NGOMA AANZA TIZI GUMU LEO BAADA YA KUMALIZA DOZI
Mshambuliaji mashine wa Azam FC, Donald Ngoma, raia wa Zimbabwe, leo Jumatatu kwa mara ya kwanza ameungana na wachezaji wenzake kwa ajili ya kuanza mazoezi ya kugusa mpira ikiwa ni baada ya kumaliza programu maalumu ya gym ambayo alikuwa anafanya.
Ngoma amekuwa majeruhi kwa muda mrefu tangu akiwa Yanga ambayo ilivunja mkataba wake kabla ya kusajiliwa na Azam FC.
Mzimbabwe huyo anasumbuliwa na tatizo la goti ambapo baada ya kutua Azam alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa vipimo zaidi.
Kwa mujibu wa Championi, Meneja wa Azam FC, Phillip Alando, amesema kuwa kuanza kufanya mazoezi magumu kwa straika huyo, kumeibua matumaini kwa benchi la ufundi la timu hiyo likiongozwa na Mholanzi Hans van Der Pluijm kuwa wanaweza kumtumia kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi dhidi ya Mbeya City.
“Ngoma kesho (leo Jumatatu) ndiyo ataungana na wenzake rasmi na kuanza kufanya mazoezi magumu, ameruhusiwa hivyo ikiwa ni baada ya kumaliza programu maalum ya gym pamoja na kukimbia ambayo alipewa ili aweze kurejea kwenye hali yake ya kawaida.
“Jambo hilo la kurejea limeamsha furaha kwa benchi la ufundi kwani wameona wanaweza kumtumia mshambuliaji huyo kwenye mchezo wetu wa kwanza wa ligi dhidi ya Mbeya City,” alisema Alando.
0 COMMENTS:
Post a Comment