December 10, 2018





NA SALEH ALLY
KATIKA mpira kuna mambo mengi sana ili timu ikamilike. Mnaweza kuwa na fedha nyingi lakini msifanye vizuri na wale wenye shida kifedha lakini wana umoja, wakawashinda.

Ukizungumzia mwenendo wa ligi kuu katika kipindi hiki, Yanga ndio inayoongoza Ligi Kuu Bara, hapa nazungumzia kabla ya mechi yao ya jana usiku.

Kama watakuwa wameendelea kuongoza sawa, wakishuka watabaki kuwa wa pili. Lakini sote tunajua na tunaelezwa uongozi hauna fedha na wachezaji, makocha na viongozi hawajalipwa hadi mishahara ya miezi minne.

Siku chache zimepita, tumemuona Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera akimwaga chozi hadharani na mwisho lilikuwa ni suala la wachezaji wake wanavyoendelea kupambana na mwisho wanaambulia patupu.

Kwanza, lazima kuwapongeza wachezaji wa Yanga hasa kama utakubaliana nami na ukumbuke kwamba ni watu nao na wana matatizo kama sisi wengine.

Pamoja na hivyo, wameonyesha mapambano ya kiwango cha juu kukipigania kikosi chao kuhakikisha kinafanya vizuri. Lakini vizuri kukumbuka kwamba ni wanadamu na kuna wakati wanafikia wanachoka.

Mfano, Kelvin Yondani ambaye kati yetu hakuna anayeweza kupinga kwamba amekuwa akiipigania timu yake kwa kiwango cha juu anapokuwa uwanjani. Lakini mara kadhaa amepewa ahadi na mwisho hakukuwa kuna utekelezaji.

Tumeona pia kwa kipa, Beno Kakolanya. Wako ambao kwa sasa wanamlaumu, lakini angalia mzunguko wake na suala la fedha zake, kuanzia msimu uliopita lakini bado ameendelea kuwa tegemeo la Yanga. Ilipofikia amechoka, wengi walisahau kwamba alivumilia.

Pamoja na yote haya, binafsi nimekuwa na swali moja najiuliza na jibu linalokosekana.

Naweza kulitupa kwa viongozi wa Yanga wakawa wana jibu zuri ambalo kama watalitoa, basi litakuwa msaada mkubwa kwetu sote kama wadau wa mpira.

Kwamba, kampuni maarufu ya michezo ya ubashiri ya SportPesa, ilianza kuwa inatoa kitita cha Sh milioni hadi 900 kwa mwaka na mwaka uliofuatia, ambao ni huu, fedha itakuwa inafikia hadi Sh bilioni 1 kwa msimu.

Vipi Yanga inadaiwa mishahara hadi ya miezi minne? Yanga ambayo inadhaminiwa na kulipwa mamilioni ya fedha kutoka kampuni hiyo, yote hayo yanakwenda wapi.

Maana wachezaji wanalalamika suala la mishahara kwa miezi minne. Wachezaji wanalalamika fedha zao za usajili? Gharama ambayo uongozi itasema ni fedha ya uendeshaji. Je, ndiyo inachukua fedha zote bilioni moja?

Kama kuna kiasi cha viingilio, kiasi ambacho kinatoka kwa wadhamini wengine mfano wa Azam TV, hizi zote zinakwenda wapi?

Yanga haijawalipa hawa ilionao, inaendelea na usajili, walioingia wamelipwa? Viongozi wanajua na hawa nao ni binadamu watachoma?

Kuna kila sababu Yanga kuanza kupiga hesabu za baadaye kwa kuwa maisha ya kikosi chao yanashindwa kutofautisha timu isiyo na mdhamini na ile yenye mdhamini mkubwa anayetoa fedha nyingi.

Wakati mwingine naona haipendezi kwa madhamini anayemwaga mamilioni ya fedha halafu anasikia kila siku timu ina njaa na watu hawalipwi.

Je, fedha hizo ambazo tulielezwa kwamba suala la kulipa mishahara sasa halina shida tena, zimetumika tofauti? Kama ni ndio, basi Wanayanga na wadau wa soka waelezwe ili kuondoa sintofahamu na hali hii ya maswali.

Wanayanga wanaweza kuwa kimya kwa sasa, Yanga ikifanya vizuri. Siku ikiteleza huenda kutakuwa na maswali magumu kuliko wakati mwingine wowote ambao viongozi wamewahi kupata na hii itawachanganya.

Wanaweza kuepuka kuja kuchanganywa baadaye na mwisho kuchanganya mwenendo wa Yanga. Vizuri mambo kama hayo yakawa hadharani kwamba kama Yanga ina udhamini ule mnono, njaa inapita katika ufa upi hasa? 






2 COMMENTS:

  1. ndio maana kuna watu hawataki uchaguzi yanga maana wana maslahi binafsi bado hujazungunzia na ile michango yao

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic