Siku chache tangu Cristiano Ronaldo atue ndani ya Juventus, straika Gonzalo Higuain, amepishana naye kwa kuwa ameamua kuelekea AC Milan.
Hadi jana mchana dili hilo lililokuwa katika hatua za mwisho kukamilika ambapo pia litamhusisha beki Leonardo Bonucci wa AC Milan ambaye anaelekea Juventus baada ya kudumu Milan kwa msimu mmoja.
Maelfu ya mashabiki walikusanyika kwenye hoteli ambayo Higuain alifikia jijini Milan kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya kabla ya kukamilisha dili la usajili, wote walikuwa wakimshangilia.
“Ni jambo zuri kuona mashabiki wengi kiasi hiki, pia nataka kuwashukuru mashabiki wa Juventus ambao walikuwa na mimi muda mwingi,” alisema straika huyo.
Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri na mwenyekiti wa klabu hiyo, Andrea Agnelli walinukuliwa wakisema watafanya jitihada zote kuhakikisha Ronaldo anapata huduma nzuri uwanjani ili ang’are, hivyo usajili wa Higuan umewashangaza wengi.
Higuain alisajiliwa na Juventus mwaka 2016 kwa pauni 79m baada ya kufunga mabao 36 katika Serie A ndani ya msimu mmoja kabla ya hapo alipokuwa Napoli. Kuondoka kwake kunaweza kuwavuruga mashabiki wengi wa Juventus ambao waliamini sasa kazi imeanza kwao.
Higuain ambaye ana umri wa miaka 30 ameshinda taji la Serie A na Coppa Italia katika misimu mwili aliyokuwa Juventus, amefunga mabao 55 katika mechi 105 za michuano yote.
Bonucci aliichezea Juventus kwa miaka saba, akiisaidia kushinda mataji sita ya Serie A kabla ya kujiunga na AC Milan kwa pauni 35m, mwaka jana, sasa ni kama anarejea nyumbani.
0 COMMENTS:
Post a Comment