NA SALEH ALLY
KUNA jambo tunaweza kujifunza na mwisho kujua faida ya kuwepo kwa Azam FC katika mchezo wa soka nchini, kwamba ni kubwa sana.
Nimeanza kuufuatilia mpira wa Tanzania Bara wakati ule kukiwa na wapinzani kama akina Sigara, Nyota Nyekundu, Mecco na Tukuyu Stars za Mbeya, CDA ya Dodoma, Biashara Shinyanga, Pamba ya Mwanza na nyingine.
Kama nitazungumzia sana timu hizo, huenda nitawapiga chenga watu wengi sana wa kizazi cha mpira wa sasa.
Hata mimi kuna mengi sikumbuki sana ingawa nilibahatika kuwashuhudia wachezaji mahiri wa zamani kama Celestine Sikinde Mbunga wa Majimaji. Baadaye kizazi ambacho nimekulia mimi cha akina Edibily Lunyamila.
Wakati huo, Yanga na Simba walikuwa na upinzani mkubwa sana ndiyo maana uliona timu kama Coastal, African Sports, Majimaji na nyingine ziliweza kubeba ubingwa mbele ya wakongwe Yanga na Simba.
Baadaye, mambo yalibadilika baada ya kuanza kudorora kwa timu hizo na ushindani ukashuka kwa kiasi kikubwa. Simba na Yanga wakawa wanafanya wanavyotaka wao na si vingine.
Muda umesonga zikiwa na ufalme huo, lakini ndani ya miaka sita utaona kuna mabadiliko makubwa ambayo yameingizwa na Azam FC ambao ndani ya miaka minne wamechukua ubingwa mara moja.
Ushindani wao wamevuruga ule “upacha” wa Yanga na Simba, kuwa kama leo si huyu, yuko yule na ni walewale. Unakumbuka timu kama zile nilizokutajia ziliwahi kuingia na kuchukua ubingwa mbele ya Yanga na Simba.
Simba wamekuwa hawashiriki michuano ya kimataifa kutokana na uwepo wa Azam FC na hii inaongeza ushindani na wingi wa mechi kubwa.
Takribani miaka 10, Simba dhidi ya Yanga ndiyo imekuwa mechi kubwa inayosubiriwa, hadi ilipoibuka Azam FC na utaona imebadilisha mambo kwa siku za hivi karibuni na kurejesha ule ushindani wa kipindi kile Coastal, African Sports, Sigara au Pilsner zikiwa katika kiwango chake.
Mfano mzuri ni mechi mbili za hivi karibuni, Azam FC ilipoikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikapoteza kwa mabao 2-1, ikakaribishwa na Simba Uwanja wa Taifa, pia ikapoteza kwa bao 1-0.
Pamoja na kupoteza kwa Azam FC, mechi hizo zinaweza kuwa mfano au kitu cha kuzungumzia katika mpira wa Tanzania kwa kuwa ushindani ulikuwa mkubwa na mpira ulichezwa kweli.
Tumeona mechi kadhaa badala ya soka kupewa kipaumbele, kunakuwa na tafrani na mambo yasiyo na msingi. Lakini mechi hizo mbili, tumeona Azam FC ikipambana kweli na wakongwe hao na ilikuwa mechi ambayo hauwezi kujua nani atashinda.
Mechi dhidi ya Yanga ilikuwa ni ile ambayo hauamini kama dakika 90 zitaisha na sare au mmoja kushinda. Lakini ile dhidi ya Simba, nayo ilikuwa vigumu kuamini Simba watashinda au ni sare hadi usikie kipenga cha mwamuzi.
Mechi za Ligi Kuu Bara, zinapaswa kuwa na ushindani wa namna ile na hakika kweli Azam FC, imeongeza utamu wa Ligi Kuu Bara kutokana na ushindani wake.
Angalia Azam FC, leo imetengeneza mechi nyingine nne za Ligi Kuu Bara ambazo zinaweza kuitwa “Big Match” badala ya watu kuendelea kusubiri mechi mbili tu katika msimu ambazo zinaitwa “Big Match”. Tena katika mechi hizo kubwa, unashuhudia soka safi na la ushindani, jambo ambalo ni bora zaidi kwa nembo ya maendeleo ya mpira wa Tanzania.
Hakuwezi kuwa na ligi bora kama hakuna ushindani sahihi wenye vipimo bora. Mwendo wa Azam unachangia hofu ya kusaka maendeleo kwa wakongwe Yanga na Simba na hofu ya maendeleo ni bora katika kusaidia kupatikana kwa mafanikio.
Mechi hizo dhidi ya Azam FC na wakongwe ni ladha zaidi na maendeleo zaidi. Huenda timu nyingine nazo zinaweza kuamka na kuongeza ubunifu ili kujenga ubora unaoweza kuzitikisa Yanga na Simba ili kusaidia kuongesha ushindani na maendeleo pia.
0 COMMENTS:
Post a Comment