Na Saleh Ally
NILIPOANDIKA kwa mara ya kwanza makala kuhusiana na mshambuliaji Donald Ngoma, nilipata watu wengi sana walionisakama kwa maneno ambayo hakika yanaudhi.
Sikujali sana kwa kuwa kazi hii sasa ni takribani miaka 20 na nimezoea kuwa na jicho la mbali kabla ya wengi na kila ninapoeleza jambo, huonekana kama ninawaangusha au kutaka kuwakandamiza.
Sikuchoka, nikaandika tena kwa mara ya pili na kuelezea namna ambavyo Ngoma raia wa Zimbabwe anavyokuwa hasara kwa Yanga na pia nikafafanua kuhusiana na uongozi ulivyokurupuka kumsajili Ngoma kwa ajili ya kuwaridhisha mashabiki wake.
Ngoma alikuwa amekubaliana kila kitu na Simba, lilibaki suala la kusaini mkataba, Yanga wakamuwahi katikati, uongozi ukataka kuwaonyesha wanachama wako uko vizuri na hauwezi kupokonywa Ngoma.
Taarifa za awali, zilieleza wazi kwamba benchi la ufundi chini ya George Lwandamina halikuwa na shida na Ngoma, lilikuwa tayari aondoke kwa kuwa alimaliza msimu uliopita akiwa nje na hakuwa na faida kubwa.
Hivyo, uongozi ulifanya mambo kisiasa, kuangalia wanachama watasemaje na si mahitaji ya kiufundi yanataka nini ambayo ni sahihi kwa asilimia 99 kuliko yale ya mashabiki au wanachama.
Ngoma amecheza mechi chache za mwanzo, baadaye amerejea tena katika kundi la wachezaji majeruhi na ndipo nilipoanza kuandika makala zangu.
Ile ya pili, nilielezea namna ambavyo Ngoma ni hasara kubwa kwa Yanga na namna viongozi walivyoshindwa kuliona na kusisitiza, wangeweza kuachana naye ili fedha wanazomlipa waziongeze kwa wachezaji wanaofanya juhudi uwanjani na kuisaidia timu.
Yanga si Real Madrid ambayo Gareth Bale anaweza kukaa nje muda mrefu, analipwa tu na mambo yakaonekana sawa. Hata Madrid wakati fulani waliwahi kuhoji suala la majeraha ya Bale na kulipwa kwake mshahara mnono.
Hivyo, Yanga walikuwa wanatakiwa kuliona hilo mapema na ikiwezekana kuepuka kuyapeleka mambo kishabiki kwa lengo la kuwafurahisha mashabiki na wanachama huku ikiendelea kutoa na wakati mwingine kuingia madeni kama ambavyo usajili wa Ngoma kumbakiza ulivyowagharimu zaidi ya Sh milioni 100 halafu wakafanya kila kitu siri.
Wale wa kunilaumu na kunibatiza kuwa mimi ni Simba ndiyo maana nimeandika hivyo wakaendelea kusema nawahujumu, natamani Ngoma aondoke aende Simba. Sikujali tena, maana mara nyingi pia nimeitwa mimi ni Yanga sana ndiyo maana naisakama Simba.
Mashabiki wengi wa Yanga au Simba, huwa wanasoma ulichoandika lakini wanaelewa kile wanachofikiria, jambo ambalo hakika huwa linachanganya sana kwa kuwa wanakuwa hawana muda sahihi wa kukifikiria kile unachokiandika kwa kuwa machoni wanaona lakini hawafikishi sehemu sahihi ya fikra ili kufanya tafakuru jadid.
Sasa nimesikia uongozi wa Yanga, umeunda kamati kwa ajili ya kulichunguza suala la Ngoma kama kweli ugonjwa wake utakuwa ni wa muda gani, anastahili kubaki Yanga au wavunje mkataba na aondoke zake.
Kwanza nikafarijika kuona kile ambacho niliwaeleza mara kadhaa kimetokea na huenda nilikiona mapema kabla yao na nikawa wazi kuwaeleza kwamba kuna shida kwa Ngoma na walipaswa kuifanyia kazi.
Lakini ukawa ni wakati mzuri wale mashabiki waliosema mimi ni shabiki wa Simba ndiyo maana nataka Ngoma aondoke asajiliwe Msimbazi. Sasa nikawa najiuliza, sijui na viongozi wao nao ni Simba? Nafikiri wakati mzuri wao kutafakari upya niliyoyaandika. Pia niwakumbushe, Yanga ni ya Tanzania na Ngoma anatokea Zimbabwe, naamini mnanielewa.
Kilichonishangaza zaidi ni kuona, uongozi Yanga ulimsajili Ngoma kwa sababu ya siasa, ukaendelea kumbakiza kwa sababu ya siasa na umeona anastahili kuondolewa, unaendelea kufanya siasa. Hili ni jambo baya kabisa.
Kuna haja gani ya kuunda kamati kwa ajili ya mchezaji kuangalia eti abaki au mkataba wake uvunjwe? Suala la kujua ugonjwa wake ukoje, kamati inajua vipi, kwa nini kitengo cha tiba cha Yanga kupitia daktari wake mkuu, angewasiliana na daktari wa Ngoma, baada ya hapo majibu ayafanyie kazi kitaalamu na mara moja kuifikishia kamati ya utendaji ifikie uamuzi mara moja.
Kama viongozi wa Yanga wanashindwa kuamua mara moja suala kuhusiana na maslahi ya klabu na wanataka kutengeneza mlolongo mrefu wa kisiasa, naona kabisa wanashindwa kujielewa na wanashindwa kugundua walifanya makosa makubwa na ya muda mrefu katika suala la Ngoma na wanazidi kuyaendeleza.
Bila hata ya kukwepesha mambo, Yanga inaingia hasara kwa Ngoma, wakati wa kumuondoa ilikuwa kabla ya msimu huu, kama walichelewa, alistahili kuondoka miezi kadhaa iliyopita.
Sasa wanaendelea kujichelewesha hadi mwisho wa msimu na huu ni uthibitisho kwamba wao si imara katika kushughulikia matatizo bila kuingiza siasa kwa kuwa ni viongozi waoga wanaohofia maneno ya wanachama ambao mara nyingi wanafanya mambo kwa furaha na si kitalaamu.
Habari bro!nimekua nafatilia sana post zako,habari za ndani kuhusu Ngoma sio ugonjwa ila ni madai yake ya hela ya usajili ambayo ni zaidi ya milion 100 kama ulivyosema,kumbuka alivyoenda kwao kutibiwa alianza kufanya mazoezi na timu ya nyumbani kwao mpaka akachaguliwa timu ya taifa kwa ajili ya CECAFA,tujiulize huo ugonjwa ni upi usiojulikana mpaka atafutwe daktari wake?Madaktari wa timu ni wataalamu wa tiba michezoni,wanaweza kugundua tatizo la mchezaji hata kwa kutazama mwendo tuu,usishangae Mavugo kupishana na Ngoma mwisho wa msimu,timu zetu zinaingia kwenye majanga ya kiuchumi kwa mambo haya haya,kama Beno Kakolanya aligoma mpaka alipwe na ni hela ndogo vipi kuhusu Ngoma?Kumbuka jengo linadaiwa na linalipiwa kidogo kidogo kwa gate collection,time will tell bro
ReplyDeleteKama ni kweli Ngoma anaumwa kumuhukumu kwa kumfutia mkataba wake haitakuwa sahihi. Jambo kama hili lilikuwa litokee kwa Simba na mchezaji wake Kapombe na magazeti mbalimbali na wadau tulilaani kitendo cha kutaka kumtosa Kapombe wakati bado anasubiri kupona sawasawa. Simba walisikia wakampa zaidi ya miezi 6 amepona na sasa yupo uwanjani ancheza mpira wa uhakika. Leo iweje kwa Ngoma tuone halali aondolewe? Ngoma anaumwa. Mimi nilidhani ungefika wakati busara itumike uongozi wa Yanga umpeleke nje kwa matibabu zaidi. Mbona wenzenu wa Azam na Simba wanawapeleka wachezaji wake nje kutibiwa? Tumtendee haki Ngoma mpelekeni akatibiwe kama walivyofanyiwa wachezaji akina Nduda wa Simba na Mbaraka wa Azam sio kufikiria kukatisha mkataba wake wakati ni mgonjwa.
ReplyDeleteKuna taarifa pia kuwa Niyonzima pia ni majeruhi na Klabu yake ya Simba inamgharamia kwenda matibabu India. Ni kweli mchezaji huyu hajaonekana uwanjani muda sasa. Ni vema Yanga ikaiga jambo hili zuri la kuwagharamia wachezaji kama Donald Ngoma aende matibabu India au Afrika Kusini kutibiwa badala ya kumtelekeza na kuanza kufikiria kukatisha mkataba wake na Klabu wakati anahitaji matibabu.
ReplyDelete