Na Saleh Ally
HIVI karibuni nilikuwa nazungumza na Kamanda wa Polisi wa mkoa mmoja kuhusiana na namna ambavyo tunaweza kusaidiana kuwaondoa vijana wa eneo lake katika wimbi la unywaji wa pombe kupindukia.
Niliamua kufanya hivyo baada ya kugundua eneo hilo limetwaliwa na pombe kali za kienyeji ambazo zimewafanya vijana washindwe kushiriki shughuli za maendeleo na badala yake kuendelea kuishi maisha ya kubahatisha na wengine kuwa wezi.
Maana kila wakiamka ni kwenda kunywa pombe na sasa yamekuwa ndiyo maisha yao. Alikubaliana nami na tumeanza kushirikiana kuhakikisha inafanyika michuano ya soka itakayowandoa kwenye mawazo hayo potofu.
Kabla ya hapo, nilifika ofisini kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye tulizungumza mengi ikiwa ni pamoja na kumuahidi ushirikiano katika mambo ya kuungana naye pamoja na wizara yake kuhakikisha tunaelimisha katika mambo mbalimbali kupitia vyombo vyetu ili kuwasaidia walinzi wetu kama askari polisi na kadhalika.
Pamoja na hayo, bado kuna askari polisi wanaonekana wamekuwa wakiamini waandishi ni adui zao na wanatamani hata kuwapiga tu ili kuridhisha nafsi zao.
Askari hawa, kama utafanikiwa kuwafikishia ujumbe, wamekuwa wakitaka kutumia maovu au upungufu wa weledi wa kazi zao kusingizia mwandishi amelitukana jeshi, jambo ambalo naliona ni ukosefu wa hoja na kushindwa kujitambua wako wapi na wanatakiwa kufanya nini.
Juzi, Mwandishi wa Habari wa redio ya dini ya Wapo ameshambuliwa na askari polisi zaidi ya wanne, akapigwa hadi akazimia wakati akiwa katika majukumu yake ya kikazi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hakika hili suala la waandishi wa habari kuonewa na polisi limekuwa sugu na inaonekana kama tumekosa mtetezi kwa kuwa hakuna anayeamini waandishi ni muhimu hadi itakapotoka sauti wa kiongozi wa juu.
Mwandishi yule alipigwa akidaiwa alimsukuma Polisi, lakini waandishi wengi waliokuwa pale walieleza kwamba askari aliyekuwa amevaa kiraia wakiamini hakuwa katika akili yake vizuri kutokana na kinywaji alianza kuwasukuma.
“Tusingejua kama ni askari na alitokea nyuma yetu wakati tukiomba kuingia kufanya mahojiano. Tulikuwa tumezuiliwa na askari polisi wakati siku zote huwa tunapita pale. Alitokea kwa nyuma na kuanza kutusukuma na ilionekana amelewa, katika kumtoa mikono asitusukume, akadai amesukumwa. Akawaita wenzake waje nao wakaanza kumshambulia mwenzetu hadi akazimia,” alinieleza mmoja wa waandishi wa redio na baadaye mwandishi wa gazeti la Championi.
Ukiangalia picha yule mwandishi na umbo lake akishambuliwa na askari zaidi ya watatu unaweza kushangaa. Maana hana silaha, hakatai alichoelezwa lakini anaendelea kupigwa na ilikuwa hivyo hadi alipozimia.
Baada ya kuzimia walimbeba na kumtupia katika karandinga hadi hapo waandishi waliposhitaki kwa Waziri Lugola ambaye aliagiza aachiwe.
Hakika hii ni aibu, hili si jambo jema na namuomba Waziri Lugola alifanyie kazi hili kwa kuwa linaonekana kuwashinda wengi na ninachokiona askari wengi wanaokwenda uwanjani huenda kuangalia mpira na kuwalinda waandishi wa habari.
Nasema hivi kwa kuwa hata siku Waziri Lugola akiwa uwanjani, shabiki aliwapita askari waliokuwa wakiangalia mpira na kwenda kumvaa Emmanuel Okwi katikati ya uwanja. Kabla ya wachezaji wa Simba hawajaingia uwanjani, wao walikuwa wamekaa wanaangalia wachezaji wanaotoka badala ya kulinda usalama.
Kuna upungufu mkubwa kwa kuwa wengi hawajui sheria za uwanjani. Mfano, waandishi wenye vitambulisho vinavyotambuliwa na TFF, wanakataliwa kuingia kwenye eneo ambalo lina vyumba maalum vya waandishi na mikutano yao. Sasa watamruhusu nani?
Askari mmoja wa kike anaonekana kwenye video akisema wameambiwa asiingie mtu hata waandishi na hatoi sababu! Ajabu zaidi anamkataza mwandishi kupiga picha.
Jiulize, kweli unakatazwa kupiga picha kwenye Uwanja wa Taifa. Sasa hii picha ipigwe wapi? Kweli askari anayekataza analitambua hili, au anaamini kusema tu ni sahihi?
TFF nayo ipo kimya, imebaki kupanga tu na wahariri lakini utekelezaji umekuwa ni duni na hii nayo inaonyesha dharau kubwa kwa waandishi wa habari ambao wamekuwa msaada mkubwa kwenu.
Kuna haja ya waandishi kuamka na kuanza kusema ukweli. Msiendelee kuwa wanyonge mkiwa mnaumizwa kila siku na wala hampaswi kuwa na chuki na askari wote kwa kuwa wako wachache wasioijua kazi yao ndiyo wamekuwa wakifanya hivyo na mwisho kusababisha chuki baina ya askari na polisi, hapa muwe makini sana.
Lakini kama waandishi na vyombo vya habari, tunapaswa kuonyesha hadharani wale ambao wamekuwa wakiwaonea waandishi na kutaka waanze kuona kazi ya uandishi ni hatari tena ndani ya nchi hii, jambo ambalo si sahihi na halipaswi kupewa nafasi.
Waandishi wanaokwenda viwanjani wapewe mafunzo, wajue waandishi wanatakiwa kupita wapi na wapi ili nao wafanye kazi zao. Siyo kwa sababu askari ana uwezo wa kuzuia, basi azuie kila kitu ili mradi bila ya kujali.
Kama askari wanataka kuheshimiwa wafanye kazi zao, basi bao wanapaswa kuheshimu kazi za wengine kwa kuangalia mipaka.
Watu wanajitokeza kwa wingi viwanjani kupitia vyombo vya habari. Waandishi hudharauliwa baada ya kufanya kazi nzuri ya kuita watu viwanjani na ujio wa watu wengi na askari nao wanapata kazi ya kulinda. Kama waandishi wasingeita watu viwanjani, askari wangewalinda akina nani?
Hivyo ni vizuri mkaacha hili na Waziri Lugola, tafadhali tusaidie kwa kuwa tuendako ni kubaya na kuna siku utatokea msiba na hasa upande wetu sisi waandishi. Maana kadiri siku zinavyosonga mbele, mambo yanazidi kuwa mabaya na wahusika hakuna wanachobadili.
Waandishi wa habari.. Mnashindwa nini kuonesha uwezo wa nguvu mlizo nazo..
ReplyDeleteKama hamjuhi ngoja niwafunde jinsi ya kufanya..!!
Susieni habari za PT kwa muda usiojulikana..!
Susieni kabisa... Wamepigwa wao susieni.. Wamekamata wezi/majambazi susieni..
NDIYO NASEMA SUSIENI HABARI ZAO
Na matokeo yake mtayaona.. Mtaitwa.. watataka mkae chini na uongozi wa PT (Piga TU) na MTAOMBA KUYAJENGA na kuweka misingi imara ya baadaye..!!
Mjumbe apigwi.. Mjumbe auwawi..!! Why sisi PT wanawaburuza tu watakavyo..??
Bg up brother kwa kaz nzurii
ReplyDeletewako askari wa aina hii wengi sana jitahidini kuwasafisha kinidhamu pamoja na kutohudhuria viwanja vya michezo
ReplyDelete