June 3, 2018






NA SALEH ALLY
Ninapata bahati kubwa ya kukutana na mashabiki wa karibu kila timu ingawa kokote uendako, mashabiki wa Yanga na Simba ndiyo wengi zaidi.


Wengi ninaokutana nao tunabadilishana mawazo, wapo wanaosema hili na wengine lile. Hakika nafurahia maisha haya kwa kuwa michezo ni sehemu ya maisha yangu kwa asilimia kubwa.


Wengi ninaokutana nao huwaomba wawe huru ili nijue walichonacho na kuweza kujifunza zaidi. Wamekuwa wakifanya hivyo, kweli ninashukuru kwa kuwa nimekuwa nikijifunza sana kutokea kwao ambalo ni jambo zuri sana.


Hivi karibuni, mashabiki wengi wa Yanga wamekuwa wakizungumzia suala la benchi la ufundi na kinachonishangaza sana ni ile kauli ya kutaka kuona wachezaji wa zamani wa timu hiyo wanaondoka katika benchi la ufundi.


Wengi wa mashabiki hao wamekuwa wakitaka kuona Shadrack Nsajigwa ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi na kocha wa makipa, Juma Pondamali wanaondoka Yanga.


Wanawataka waondoke kwa kuwa wanawaona ni tatizo ndani ya kikosi chao. Hivyo kama wataondoka Nsajigwa na Pondamali, basi kwao litakuwa jambo zuri.


Kuondoka kwa Pondamali na Nsajigwa inawezekana, pia ni uhakika wataondoka hapo na hawatadumu milele, sote tunajua. Lakini ninachoona, huenda wakati huu, Yanga wanawahitaji zaidi Pondamali na Nsajigwa kuliko ilivyokuwa hapo awali.



Mazungumzo na mashabiki wengi wa Yanga, nimegundua wanaotaka Nsajigwa na Pondamali waondoke, hawana taarifa za kutosha na huenda ni watu wanaojazwa maneno na wao wakayachukua kuyasambaza.


Inawezekana kabisa kuna mtu ana matatizo yake binafsi na Nsajigwa au Pondamali, hivyo anajaribu kutafuta njia ya kuwakomoa au kutimiza nia yake ili kujifurahisha.


Wengi wa mashabiki wanaotaka Pondamali aondoke, wanasema wamechoshwa, wachache wamenipa sababu ya ajabu kabisa. Mfano Pondamali wamemchoka tu kwa kuwa makipa wanaonekana hawana viwango vizuri na baadhi wakisema Nsajigwa alimfanyia mabadiliko Kamusoko katika mechi moja wakati akijua anategemewa!



Waungwana, Kamusoko amekuwa akicheza wakati akiwa mgonjwa au hajapona vizuri. Nsajigwa anayajua matatizo ya wachezaji wake kuliko sisi, huenda alitakiwa kufanya hivyo na daktari au ni masuala ya kiufundi.

Hivi ni kweli Nsajigwa aondoke kwa kuwa tu alimtoa Kamusoko? Kwa nini tunazungumza maneno yasiyo na nguzo na badala yake tunakubali kuwa bendera fuata upepo kwa kushirikiana na maneno ya kusikia bila ya kuwa na uhakika?


Kiwango cha Rostand kimeshushwa na Pondamali? Nani anaweza kusema Rostand alikuwa bora akiwa African Lyon na sasa ameshuka? Kama ni kweli, tujiulize wangapi wamefundishwa na Pondamali na waliisaidia Yanga?


Tukumbuke, Pondamali anaweza akawa na upungufu wake kama mwanadamu, lakini niwakumbushe, makipa wake walichukua ubingwa mara tatu na kuwafanya Wanayanga kujiamini na kuishi kwa furaha kuu.


Anaweza akawa anaongeza ujuzi kila baada ya muda fulani. Ufundishaji unabadilika, lakini hadi sasa ameonyesha anaweza kufanya kazi yake vizuri, basi aungwe mkono.


Kumbukeni Pondamali na Nsajigwa ni wazalendo na wanafanya kazi yao katika mazingira magumu sana. Kati yenu hakuna amewahi kuwatetea kwamba wanastahili kulipwa fedha zao.


Angalia wachezaji wanagoma, wanaondoka wanakwenda wakirudi wanawakuta. Haujawahi kusikia Pondamali au Nsajigwa wakilalamika kutokana na kucheleweshewa fedha zao kwa misimu mitatu.


Wanaijua Yanga, kwao ni nyumbani. Wanazijua shida za Yanga, watakuwa wako tayari kusaidia ili mambo yaende sawa na walipwe baadaye. Kumbukeni makocha wengine wamekimbia kutokana na kutolipwa kama wao, wanaendelea tu.


Nawakumbusha kuna wachezaji walisusa lakini wakawakuta Nsajigwa na Pondamali bado wanaendelea. Kwao inakuwa rahisi kwa kuwa Yanga ni kazini na pia sehemu yalipo mapenzi yao.


Wanaweza kuondoka, lakini vizuri wakapewa heshima na thamani yao. Kati yenu hakuna aliyewalilia na kuwapigania kupata haki yao. Wao wameonyesha heshima kwa kuendelea kufanya kazi bila ya malalamiko hadharani.


Tuache kuona kila mzalendo ni sahihi kumdharau au kuamini hajui. Tunaweza kukosoana lakini pia ni vizuri kupima badala ya kila unaloambiwa basi unachukua na kuliona ni sawa.


Binafsi naona mnaowaonea Pondamali na Nsajigwa kwa kuwa mnaona ni wazalendo, mnaona ni wa hapahapa na mmesahau hata walivyoipigania Yanga wakiwa wachezaji na sasa makocha.

Kufanya vibaya kwa Yanga kwa sasa, kila mmoja wetu anajua kwamba si suala la makocha hao. Ni ukata na ikiwezekana mumtafute aliyesababisha ukata kutawala na si wao.




1 COMMENTS:

  1. hili ni wanachama wenyewe ndio wenye matakwa na maamuzi ya mwisho

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic