Benchi la Ufundi la Njombe Mji ya Njombe chini ya kocha mkuu, Ally Bushiri ‘Benitez’, limeibuka na kumwaga siri kuwa kwenye mchezo wao dhidi ya Simba wataingia kwa tahadhari kubwa sana kwa kuogopa kipigo kikubwa kama ambavyo Simba wamekuwa wakitoa kwa wapinzani wao wengi wanapokutana nao.
Njombe Mji walio nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, watakuwa wenyeji wa Simba wanaofundishwa na kocha Pierre Lechantre raia wa Ufaransa, katika mchezo am bao umepangwa kupigwa katika Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.
Benitez amesema kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakiisoma Simba ili kupanga mbinu ambazo zitawafanya wasiwemo kwenye mkumbo wa timu ambazo zimefungwa mabao mengi na kikosi hicho ambacho kinaongoza ligi kwa sasa kikiwa na pointi 46.
“Hizi rekodi za Simba kushinda mabao mengi kuanzia 3-0 au 4-0 zimekuwa zikitufanya kwa muda mrefu tutafakari tufanyeje kuepuka kuwa kwenye sehemu ya timu ambazo zimepokea vipigo vikubwa, hivyo tutakapokutana nao tutaingia kwenye tahadhari ya hali juu sana.
“Lakini kwa muda mrefu tumekuwa tukitafuta mbinu mbadala ya kuwazuia ambapo tumebaini kwamba mabao yao mengi yamekuwa yakitokea upande wa viungo washambuliaji wa pembeni (mawinga) hivyo nikiwa kocha ambaye naujua vyema mfumo huo basi ninajipanga vilivyo kuhakikisha kwamba tunawanyima nafasi hiyo pale tutakapokutana nao,” alisema Benitez.
Njombe Mji ilipigwa mabao 4-0 na Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, lakini ilipigwa tena 4-0 na Yanga kwenye uwanja huohuo, hivyo ndivyo vipigo vikubwa zaidi timu hiyo imevipata msimu huu.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment