February 2, 2018






NA SALEH ALLY
HIVI karibuni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe aliibuka na kutoa maneno ambayo yalionekana ni makali kwa beki Shomari Kapombe.

Kapombe amerejea Simba safari hii akitokea Azam FC. Kabla beki huyo alipata umaarufu mkubwa akiwa Simba ambayo ilimsajili kutoka mkoani Morogoro akiwa kinda.

Baada ya kufanya vizuri akiwa Simba, Kapombe alipata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa katika Klabu ya AS Cannes ya nchini Ufaransa.

Pamoja na klabu hiyo kusifiwa kwa kuwatoa wachezaji wengi maarufu akiwemo William Gallas, mwisho Kapombe alishindwa na kuamua kurejea Azam FC ambayo aliichezea hadi alipojiunga Simba tena.

Hata hivyo, hadi Simba inacheza mechi ya tisa, Kapombe alikuwa bado nje ya uwanja anauguza majeraha ambayo yalimuandama sana katika siku za mwishoni akiwa na Azam FC kabla ya kurejea Simba.

Hans Poppe ambaye ndiye anashughulikia usajili akiwa msimamizi mkuu alionyesha kukerwa na Kapombe kutopona na kuendelea kubaki nje huku wenzake wakiendelea kuitumikia klabu hiyo katika mchuano mkali dhidi ya Yanga na Azam FC ambazo zilikuwa zinakimbizana na Simba kwa mwendo wa “zero distance”.

Hans Poppe alionekana na kushangazwa na Kapombe kuchelewa kupona wakati aliamini alitakiwa kuwa tayari amerejea uwanjani na kuanza kuitumikia timu hiyo ambayo kweli ilikuwa ikimhitaji.

Wakati huo Simba ilikuwa ikilazimika kuwatumia wachezaji mbadala kutokana na namna hali ilivyokuwa na huenda Hans Poppe alikuwa akijua jambo zaidi kuliko mashabiki, ndiyo maana hata alichokisema kiliwakwanza wengi na wakaamini hakuwa sahihi.

Siku chache baada ya Hans Poppe kusema kauli hiyo, Kapombe alionekana akiwa ameanza mazoezi na baadaye kuanza kuitumikia Simba. Hakuna ubishi, hata Kapombe atakuwa aliguswa iwe kwa kuudhiwa au kuona kama ameonewa.

Lakini kauli ya Hans Poppe ambayo ilikuwa chungu kwake, ndiyo iliyomuamsha upya na ikiwezekana kufuatilia matibabu yake kwa umakini zaidi na ikiwezekana kupata moyo wa kijasiri kuhakikisha anatoka katika maumivu na kurejea.

Wakati mwingine maumivu ni jambo la kisaikolojia, yanaweza kuwa madogo, lakini hisia zikakutuma kwamba maumivu yake ni makali sana na kama utaamini hivyo, basi mambo yatakuwa hivyo kweli.

Kurejea haraka kwa Kapombe kunaweza kuwa ni maneno ya Hans Poppe ambaye huenda alikuwa akimaanisha jambo sahihi lakini aina ya uwasilishaji mambo ndiyo ukawa tatizo kubwa na mwisho akawaudhi wengi.

Hata baada ya Kapombe kurejea uwanjani, unaona ile kauli ya Hans Poppe inaendelea kuwa dawa kwake kutokana na namna ambavyo anacheza kwa juhudi ya juu kabisa.

Hakuna ubishi kwamba kwa namna anavyocheza Kapombe kwa sasa, ni mtu anayetaka kufanya jambo zuri na lenye manufaa kwa klabu yake na kuwaonyesha kwamba ni mtu mwenye manufaa na faida na kukaa kwake nje kama alivyowahi kusema halikuwa jambo alilopanga au kutaka.

Usitake kulazimisha kujiuliza, kwa nini baada ya Hans Poppe kuzungumza na siku chache Kapombe akarejea. Angalia namna maneno yake yalivyokuwa kama shubiri kwa uchungu na ukali lakini matokeo yake yamekuwa jambo jema kabisa na lenye manufaa kwa Kapombe na Simba pia.

Tayari Kapombe ameomba apewe muda zaidi. Kwamba pamoja na kurejea, anaamini anahitaji muda wa kuwa fiti zaidi na ana imani atafanya vema zaidi.

Kwa suala la uwezo, hakuna sababu ya kuingia hofu na uwezo wake. Lazima tukubali, katika maisha hakuna jambo zuri kama kuelezana ukweli kwa kuwa ukweli unauma lakini ni dawa.

Kitu kikubwa, wakati mwingine ni vizuri kuangalia katika uwasilishaji wake maana hata kwa njia nzuri ukweli hufika na inawezekana tunaweza kujifunza jambo kupitia maneno ya Hans Poppe kwa Kapombe ambaye sasa amerejea na hakuna maneno tena.



1 COMMENTS:

  1. Hakuna Binaadamu mkamilifu. Kapombe na Hanspope ni sawa na kijana na mzazi wake hasa ukichukulia maanani makuzi ya shomari ndani ya simba. Shomari kapombe ni mwanafamilia wa wa Simba sports cub na Hanspope ni miongoni mwa walezi wazuri sana tu ndani ya Simba. Licha ya maneno ya Hanspope kuhusu kapombe kutafsiriwa vibaya amini usiamini Hanspope hakuwa na nia mbaya pengine ni upendo wake zaidi juu ya kapombe kutaka kumuona akiwa fit. Kama kuna watu wanaojitolea kwa hali na mali katika mpira basi ni Hanspope, na kwa kweli jitihada zake kama vile vyombo vya habari au watu hawazioni na kumpa credit kwa kile anachokifanya lakini kwa haraka na kwa kasi ya radi watu walikimbilia kumshambia baada ya kauli yake ile ya ushauri kwa kapombe. Unajua kila mtu ana maadui wake na hungojea pale watakapopata sapota ya watu zaidi kukumaliza. Tumekaa na kumsikiliza muheshimiwa Magufuli katika hutuba zake nnaimani zina vitu vya kujifunza katika masuala ya kuambizana ukweli.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic