June 16, 2018


Klabu ya Al Mokawloon ya Misri imemuondoa straika Obrey Chirwa Yanga na wako kwenye hatua za mwisho za kumsainisha, jambo ambalo limemuweka mbali na rada za Simba ambao wanamtamani.

Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Chirwa ambaye alikuwa tegemeo la Yanga msimu uliopita amemaliza mkataba wake na klabu hiyo huku Simba ikitajwa kwamba ilikuwa kwenye rada ya kumsainisha azibe pengo la Laudit Mavugo ambaye wamempiga chini baada ya kuona ni mzigo.

Simba walishafanya mazungumzo nae mara kadhaa na walikuwa wakichanga karata zao. Mchezaji huyo alisajiliwa na Yanga msimu wa mwaka 2016/17 na kuitumikia kwa misimu miwili akitokea katika klabu ya FC Platinum ya nchini Zimbabwe ambapo Yanga walivutiwa na uwezo wake walipokutana kwenye michuano ya kimataifa.

Al Mokawloon inashiriki Ligi Kuu ya nchini Misri na zamani ilikuwa inafahamika kama Arab Contractors na kwenye ligi ipo katika nafasi ya kumi kati ya timu 18 ambazo zinashiriki ligi hiyo.

Habari za ndani zinadai kuwa mshambuliaji huyo yupo nchini Misri kukamilisha taratibu za kuingia mkataba na klabu hiyo huku Yanga wakiendelea kumlainisha ingawa bado hajawaelewa.

Taarifa zinadai kuwa awali straika huyo alikuwa ajiunge na kikosi cha Difaa El Jadid cha nchini Morocco lakini mambo hayakuwa sawa kama ambavyo walitarajia na nafasi yake alichukua straika mwingine wa maana kutoka Afrika ya Kati.

“Ni kweli Chirwa kwa sasa yupo nchini Misri na ameenda huko kwa ajili ya kusaini mkataba na klabu yake mpya ya Al Mokawloon ambayo imevutiwa na uwezo wake na inataka kufanya naye kazi,”kilidokeza chanzo chetu.

Jonas Tiboroha ambaye ni meneja wa mchezaji huyo alipoulizwa jana alisema; “Chirwa kweli yupo Misri na ameenda huko kwa ajili ya kuingia mkataba na timu yake mpya ambayo atakuwa nayo msimu ujao kusema anaenda timu gani na anaingia mkataba wa muda gani siwezi kusema kwa sasa ni mapema mno lakini taarifa rasmi nitazitoa siku ya Jumatatu.”

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic