December 9, 2018


Mambo ni moto ndani ya Yanga. Hivyo ndivyo unaweza kusema baada ya bilionea ambaye amekuwa akitoa msaada ndani ya kikosi hicho, Yanga Makaga, kusema kuwa ameshakamilisha usajili wa wachezaji wawili.

Kwa mujibu wa Championi, Makaga ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga na wakati timu hiyo ina mechi Kanda ya Ziwa, yeye ndiye alikuwa akiihudumia kwa kiasi kikubwa huku akiipandisha ndege kwenda kucheza mechi za kanda hiyo.

Lakini pia Makaga alishiriki kwa kiasi kikubwa Yanga kupata ushindi mkoani kutokana na huduma za ‘kishua’ alizokuwa akiwapa wachezaji na benchi zima la ufundi.

Sasa Makaga aliweka wazi nia yake ya kusaidia baadhi ya mambo ya usajili na kukiri kuwa tayari kuna wachezaji wawili ameshamalizana nao, kilichobaki ni kutambulishwa tu na uongozi wa timu hiyo.

Bilionea huyo mwenye vitega uchumi kibao, aliongeza kuwa yeye amekuwa akijitolea kusaidia kwa mapenzi yake kwa kuwa anaipenda Yanga kutoka ndani ya moyo wake.

“Kuna wachezaji wawili niliuambia uongozi wangu kuwa nitasaidia kuwasajili hivyo ifanye nao mazungumzo na watakapokuwa tayari waniambie.

“Kwa hiyo, hivi karibuni uongozi uliniambia kuwa tayari wameishafanya mazungumzo na wachezaji hao, hivyo kilichobakia ni kumalizana nao, kwa hiyo bila ya kupoteza muda niliweka mambo sawa na wachezaji nimeambiwa kuwa tayari wameshasaini.

“Hata hivyo, kwa sasa siwezi kuwataja majina yao kwani hilo siyo jukumu langu, ni jukumu la uongozi, ila wote ni viungo washambuliaji na wanatoka katika timu za hapa nchini, siyo wa nje ya nchi,” alisema Makaga na kuongeza:

“Lengo langu ni kutaka kuiona timu yetu inafanya vizuri kwani huwa naumia sana ninapoiona ikifanya vibaya, kwa hiyo kwa usajili wa wachezaji hawa pamoja na wengine ambao uongozi unaendelea kufanya nao mazungumzo, naamini kabisa hakuna timu yoyote ligi kuu itakayotuzuia kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema Makaga.

Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo tumezipata, zinasema kuwa wachezaji ambao Makaga ametoa fedha za kuwasajili miongoni mwao ni, Kenny Ally, Tibar John (Singida United), Vitalis Mayanga (Ndanda FC) na Charles Imlanfya (Mwadui FC).

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic