June 3, 2018






Na Saleh Ally
WAKATI mwingine ambao mashabiki wa soka wamekuwa wanausubiri kwa hamu sana, huu ni ule wakati wa usajili ambao wachezaji nao huusubiri kwa hamu hata kuliko mashabiki.

Usajili una faida kubwa kwa wachezaji zaidi hasa kwa wale ambao walifanya vizuri katika msimu unaokuwa unamalizika na mikataba yao ikawa imeisha au wana uhakika wa kuuzwa kutoka timu ndogo kwenda kubwa.

Wakati neema kubwa inakuwa ni kwa wachezaji hasa waliofanya vizuri, kunakuwa na burudani pia hofu kubwa kwa makundi mawili. Kwanza ni kundi la viongozi na pili lile la mashabiki.
Makundi haya yanakuwa na hofu kwa aina tofauti kabisa ya mwenendo. Viongozi wanajipambanua kuwa wao ni walinzi wa wachezaji wanaotakiwa kubaki au wale tegemeo katika klabu zao, ni lazima kuwalinda ili wahakikishe wanabaki na kuendelea kuwa msaada.

Suala la kuwalinda si dogo, si jambo la mzaha na hasa kwa wachezaji wanaokuwa wamefanya vizuri. Wanaweza kununuliwa au kuamua tu kuondoka.

Maana yake kiongozi anakuwa katika presha ya juu pale dirisha linapofunguliwa na itashuka baada ya kufungwa. Haiwezi kuwa kazi rahisi maana inataka maandalizi na hasa kifedha. Kuwabakiza wanaotaka kuondoka kwa kusaini nao mikataba mapema na kadhalika.

Kwa mashabiki, presha yao ni ushabiki. Hufurahia kuona wamenasa nyota wapya lakini huwa na presha ya juu pale inapotokea kuna timu ina fedha zaidi na kuchukua wachezaji kila sehemu.

Mashabiki wasingependa kuona wachezaji nyota na vipenzi vyao wanaondoka katika timu na kwenda nyingine. Ikitokea hivyo lawama na presha yote huelekeza kwa wachezaji wenyewe kwamba wana tamaa, pia viongozi kwamba wameshindwa kuwalinda.

Mashabiki hawajali kwamba wachezaji nao ni wanadamu na wanakuwa na ndoto zao. Hivyo hutaka watimize kile ambacho kinawafurahisha wao.
Wakati hii presha inakuwa kubwa, mwisho imekuwa ikitibua mambo mengi sana. Katika usajili mara nyingi tumeona viongozi wakisajili kwa kutaka kuwafurahisha mashabiki badala ya kuangalia kocha au benchi la ufundi linasema nini.
Kwa kuwa presha mwisho huishia kwao, viongozi huifanya kazi hiyo kwa presha na wakati mwingine inawezekana kiongozi wa Yanga angeweza kumsajili mchezaji mwenye kiwango kizuri kutoka Stand United ya Shinyanga. 
Lakini kwa kuwa amelenga kuwafurahisha mashabiki, basi atachukua mchezaji kutoka Simba hata kama mahitaji ya kocha yanaonekana yule wa Stand ni bora zaidi.
Hii inaweza kutokea kwa Simba pia, kutaka kuchukua mchezaji wa Yanga ilimradi kuwafurahisha mashabiki wao kwamba wanaibomoa Yanga au wanalipa kisasi. Hii si sayansi sahihi ya kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu unaofuata.
Usajili maana yake ni kuboresha au kuimarisha. Usajili maana yake kuwa imara zaidi kuliko msimu huu kwa ajili ya msimu ujao.
Suala la usajili si la kishabiki. Lazima tukubaliane, usajili ni hesabu za kitaalamu ambazo zinapaswa kutekelezwa sahihi ili kufikia lengo ambalo lilikuwa linatakiwa kufikiwa.
Mnaweza msikubali lakini viongozi mnajua mnavyokuwa na furaha mnapopata mchezaji kutoka timu pinzani hasa ile ambayo mna ushindani nayo kwa kuwa huona mmetengeneza kero upande wa pili na kujenga furaha upande wenu, hizo ni siasa.

Vizuri kuachana nazo na kikubwa iwe kulenga mafanikio kwa ajili ya msimu unaofuata na hakuna kitakachofanya utaratibu huo ufuatwe bila ya kufuata kile anachotaka kocha na benchi la ufundi.

Benchi la ufundi, lazima litaundwa na wataalamu. Tukubaliane wataalamu ni watu wanaofanya mambo yao kwa hisabati. Hivyo ni sahihi zaidi kuwafuata wao badala ya mioyo ya mashabiki au viongozi.

Tumeona mara nyingi mmepotea katika kipindi cha usajili kwa sababu mlitaka kufuata matakwa ya mioyo yenu au mioyo ya mashabiki na wanachama wenu. Hili limekuwa kosa la miaka nenda rudi na sasa ni wakati mwafaka wa kulirekebisha na kutuonyesha mnaelewa maana ya sayansi ya mpira.



1 COMMENTS:

  1. Wachambuzii wengiiii hawajui mpira na baadhi ya makocha wanabaka fani..
    Mi sio shabiki wa Soka la bongo ila nafatilia Soka la bongo.

    Mfano. Msimu uliopita simba imekuwa ikiteseka mnooo inapowakosa boko au okwi na ikiwakosa kwa pamoja ndo tatizo zaidi.
    Usajili iliyoufanya mbaka sasa 100% good.kwa sabu MTU kama salamba ni aina ya boko pure no 9 na kama atajituma atakuja saidia taifa.bonivenja...100% good ndo aina ya kinaokwi so wanapochoka kinaokw wakuwarithi wanaonekana .rashid 100% safi kabsaa tena kocha atakuwa na upana wa kuchagua. Tena ningekuwa kweny bench ningeshauri tupate no 9 mngine mwenye uzoefu ya boko tena ..zen turudi kuangalia nyuma na katika ti.
    Usajirii mzurii simba tena wakitaaram.
    Hata azam usajiri Wao unaonekana unaleta kitu.
    Ila singida kidoogoo napata wasiwasi ingawa wana macho mazuri kwenye kupoint mchezaji ingawa not 100%

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic