February 16, 2018




NA SALEH ALLY
MARA nyingi tumewahi kuzungumzia kuhusiana na kiwango cha chini cha Ligi Kuu Bara katika mambo mbalimbali ya kiufundi.

Pamoja na ubora wa mambo kadhaa kumekuwa na mabadiliko ya vitu ambavyo kama vitaendelea kuboreshwa basi kuna jambo litakuwa likionekana katika ligi yetu.

Ligi Kuu Bara imeonekana kuimarika katika kiwango na hasa katika suala la uchezaji hasa unapozungumzia timu zinapokutana.

Zinapokutana utaona kweli kuna mpira unachezwa, mfano mzuri mechi ya juzi kati ya Majimaji na Yanga. Wageni hao jijini Dar es Salaam, wamekutana na kipigo cha mabao 4-1 lakini mechi imeisha wao wanaongoza kwa umiliki wa mpira.

Majimaji imekuwa na umiliki bora kuliko Yanga tena ikiwa ugenini. Lakini yenyewe imepoteza kwa kufungwa mabao zaidi ya matatu, jambo ambalo linaonyesha soka linapiga hatua.

Umiliki wa mpira maana yake ni mafunzo, timu inajiamini na inajua inachofanya. Lakini ukiangalia Yanga wamefunga mabao manne, kati ya hayo manne unaona kuna mvuto wa asilimia zaidi ya 80 ya mabao hayo.

Mfano, angalia bao la Emmanuel Martin au lile la Papy Tshishimbi, ni mabao safi na ya kiwango ambacho yanaonyesha kuna jambo fulani katika mpira wa nchi hii.

Kama uliangalia mechi ya Mwadui wakiwa nyumbani kwao mjini Shinyanga dhidi ya Simba, utaona kujiamini kwa Mwadui FC na uchezaji wao ulivyokuwa, mambo yakienda kwa uhakika bila kujali walishinda au walipoteza.

Kiwango cha mpira kinapopanda, haiwezekani ikawa ni timu mbili pekee. Badala yake inatakiwa timu nyingi ziwe zimepandisha viwango vyao na kucheza soka linaloeleweka, lenye mvuto na ushindani kwa kila upande.

Ukiachana na timu, hata wachezaji wanapaswa kupandisha viwango vyao ili kutengeneza ile hali ya ushindani kwa kuwa wanaocheza ni wachezaji. Miiko na ubora inajulikana inapatikanaje.

Utaona upande wa wachezaji kuna mabadiliko na unapoona wachezaji wanafanya vizuri maana yake kuna mabadiliko kwa walimu ambao ndiyo wanakuwa wanawafundisha.

Hapa inawezekana walimu wamejiongeza zaidi kimafunzo na wanachokitoa kinakuwa ni msaada. Lakini inawezekana pia mafunzo yao sasa yanafika vizuri kwa wale ambao wanafundishwa na wanayafanyia kazi kwa ubora ambao ni sahihi kabisa.

Tayari unaona Bodi ya Ligi imesimamia suala la viwanja kuwa na ubora na kama utaendelea kujumlisha haya mambo, mwisho jibu linakuwa ni ubora wa usahihi.

Suala la ubora wa viwanja halijaisha, kwa maana ya kwamba viwanja sasa ni vizuri sana. Kuna hali ya unafuu lakini bado kinachotakiwa ni kuweka mkazo.

Mfano, Uwanja wa Kambarage ambao ilichezwa mechi kati ya Simba na Mwadui, utaona kulikuwa na hali ngumu kwa wachezaji kuweza kumiliki mpira vizuri.

Hiki ni kati ya vitu ambavyo tumekuwa tukipigia kelele kuhusiana na namna hali ilivyo. Suala la uwanja na majani wala si gumu sana, yaani linawezekana na liko ndani ya uwezo wa wahusika na wakiamua wanaweza kufanya.

Lazima tukubali kwamba ili kiwango cha mpira kikue, basi ni lazima kuwe na mabadiliko ya vitu kadhaa ambavyo baadhi yake nimevitaja.
Ushindani hauwezi kukamilika bila ya kuwa na viwanja bora, uchezaji wa ushindani ambao viwango vitaendana na mambo kama hayo niliyoyaelezea.

Kama kuna uwanja bora, wachezaji hawamiliki mpira kwa uhakika, hawatoi pasi za uhakika, hakuna mabao bora kama vile kupiga mashuti na kadhalika, kiwango hakiwezi kuwa cha kupongezwa au bora.


Kila kitu kinawezekana na kinachotakiwa ni uamuzi na kila mmoja kama mdau kufanya kazi katika eneo lake na mwisho tukijumlisha, ubora na kiwango vinakuwa juu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic