June 12, 2018




 


NA SALEH ALLY, NAKURU
UKIZUNGUMZIA wachezaji kutoka Bara la Afrika waliocheza mechi nyingi na kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu ya England, basi Yakubu Aiyegbeni ni kati ya waliofanya vizuri zaidi.

Yakubu, raia wa Nigeria, amecheza zaidi ya timu tano za England na zote alifanya vizuri huku kwa muonekano akiwa ni kama mchezaji asiye na nafasi ya kufanya vizuri.

Mpira wake haukuwa wa mbwembwe, Waingereza wanasema “direct football”, mtu ambaye anachotaka ni kutimiza malengo na kufanya kilicho sahihi. Hakuwa akijali kufurahisha, kwa kuwa ni mshambuliaji, yeye alichotaka kufunga tu na kweli alifanikiwa.

Hadi anamaliza kucheza soka la kulipwa, Yakubu alifunga mabao 172, kati ya hayo zaidi ya 100 akiwa ameyafunga nchini England akizitumikia timu mbalimbali.

Alitokea katika Klabu ya Julius Berger kwenda Gill Vicente kwa mkopo na huko akauzwa Maccabi Haifa ya Israel alikofanikiwa kufunga mabao 24 katika mechi 49, nao wakampeleka kwa mkopo Hapoel Haifa Saba ambako ndani ya mechi 23, akafunga mabao sita. Wao wakampeleka England katika Klabu ya Portsmouth ambako maisha yake yalianza England.

Akiwa England, aliifungia Portsmouth mabao saba katika mechi 13, haraka wakaona anafaa na kuamua kumsajili rasmi na maisha yake England yalianza na huko baadaye alizichezea timu za Middlesbrough, Everton, Leicester City, Blackburn Rovers na baadaye Reading na Coventry City za daraja la kwanza.





Yakubu yupo hapa nchini Kenya ambako ameletwa na Klabu ya Everton kupitia wadhamini wake SportPesa kwa ajili ya programu ya Kit For Africa ambayo hutoa vifaa na mafunzo kwa watoto wa Kiafrika.

Katika mahojiano maalum yaliyofanyika na Global Tv Online na baadaye Gazeti la Championi, Yakubu anasema yako mengi ambayo yanawezekana Afrika lakini kumekuwa hakuna njia sahihi ya kuyainua.
“Kuna mambo mengi yanawezekana lakini tumeamini hayawezekani ndiyo maana hayawezekani kweli.

“Kama ningeamini kwangu haiwezekani, leo nisingekuwa hapa. Nilicheza mpira bila viatu hadi nikiwa na miaka 12, sikuwahi kuacha na niliamini licha ya kuwa sina uwezo wa kununua viatu bado ningeweza kufanikiwa. Baadaye kaka yangu alininunulia viatu,” anasema na kuendelea.

“Vile viatu kwangu ilikuwa ni kama maisha mapya, niliona nimekuwa mpya zaidi, niliamini ninaweza zaidi na ulikuwa wakati mpya na tokea siku hiyo sikuwahi kuvunjika moyo maana niliona kama niliweza bila viatu, sasa ninavyo, nitashindwa nini!

“Ndiyo maana pia unaona tunafanya Kit For Africa. Lengo ni hilohilo, kuwahamasisha watoto wa Afrika, waamini inawezekana kwa kuwa wamekuwa wakivunjwa moyo na umasikini na hii inasababisha mioyo yao kukata tamaa.”

Kwa sasa Yakubu ni shujaa wa Everton inayodhaminiwa na SportPesa, ni kati ya wachezaji wanaopewa heshima ya ‘wakongwe wa heshima’. Sasa anatumika kama balozi wa klabu hiyo sehemu mbalimbali duniani.

Akiichezea Everton tangu 2007 hadi 2011, alicheza mechi 82 na kufunga mabao 25. Katika historia yake ya soka, Everton ndiyo klabu aliyoichezea mechi nyingi zaidi na ni kati ya timu tatu alizofunga mabao mengi zaidi ambazo ni Everton, Portsmouth na Middlesbrough.


Pamoja na vijana kuhamasishwa, Yakubu anaamini Afrika inahitaji kuwa na walimu waliofunzwa, walimu ambao wanapewa nafasi ya kujua nini cha kufanya kuhusiana na watoto.

“Kumfundisha mtoto, si kazi rahisi na kunakuwa na tofauti kubwa na wakubwa. Lazima kuwe na walimu waliopata mafunzo sahihi katika upande wa watoto.

“Kits For Africa inaweza kusaidia kuinua mioyo yao, lakini bado wanatakiwa makocha wao kuendeleza kazi hiyo na kuwaonyesha inawezekana. Haliwezi kuwa jambo la siku moja kwa kuwa si kitu kinachowezekana ili mradi tu.”

Kuhusiana na suala la yeye kufanikiwa, Yakubu anasema haikuwa rahisi hata kidogo kama watu wanavyofikiri. Ni lazima kupitia maumivu ya kila namna kufikia hapo.

“Haikuwa kazi rahisi, ni ngumu na inahitaji mtu aliyeamua kufanya vizuri na kufikia anapopataka. Lazima kuna vipingamizi vingi, kukatishwa tamaa lakini hautakiwi kuacha.

“Kwa umri mdogo, inatakiwa kuwa na watu wanaoweza kukuongezea nguvu na kukuambia kuwa inawezekana kama ambavyo unaona tunafanya kwa watoto katika Kits For Africa.

“Lakini unapokuwa, inabidi upigane mwenyewe bila ya kuchoka. Unapotolewa kwa mkopo inakuwa ni kama kushushwa, lakini usiache, pigana tena na tena ili kufanya vizuri badala ya kukata tamaa.”

Pamoja na mafanikio upande wa klabu, Yakubu atakumbukwa sana kwao Nigeria wakati akiichezea timu ya taifa ya nchi hiyo, Super Eagles alipofunga mabao yaliyoipeleka Kombe la Mataifa Afrika na baadaye Kombe la Dunia.

Aliwahi kuwa nahodha wa Nigeria ambayo   aliitumikia  tokea mwaka 2000 hadi 2012 akifunga mabao 21 katika mechi 57 na kuwa mmoja wa wachezaji waliofunga mabao mengi zaidi katika kikosi hicho.

Bado anakumbukwa kwa kukosa lile bao dhidi ya Korea Kusini lango likiwa wazi katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka 2010.

“Sijaacha kukumbuka, ni jambo ambalo halitoki kichwani. Lakini mpira lazima utakuacha na kumbukumbu ya mambo mazuri na yale ambayo usingependa kuyakumbuka hata kidogo.”







0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic