June 12, 2018




NA SALEH ALLY
JUZI Jumamosi kulikuwa na mechi ya kirafiki ya burudani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, pale vikosi vilivyoongozwa na mwanasoka maarufu nchini, Mbwana Samatta na msanii maarufu, Ally Salehe Kiba maarufu kama Alikiba vilipopambana.

Mechi hiyo ilipewa jina la Nifuate na ilikuwa na malengo mawili makubwa, kwanza kuburudisha na kudumisha umoja, pia kuchangia elimu.

Samatta na Kiba waliamua kuchangia elimu kwamba kwa kile kitakachopatikana kitumike kwa ajili ya kuchangia elimu nchini. Wanajua wenyewe watapeleka katika shule gani, lakini watakapopeleka ninaamini watakuwa wamechangia elimu.

Nilielezwa wanaweza kupeleka katika shule walizosoma, bado naona ni jambo zuri kwa kuwa watakuwa wamehamasisha mambo mengi kwa wakati mmoja kwa watoto wanaosoma.

Watakapopeleka fedha hizo, basi watasaidia mambo muhimu. Ingawa bado ninaona wangeweza kununua mahitaji yanayohitajika na kupeleka ili kuweka uhalisia wa mambo.

Pamoja na hilo kwa watoto wanaosoma katika shule hizo, watakapowaona watu kama Samatta na Kiba wakienda katika shule hizo, basi watahamasika na kujua kwamba hata wao wanaweza.

Wataona wanaweza kwa kuwa kama Samatta au Kiba alisoma shule anayosoma yeye, leo ni mtu maarufu na mwenye mafanikio basi bila shaka na yeye atakuwa anaweza. Hivyo kama kuna sehemu walikwama, watafanya kila linalowezekana kujitutumua na kuamka upya ili wapambane.

Mwisho watoto hao pia wataanza kutamani kutimiza ndoto ya siku moja kurejea shuleni hapo na kusaidia kama ambavyo wamefanya Samatta na Kiba, jambo ambalo litawabadilisha na kusoma kwa juhudi na kama wana kipaji, basi watataka kukiendeleza hasa.

Kwa kifupi, naweza kusema walichokifanya Samatta na Kiba, pia wale watu waliowasaidia kufanya maandalizi ni jambo zuri na linapaswa kuigwa. Kikubwa cha kwanza nishauri, Samatta na Kiba wasiishie hapo na matarajio yetu makubwa ni kuona mwakani mechi hiyo inaendelea na watoto wanaendelea kuchangiwa.

Samatta na Kiba, tuseme kama ndiyo wameanzisha, wamewafungua nyota wengine katika tasnia mbalimbali kwamba kuna mambo huenda waliona hayawezekani, kumbe yanaweza kufanyika na kukawa na faida kubwa.

Nani anaweza kuwa maarufu bila ya kushirikiana na jamii. Kama unajulikana, unajulikana na kina nani? Kama una mashabiki, hao mashabiki ndiyo jamii yenyewe.

Hivyo, jamii inahitaji kuona inapata kitu kutoka kwako hasa kama inakuunga mkono na kukupa nafasi ya kuitwa nyota au maarufu. Vitu hivi vimekuwa vikifanyika katika nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo katika michezo au burudani, sasa Samatta na Kiba wameanzisha hapa nyumbani na huu uwe mwanzo mzuri.

Isitokee kuna mtu anataka kufanya jambo zuri huenda kama hili au zaidi ya hili aone haya kwamba ataonekana ameiga hivyo arudi nyuma na kuachana nalo. Kunapokuwa na jambo zuri, si vibaya kuiga au kulifanya kwa faida pia.

Suala hili si ushindani, badala yake kurudisha kwa jamii ni muhimu na kila mmoja anaweza kufanya. Jamii unayoitegemea, lazima kuijali na kuionyesha upendo na hasa kama umefanikiwa kupata nguvu na nguvu yako ni hiyo jamii, basi ni jambo jema sana kuipa kitu.

Kama kuna mtu atakuwa anaweza kubuni jambo lingine linalofanana na hilo kwa faida ya jamii, pia litakuwa bora zaidi ili kuweza kusaidia kwa kuwa tukubaliane. Kama Serikali itaachiwa ifanye kila kitu, basi mwisho tutaishia kuilaumu tu.

Hivyo wanaokuwa na nafasi kama hii, basi wafanye mambo ambayo yatakuwa na msaada na kuinua mioyo ya waliokata tamaa.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic