June 10, 2018


Mshambuliaji mpya wa Simba, Adam Salamba anafahamu kila kitu kuhusiana na mtihani na ushindani alionao mbele ya Emmanuel Okwi lakini amesisitiza kwamba atakaza.

Salamba ambaye amejiunga na Simba hivi karibuni akitokea Lipuli FC ya Iringa kwa dau la Sh mil 40 msimu uliopita alifunga mabao sita ambayo yote aliifungia Lipuli kwani mzunguko wa kwanza alicheza Stand United.

Straika huyo mwenye kiduku cha rasta, alianzia benchini katika kikosi cha Simba kilichokuwa kikicheza dhidi ya Kakamega na kesho Jumapili watamenyana na Gor Mahia ya Kenya.

Msimu uliopita wa ligi kuu Simba ndiyo timu iliyofunga mabao mengi zaidi huku nyota wake Okwi akiibuka mfungaji bora akitupia kambani mabao 20 na John Bocco aliweka kimiani mara 14 huku Shiza Kichuya akisifika kwa pasi nzuri za mwisho.

 Salamba ambaye ni ‘brazamen flani hivi’ alisema anafahamu Simba ina mastraika wakali, wakongwe na wazoefu hivyo anajipanga kuhakikisha anapambana nao ili waisaidie timu hiyo iweze kupata mafanikio.

“Siwezi kusema nitafunga mabao mangapi lakini mimi kama straika ni lazima nipambane na kufunga mabao. Najua timu niliyoingia ina mastraika wazuri, wakongwe na wazoefu hivyo nitafanya kadri iwezekanavyo ili nipate nafasi ya kucheza na kuisaidia timu kama ilivyo niheshimu na kunisajili.

“Hapa kikosini changamoto ni kubwa kwani Simba ina wachezaji wengi wazuri, lakini nitapambana kwanza kuhakikisha timu yangu naipa ubingwa wa SportPesa na kwenda Everton,” alisema Salamba ambaye ni mkali wa vichwa.

Naye Kocha wa Simba, Masoud Djuma, jana alionekana kumuandaa Salamba ili awamalize Gor Mahia katika mchezo wao fainali.

“Katika mchezo uliopita dhidi ya Kakamega, nilimpa nafasi ya kucheza kidogo kutokana na kutokuwa na wenzake kwa muda mrefu, lakini hata hivyo ameonyesha ni mchezaji mzuri.

“Kwa jinsi nilivyomuona, naamini katika mchezo wa fainali ataweza kutusaidia kwani anaonekana ni mchezaji mzuri,” alisema Djuma ambaye wiki ijayo atakabidhiwa Simba akisaidiwa na Seleman Matola.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV