na mechi walizocheza. Yanga ina wastani wa 1.66 katika kila mechi na Azam FC ni bao moja katika kila mechi.

Simba inaonekana kuwa na tofauti kubwa na huenda wameamua kurekebisha kosa la mabao ya kufunga na kufungwa yaliyowanyima ubingwa msimu uliopita baada ya kumaliza ligi wakiwa na mabao sawa ya kufunga na watani wao Yanga.

Washambuliaji wawili tu wa Simba, yaani Emmanuel Okwi na John Bocco wamefunga jumla ya mabao 26. Okwi ana 16 na Bocco ni 10, idadi ambayo ni kubwa zaidi ya timu nyingi za ligi hiyo.
Bocco peke yake amefunga mabao mengi kuliko Stand United na Njombe Mji kwa kuwa kila moja imefanikiwa kupachia mabao tisa pekee.
Kwa upande wa Okwi, yeye amefunga mabao mengi kuliko Mtibwa Sugar, Lipuli, Stand United, Njombe, Ndanda, Kagera na Majimaji!

Unaweza ukawa ni wakati mzuri sana wa washambuliaji wa timu  hizo nao kujiuliza kupitwa na mshambuliaji mmoja kwa idadi ya wao wote kama ni jambo sahihi.

Inaweza ikawa haifurahishi kama itaingizwa katika ushabiki lakini kitakwimu na suala la kutaka ubora, basi kuna kila sababu timu ambazo washambuliaji wake kwa ujumla wanazidiwa na mshambuliaji mmoja au wawili kutoka Yanga au Simba, wanapaswa kujiuliza na kufanya ya uhakika kuzikomboa timu zao.

Raha ya mechi bao, kweli mabao yanafungwa mengi lakini inaonekana wafungaji wameelemea upande mmoja na wengine wamelala kabisa.

Je, ni utafutaji wa washambulizi haukuwa sahihi au wafungaji wenyewe wameshindwa kujiamini au hawapewi nafasi? Ni kosa lao au la kocha kwa sababu mifumo inawashinda? Haya yote ni mambo ya kujifunza.

Kwa somo la Okwi au Obrey Chirwa wa Yanga ambao wameweza kufunga mabao zaidi ya timu nyingine, linaweza kuwa kona ya mabadiliko.

Washambuliaji wengi nao wanapaswa kuona wivu na kutaka kufanya vizuri kama Okwi na baadaye zaidi ya hapo.

Haiwezekani timu nzima, tena zaidi ya watu watatu au wanne wanazidiwa na mchezaji mmoja au timu mbili zinazidiwa na watu wawili.

Kuna kila sababu ya kulichukulia jambo hilo kama somo na mwisho kujipima kwamba wewe ni mshambuliaji kweli au unapenda kuwa mshambuliaji na hauna vigezo?

Mshambuliaji lazima ajifunze, afanye mazoezi ya ziada atafute mbinu za ziada na kadhalika. Kuendelea kupitwa kwa kiasi cha kupindukia ni kuukubali uzembe.

Okwi, Chirwa na Bocco nao wanastahili pongezi kwa mwendo wanaokwenda nao na wengine wanapaswa kuiga kwa kuchukulia ni somo lenye ushindani linaloweza kuwapa mabadiliko.



TANZANIA BARA
                                 P         W     D     L        F     A      GD  PTS
1. Simba                  19     13    6       0       46    8       38    45   
2. Yanga                  18     10    7       1       30    9       21    37   
3. Azam                   19    9       8       2       20    9       11    35   
4. Singida                  19   9       7       3       20    16    4       34   
5. Prisons                  19   7       8       4       18    14    4       29   
6. Mtibwa                19    6       9       4       14    13    1       27   
7. Ruvu                    19    6       5       8       16    24    -8     23   
8. Lipuli                   19    4       8       7       12    15    -3     20   
9. Mbeya                 19   4       8       7       16    22    -6     20   
10. Stand                  19    5       5       9       8       19    -11   20   
11. Mwadui              19    3       10    6       21    26    -5     19   
12. Mbao                 19     4       7       8       17    25    -8     19   
13. Ndanda             18    3       9       6       12    17    -5     18   
14. Kagera               19    2       9       8       10    18    -8     15   
15. Majimaji            19    2       9       8       15    26    -11   15   
16. Njombe              19    2       9       8       9       23    -14   15   

        

1 COMMENTS:

  1. Ushauri mzuri sana. Kwa kuongeza bidii kwa wachezaji ndivyo timu zitavuna magoli mengi zaidi na ushindi zaidi. Isipokuwa hiyo pia inategemea na majukumu wanayopewa wachezaji na kocha wao pale uwanjani. Mfano tumeelezwa Kichuya wa Simba amepewa jukumu la kuwalisha mipira wachezaji wenzie hususan Okwi na Bocco na hivyo kujipunguzia nafasi ya yeye mwenyewe kufunga magoli. Ni kweli wachezaji wote 10 wa timu ukitoa golikipa, wakipata nafasi tunategemea wapachike magoli lakini kocha kwa mifumo yake kuna watu 2 au 3 au 1 ndiye zaidi anampanga kwa nafasi ya kupachika magoli.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic