October 19, 2018








NA SALEH ALLY
MARA ya mwisho, Tanzania ilicheza Kombe la Mataifa Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria. Inawezekana kabisa kwa asilimia 90 wote wanaocheza Lig Kuu Bara walikuwa hawajazaliwa.

Mwaka 1980, ni uhakika kabisa wanaocheza Ligi Kuu Bara na Zanzibar kwa sasa walikuwa hawajaanza hata darasa la kwanza. Maana yake imekuwa ni muda mwingi sana tokea Tanzania imeshiriki michuano hiyo.

Safari hii kuna ongezeko la timu zitakazoshiriki michuano hii kwa kipindi hiki maarufu kama Afcon. Badala ya timu moja, sasa ni timu mbili kutoka katika kila kundi la timu nne zitafuzu kwenda kucheza katika michuano hiyo itakayopigwa nchini Cameroon.

Tanzania ipo kundi moja na timu za Uganda, Lesotho na Cape Verde na hakika hakuna ubishi, Taifa Stars inastahili kufuzu katika kundi hilo ambalo si suala jepesi lakini lina timu ambazo Stars inazimudu.

Awali hakukuwa na umakini kama ambavyo Stars ilitoka sare na Lesotho nyumbani Tanzania. Tena mechi ikiwa imepelekwa kwenda kuchezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex na hakuna ubishi, hii ilikuwa ni sehemu ya kuonyesha kutojali sana mchezo huo ambao ilikuwa ni lazima kuhakikisha kila mechi ya nyumbani inaingiza pointi kibindoni.

Chini ya Kocha mpya, Emmanuel Amunike, Stars imefanikiwa kupata sare nchini Uganda, haikuwa kazi nyepesi na ilikuwa ngumu kweli. Lakini imeshinda nyumbani jambo ambalo lilikuwa linatakiwa hasa baada ya kupoteza Cape Verde huku timu ikionyesha kiwango kibovu.


Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde, umeamsha matumaini na Stars inatakiwa kufanya jambo moja ili kujiweka katika nafasi ya asilimia 95 kufuzu kucheza Afcon na kuandika rekodi mpya.

Jambo hilo ni ushindi tu. Stars inatakiwa kushinda mechi zake mbili, moja ya ugenini dhidi ya Lesotho na nyingine dhidi ya Uganda ambayo itakuwa nyumbani Tanzania. Sasa vipi inashindikana waungwana?


Binafsi ninaamini kama juhudi zitafanyika katika maandalizi bora na uhakika, kuondoa ushabiki na kuungana pamoja kuwa Watanzania tunaotaka jambo moja basi tuna uhakika wa kufanikisha hili.


Kuungana kutatengeneza nguvu kubwa sana, nguvu inayosambaa na kuifanya Tanzania kuwa imara kufikia lengo sahihi inalolitaka kulifikia. Tuache kuwa watu tusiokubaliana hata tunapotakiwa kuungana.

Hata kama tutaungana, bila ya Serikali ya Tanzania au ya Watanzania kuwa pamoja katika hili, basi hakutakuwa na nafasi ya kulifanikisha. Kuna kila sababu ya viongozi wa Serikali kukumbuka, ushindi wa Taifa Stars ni ushindi wa taifa na Serikali inapaswa kushiriki kwa vitendo, hatua kwa hatua, mguu kwa mguu, jino kwa jino hadi mwisho wa safari hii.


Nimekuwa nikimuona Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akishiriki. Hili ni jambo jema ingawa mimi naona ushiriki huo unaweza kuongezwa kwa kiwango zaidi cha kutosha hasa katika uhamasishaji.
Motisha kwa wachezaji, motisha kwa mashabiki na kadhalika.

Serikali ijipange na kupanga mambo ambayo yataonyesha imedhamiria kuiona Stars inafanikiwa baada ya kupata ushindi huo wa mechi mbili. Hili linawezekana na huu ndio wakati wake sahihi wa kulifanya.


Kuwapa vijana morali kwa maneno matamu ni jambo zuri sana. Basi wapewe na morali kwa vitendo. Si vibaya kusema wakifuzu kuna hiki na kile. Si vibaya kusafirisha mashabiki kwenda Lesotho, si vibaya kusema mechi dhidi ya Uganda ni bure na ikiwezekana kuhakikisha kweli Lesotho wanafia kwao na tunarejea kuwazika Uganda hapa Taifa “Kwa Mchina”.


Shime, tusogee karibu na Stars kwa vitendo na huu ndio wakati wenyewe wa kuhakikisha mambo yanafanyika na kufanikiwa. Tukiamua kwa pamoja na msaada wa Serikali yetu tena kwa vitendo, hili halitashindikana.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic