February 10, 2018




Na Saleh Ally
MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga wanashuka dimbani leo dhidi ya St Louis ya Shelisheli. Hii ni mechi muhimu ya Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi hii, inawakutanisha Yanga na mabingwa wa Shelisheli ambao tayari kocha wao, Ulrie Mathiot ameweka wanachotaka kufanya kwamba wataishangaza Yanga katika mechi ya leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo huenda inafanana sana na ile ya Simba kesho ambao wanacheza na Gendamarie, timu kutoka nchini Djibouti ambayo imetua nchini jana, ikiamini inakwenda kucheza na vigogo.

Hakuna anayejua maandalizi ya Gendamarie lakini sifa yake ni kuwa, timu inayocheza pasi nyingi, ina wachezaji wenye vipaji lakini hawana uzoefu na mara nyingi soka kwao si la kiwango cha juu kwa maana ya mafanikio.

Yanga na Simba, ndiyo wawakilishi wa Tanzania na wamepangiwa timu zinazotokea katika nchi ambazo hakika si vibaya kusema ni vibonde.



Vibonde kwa maana wako chini sana kimafanikio ingawa sisi tunajiona tuko chini. Kuna rekodi zinaonyesha namna ambavyo wamekuwa wakinyanyasika na timu za Tanzania, Pamba iliwahi kushinda zaidi ya mabao 10 dhidi ya timu ya Shelisheli.

Nakumbuka Simba iliwahi kuishindilia Gendamarie mabao 6-0. Lakini kikubwa ambacho Yanga na Simba wanapaswa kukumbuka, zama zinabadilika na Wajibouti na Washelisheli, hawawezi kuendelea kubaki walivyo milele.

Huenda kazi ya mabadiliko katika timu zetu imekuwa ni ya chini sana, hivyo tunaweza kujikuta tunaamini tumebadilika, kumbe wako wanaokimbia na kutufikia.

Yanga na Simba wakishinda watacheza dhidi ya timu za Misri au Zambia na kadhalika. Sote tunajua kwamba kiwango cha nchi ambazo watakutana nazo baada ya kushinda sasa kipo juu.

Kikubwa wanachotakiwa kuanza mapema leo na kesho, ikiwezekana kushinda kwa kishindo na kurahisisha marudio ya mechi zinazofuatia watakapokwenda kucheza ugenini.

Kama watafanya mzaha halafu Simba au Yanga watolewe na timu hizo, basi itakuwa ni aibu ya karne kama ambavyo Kilimanjaro Stars ilivyowahi kufungwa na Somalia katika michuano ya Chalenji.

Mpira una fomula ambayo inaonyesha hauwezi kushinda bila kucheza, hauwezi kupata ushindi bila ya kupanga mipango bora ya namna ya kushinda kwa kufanya maandalizi sahihi yanayotakiwa.



Simba na Yanga wamefanya maandalizi, wanakutana na wawakilishi wa kimataifa wa nchi hizo mbili na lazima wajue lazima wamebadilika hawawezi kuwa wale wa miaka ya 1990 au mwanzoni mwa 2000.

Wachezaji wote wa Yanga na Simba lazima wajue wanaliwakilisha taifa kwa wakati wanapokuwa wanacheza na lazima wanapokuwa uwanjani watambue hilo.

Dharau za wachezaji, mara nyingi ndiyo zimekuwa chanzo cha kuanguka kwa timu na baadaye lawama zikaangukia kwa makocha na viongozi. Safari hii, wao ndiyo wanapaswa kujua wanawajibika na ni lazima washinde.

Kingine Yanga na Simba, kama nafasi itatokea, basi waitumie zaidi kushinda mabao mengi na kuonyesha kuwa hawataki mchezo.

Kama watashinda kwa mabao mengi, kwanza watakuwa wamelainisha mechi zinazofuata za ugenini kwa kuwa bado hawajajua mazingira ya ugenini yana usalama upi.

Lakini hiyo pia itasaidia kuwapa hofu hata wapinzani wao watakaocheza nao katika mechi zinazofuata kwa kuwa watajua wanakutana na timu zilizo makini. Hofu hiyo inaweza kuwasaidia kufanya vema.

Nawakumbusha, mwaka 2003, Simba iliivua ubingwa wa Afrika Zamalek ya Misri. Wakati huo Zamalek ndiyo ilikuwa timu bora barani Afrika. Halikuwa jambo dogo na lilikuwa jambo ambalo hakuna aliyelitarajia.



Simba kwa Zamalek, ndiyo sawa na Yanga na timu za Shelisheli au Simba na timu za Djibouti. Maana yake, hata timu hizo zina uwezo wa kuzitoa timu za Tanzania kama zitafanya uzembe.

Karata ya kuanzia ipo mikononi mwenu na ndiyo wenye chaguo la kuonyesha kweli mmepania kufanya vema na kuipeperusha bendera ya Tanzania. Sisi hatuna uwezo wa kuingia lakini tutakuwa majukwaani kwa siku zote mbili tukiwaunga mkono. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic