Na Saleh Ally
MWANZONI mwa miaka ya 2000 ndiyo mwamko wa soka la wanawake ulianza kuonekana lakini zaidi ilikuwa burudani tu.
Watu ambao waliufanya mchezo huo uanze kuwa na mvuto walikuwa ni wale wanaojitolea kwa ajili ya mapenzi yao kwa kuwa waliamini.
Asilimia kubwa ya waliofanya kazi hiyo wapo nje ya mchezo wa soka kwa sasa, wako waliotangulia mbele ya haki na wengine wameamua kuendelea na maisha yao.
Haikuwa kazi rahisi kwa kuwa kulikuwa na upinzani mkubwa sana kwa watu kuamini hata hapa nyumbani wasichana au wanawake wanaweza kucheza soka.
Historia ya soka la wanawake kwa hapa nyumbani ina milima na mabonde na wengi hawakuamini kuwa ni sahihi na ilikuwa ni vigumu sana kwa watu kujitokeza na kusaidia hadharani.
Lakini walioianzisha Sayari FC na baadaye Mburahati FC ambaye alikuwa ni Dk Tamba, waliendelea na moyo wao wa kujitolea hadi ilipofikia mambo kuanza kwenda vizuri.
Timu ya Sayari FC inastahili sifa katika soka la wanawake nchini na baadaye Mburahati lakini Twiga Stars ambayo ilikuwa ikiundwa bila ya wachezaji kutoka katika timu zinazoshiriki ligi.
Twiga Stars ilifanya vizuri hadi kufikia kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika na ikaitangaza Tanzania hasa.
Stori ni ndefu na wote wanastahili sifa lakini kwa sasa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), hakika inastahili sifa zaidi.
Serengeti kupitia kinywaji chake cha Serengeti Lite imeamua kumwaga Sh milioni 450 kwa muda wa miaka mitatu kudhamini Ligi Kuu ya Wanawake.
Ligi ya wanawake ina nafasi kubwa ya kutengeneza ajira, afya bora na sifa kwa taifa na hakika SBL kupitia Serengeti Lite wameonyesha upendo wa hali ya juu.
Hata kama watakuwa wanajitangaza lakini unaweza kuona kwamba walichofanya ni kuamini kile kilichokuwa kimesahaulika na kuliletea sifa taifa.
Kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linapaswa kuhakikisha ligi inakuwa bora na ya uhakika ili kuwarejeshea Serengeti Lite kile wanachohitaji na heshima kwani uamuzi wao unaweza kuendeleza mchezo huo kwa upande wa wanawake.
Wale wanaoshughulikia au kusimamia soka la wanawake lazima wafanye kazi kwa juhudi zaidi kuwaonyesha Serengeti Lite wako sehemu sahihi na wanapaswa kuendelea kubaki na ikiwezekana, waongeze fedha zaidi.
Waamuzi wachezeshe kwa kufuata sheria 17, waonyeshe ni mchezo wa haki kwa lengo la kuukuza. Viongozi wa timu waonyeshe wanastahili kuwa na ligi na inapaswa kukua.
Lakini wachezaji waonyeshe wana malengo na wanataka ikue nao wakue pia na ikiwezekana siku moja wacheze nje ya Tanzania.
Kama ushindani utakua, ligi itakua na Serengeti Lite watakuwa na cha kujivunia na hawatawaacha dada zetu.
Kuwapoteza Serengeti Lite litakuwa pigo kubwa, lakini kubaki nao inawezekana ikawa faida maradufu kwa kuwa wanaweza kuongeza dau zaidi.
LIGI KUU WANAWAKE
NANE BORA 2018
P W D L GF GA GD Pts
1. JKT 3 3 0 0 19 0 19 9
2. Kigoma 4 3 0 1 5 3 2 9
3. Mlandizi 4 2 0 2 10 4 6 6
4. Baobab 3 1 2 0 6 5 1 5
5. Alliance 3 1 1 1 3 6 -3 4
6. Simba 3 1 0 2 2 6 -4 3
7. Panama 4 0 2 2 3 11 -8 2
8. Evergreen 4 0 1 3 1 14 -13 1
0 COMMENTS:
Post a Comment