NA SALEH ALLY
NAKUKUMBUSHA kuhusiana na wachezaji wengi sana wa Tanzania ambao walifeli maisha yao kwa kuwa waliamini ndoto yao kuu kimaisha ya soka ni kucheza Yanga au Simba na baada ya hapo ingetosha kabisa.
Kwa kuwa walipambana na baadaye kufanikiwa kupata nafasi ya kucheza katika klabu hizo, basi ukawa ni mwisho wa maisha yao ya soka na leo wanaishi maisha magumu mtaani huku wakitupa lawama kwa klabu hizo au uongozi wa juu wa mpira wa Tanzania.
Umesikia mara nyingi wachezaji wakongwe wakilia kuhusiana na kuonekana hakuna anayewajali. Lakini wao wamekuwa hawawazi hata kidogo wapi walikosea na huenda kujilaumu wao kuzitukuza Simba na Yanga kwa kuamini ndiyo ukomo wa maisha bora ya mpira.
Wako wachezaji wengi sana walipata nafasi ya kucheza nje ya Tanzania. Mfano Ujerumani, Sweden, Urusi lakini mambo hayakuwa mazuri si kwa sababu ya uwezo.
Walishindwa kufanya vizuri kwanza kabisa kwa kuwa walikuwa wanaamini bado wanahitajika Tanzania. Huku walijua wanakubalika katika klabu hizo kubwa za Yanga na Simba.
Hawakuongeza juhudi kule kwa kuwa waliamini wakirejea watapokelewa na walipofanya hivyo ikawa hivyo. Maisha yakaendelea Tanzania na leo kama nilivyokueleza, wanalaumu tu.
Lakini wako wachezaji pia ambao pamoja na kupata bahati ya kwenda kufanya majaribio katika nchi kama Urusi na kadhalika, waliona ingekuwa nafuu kwao kuendelea kubaki Tanzania kuzichezea Yanga na Simba ambayo ni heshima kuu kisoka kwa Mtanzania wa kawaida. Heshima kwa marafiki na familia.
Ajabu wengi walitaka kuondoka na kwenda kucheza Ulaya au nje ya Tanzania baada ya mambo yao kuwa yameshaharibika au thamani zao kuwa zimeporomoka katika klabu hizo. Wakawa wamechelewa.
Nafikiri hili limfikie kijana Kelvin John ambaye sasa ni nyota wa kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys. Tayari ameshatupia mabao sita kabla ya mechi ya leo.
Amefanikiwa kufunga hat trick, ameonyesha uwezo mkubwa kwa maana ya kufunga na kuisaidia timu kupata ushindi. Tayari timu kubwa zimeanza kuvutiwa naye na inaonekana wazi anaweza kupata timu hapa ndani au nje ya Tanzania.
Kwa mchezaji kama yeye, hahitaji kwenda Yanga au Simba kwa kipindi hiki. Inawezekana kabisa kila mwanadamu angependa kupata fedha zaidi, lakini suala la kuangalia mbali ni kubwa zaidi.
Kelvin anapaswa kukataa fedha nyingi za Yanga au Simba kama itatokea ili apate nafasi ya kutoka nje ya Tanzania kwa kuwa hasa Ulaya wanahitaji mchezaji wa umri wake ili kumpa makuzi wanayoamini kwao ni sahihi.
Ule msemo wa “samaki mkunje angali mbichi”, wenzetu wanauamini sana. Wangependa mchezaji ambaye anaweza kukunjika na kwenda kwa mwendo sahihi wanaouamini wao.
Kipindi hiki kwa Kelvin ni bora zaidi tena kama atapata nafasi ya kucheza Kusini mwa Afrika, Kaskazini au nje ya bara hili litakuwa jambo zuri sana kwake, kuliko kuchukua mamilioni ya Simba au Yanga halafu akae benchi akisubiri nafasi ya wakongwe waumie au kuonewa huruma ili acheze.
Vizuri akikubali kupoteza nafasi ya kupata mamilioni sasa ili aje ayachote hapo baadaye. Huu ndiyo wakati mzuri kwake wa kujinyima achote kidogo ili hapo baadaye afanikiwe kuchota kwa wingi zaidi huku akiwa shujaa wa taifa letu.
Nini hana? Kama kasi, akili, nguvu na hata umbo ambalo limewaangusha Watanzania wengi, kwake si ishu.
Kinachotakiwa ni hesabu za uhakika sasa kwamba baada ya miaka mitano mbele anatakiwa kuwa wapi. Aachane kabisa na suala la klabu hizi kongwe, la sivyo ataishia katika rekodi za wengine na mwisho naye ataishia kulaumu tu.
SOURCE: CHAMPIONI
SIMBA na YANGA zimekuwa mbuzi wa kafara kwa kila uozo uliopelekea kufeli kwa Soka letu lakini kiuhalisia Tanzania kama si Simba na Yanga basi mpira wetu ungelikwishakuwa kuzimu zamani sana. Kiuhalisia wachezaji ndio wanazoziharibu Simba na Yanga kwa kushindwa kuzingatia maadili ya kazi baada ya kuajiriwa. Tanzania kuna timu nyingi tu mpaka Zanzibar sasa mchezaji gani wa kitanzania alietoka nje ya Simba na Yanga akaenda kucheza nje ya nchi kwa mafanikio?
ReplyDelete