August 20, 2018


Baada ya kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Mtibwa Sugar, kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, ametamba kuwa huo ni mwanzo, hivyo wamepanga kutwaa mataji yote ya makombe watakayoshiriki msimu huu.

Simba imefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuwafunga Mtibwa Sugar mabao 2-1 juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Katika mchezo huo, mabao ya Simba yalifungwa na Mnyarwanda, Meddie Kagere na Hassani Dilunga huku lile la Mtibwa Sugar likifungwa na Kelvin Sabato.

Kichuya alisema kuwa hakuna kitakachoshindikana kwao kutokana na ubora wa kikosi chao na morali iliyopo kwa wachezaji.

Kichuya alisema, Ngao ya Jamii waliyoipata itakuwa mwanzo mzuri kwao katika kuelekea msimu mpya wa ligi, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi keshokutwa Jumatano.

“Nianze kwa kuwashukuru mashabiki wa Simba kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kutupa sapoti ambayo imetuongezea morali ya sisi kupambana na kupata matokeo hayo mazuri.

“Kikubwa mashabiki wetu wasiache kujitokeza uwanjani kwa ajili ya kutupa sapoti na tunawaambia hatutawaangusha tukielekea katika msimu mpya wa ligi ambao hatuachi kitu, tumepanga kuchukua makombe.

“Tumeanza na Ngao ya Jamii, hivi sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye ligi huku tukijiandaa na mashindano mengine yanayokuja,” alisema Kichuya.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic