May 3, 2018



Bao pekee katika mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga alilofunga beki Erasto Nyoni limehamisha kutoka mchezaji maarufu hadi gumzo zaidi.

Nyoni amekuwa gumzo kutokana na bao hilo ambalo liliipa ushindi Simba wa bao 1-0, lakini mwenye amesema, simu za pongezi na kupewa moyo zimekuwa hazina idadi.

Nyoni alifunga bao hilo wakati ikishinda bao 1-0 dhidi ya Yanga, Jumapili iliyopita na kujiweka katika nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Nyoni ameona tofauti kubwa likiwa ni bao lake la kwanza katika mechi ya “Watani wa Jadi wa Kari­akoo” kutokana na kupigiwa simu nyingi za pongezi.

Nyoni ameiambia Championi Jumatano kwamba baada ya kufunga bao hilo licha ya kwamba ilikuwa mapema lakini alijua tayari walikuwa wameshinda.

“Baada ya kufunga tu, nikajua mechi imeisha. Si kwamba Yanga wasingeweza kufunga katika dakika zote 90 lakini tulijiandaa sana,” alisema akizungumza na Championi Jumatano, jana.

“Nilishangilia sana kweli na si kawaida, unajua mechi ilikuwa na hamasa na majigambo. Hivyo nilitamani tufanye vizuri na kufunga maana yake tunakwenda kwenye malengo sahihi.”

Kuhusiana na suala la kupigiwa simu nyingi jambo ambalo hakulio­na akiwa Vital’O ya Burundi na Azam FC, Nyoni anasema zimekuwa zikimiminika.

“Simu ni nyingi kwa kweli, ni nyingi sana na wengi ni wale watu wanaonipongeza na kunitakia kila la kheri nifanye vizuri zaidi,” alisema akisisitiza si kawaida katika timu alizozichezea kabla.

Kuhusu ubingwa amesema: “Ub­ingwa bado, kikubwa sisi tunataka kushinda kila mechi. Hivyo tunashiri­kiana hadi mwisho, sasa hatu­jajiaminisha kuwa kazi imeisha.”

Beki huyo aliyewahi kucheza soka la kulipwa nchini Burundi ali­funga bao hilo kwa kichwa baada ya mpira wa adhabu wa Shiza Ki­chuya kugongwa na Raphael Daud na kumkuta akiwa peke yake, akaukwamisha.

Mechi hiyo ya “Derby ya Kari­akoo”, ilikuwa ya pili kwa Nyoni ingawa amekuwa wakionyesha ki­wango kizuri alipokutana na Yanga au Simba wakati akiwa Azam FC.

Nyoni amekuwa mmoja wa mabeki viraka ambao wana uwezo wa kucheza nafasi nyingi hali inayoongeza thamani yake kila kukicha.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic