AFYA YA SINGIDA UNITED, INA UTATA
Na Saleh Ally
KLABU ya Singida United imekuwa mfano wa kuigwa ndani ya muda mfupi sana. Hakuna cha kujadili sana, bali ni kusifia kazi nzuri ya uongozi wake.
Uongozi wa Singida United umefanya kazi yake vizuri kabisa. Kwa maana ya kwamba, kumekuwa na mpangilio sahihi kwa wakati mwafaka.
Utaona namna ambavyo Singida United ilipanda daraja hadi kwenda kuwa timu tishio katika Ligi Kuu Bara na mwisho ikaishia fainali ya Kombe la Shirikisho. Ilibaki kidogo iweke rekodi ya kurejea ligi kuu na kuwa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.
Mtibwa Sugar ndio waliotibua baada ya kuwafunga katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) jijini Arusha.
Pamoja na kwamba ilikuwa imerejea ligi kuu, Singida United ilibadilika na kuwa timu kubwa sana. Lakini kwa sasa, mambo yanakwenda yanabadilika kwa haraka sana na mipango inavurugika.
Huenda ni vigumu kwa Singida United kusema kwamba mambo si mazuri lakini yanayojitokeza yanaonyesha kuna jambo ambalo si sahihi linaendelea ndani ya klabu hiyo.
Wachezaji kadhaa wameondoka Singida United na inaonyesha au inajulikana walikuwa wanategemewa.
Wako wamekuwa wazi na kuzungumza kwamba wanadai fedha au kuna deni hawajalipwa na kuondoka kwao kunatokana na kudai bila ya mafanikio. Hii imewafanya kuwa na jazba na kuamua kujiondoa.
Wako waliondoka wakapata timu, wako walioondoka wameamua kubaki nyumbani tu. Lakini wanataka kuonyesha hisia zao za kuchoshwa na hali inayoendelea.
Walioondoka Singida si kwa kutaka au wamelazimika kutaka ni pamoja beki wa kushoto, Shafiq Batambuze raia wa Uganda, ambaye ameenda Gor Mahia ya Kenya. Kipa Peter Manyika, taarifa zinaeleza karejea kwao Dar, huenda atajiunga na Singida mambo yakikaa sawa siku yoyote.
Jamal Mwambeleko naye kuna taarifa kachoka, kaona akatafute maisha Kenya. Kuna hali fulani ya malumbano ilitokea, ikapozwa juu kwa juu.
Beki Miraji Adam ilielezwa alikutana na hali hiyo, kaamua kutafuta maisha nje ya Tanzania.
Pia kuna Kazungu Mashauri naye aliondoka, inawezekana karejea kama kuna maelewano basi huenda akarejea. Kwa kifupi hii si afya njema kwa Singida United.
Jambo hili linaweza kuonekana kama ni la kawaida na kama watakuwa wamezidiwa kifedha, Singida United wanahitaji kujipambanua kuhusiana na hali yao, halafu washughulikie.
Naamini si busara kuona wanakosea sana kutokana na kipindi walichonacho, basi vema wapewe ushauri na si kuzodolewa utafikiri wameingia katika matatizo kwa makusudi.
Pia niwakumbushe Singida United, kwamba matatizo yanaweza kutokea wakati wowote. Lakini matatizo pia yapo ya kujitakia kama wanaona wanapita katika njia ya matatizo ya kujitakia, vema kujitambua mapema na kubadili gia angani ili kuokoa hali iliyopo sasa.
Wakati huu ni mzuri kuwang’amua viongozi sahihi wa Singida United. Kwamba wana uwezo wa kiasi gani kupambana na kutatua matatizo yao.
Matatizo ni sehemu ya kukua zaidi. Unapoingia kwenye matatizo, ukiyamaliza ni dalili za kukua zaidi kwa kuwa mengi yana mafunzo.
Ninaamini Singida watakuwa wamejifunza na tayari kuanza maisha mapya. Lakini kwa wachezaji pia wanapaswa kujua kama wakati wa raha walikuwa pamoja wanaweza kujaribu kurudi nyuma na kuangalia wanapoweza wakashirikiana kwa shida ili kusaidiana kuliendeleza gurudumu na siku nyingine, afya irejee tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment