Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema kuwa kamati ya masaa 72 itatoa taarifa rasmi kesho kuhusu hatma ya wachezaji wanaodaiwa kufungiwa kucheza michezo ya Ligi Kuu pamoja na faini.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya uwepo wa taarifa juu ya kufungiwa kwa mchezaji wa Simba Hassan Dilunga na Ibrahim Job wa Lipuli kwa kuchelewa kutoka uwanjani wakati wa kipindi cha mapumziko.
Ofisa habari wa TFF, Cliford Ndimbo amesema kamati ya masaa 72 ndiyo ina mamlaka ya kuzungumzia masuala yote ambayo yanahusu adhabu za wachezaji pamoja na faini na itatoa taarifa rasmi kesho.
"Masuala yote ambayo yanawahusu wachezaji hasa wanaopaswa kupewa adhabu kwa utovu wa nidhamu yapo chini ya kamati ya masaa 72, kesho kamati itatoa taarifa rasmi kuhusu masuala hayo," alisema.
Dilunga na Job walichelewa kutoka uwanjani kwenye mchezo wa Ligi kuu uliochezwa uwanja wa Taifa, Novemba 23 na timu zote kufanikiwa kutoshana nguvu ndani ya dakika 90 bila kufungana.
0 COMMENTS:
Post a Comment