December 19, 2018







Na Saleh Ally
ITAKAPOFIKIA Machi 13, mwakani, England watakuwa wamepata jibu kuwa watakuwa na timu ngapi zitakazosonga mbele kwenda kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

England kupitia Premier League ilikuwa gumzo kwa kuingiza timu nyingi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham kupata nafasi ya kutinga katika 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

England imefuatiwa na Hispania na Ujerumani ambazo kila upande una timu tatu, Italia na Ufaransa kuna timu mbili kutoka katika kila nchi.

Baada ya kufanikiwa kupata timu nyingi, kwa England ilionekana ni baraka au bahati ya kusonga mbele na kufika mbali katika michuano lakini kikubwa ilikuwa ni kuomba kupangwa kwenye nafuu ingawa mambo yanaonekana hayajawa hivyo.

Timu ambayo inaonekana imepangwa kubaya ni Manchester United ambayo itacheza na PSG ya Ufaransa lakini United wakiwa na kocha mpya baada ya Jose Mourinho ‘“kutumbuliwa” watakuwa nyumbani na kocha mpya.

Pamoja na kuona kama United wako katika wakati mgumu, uhalisia unaonyesha timu tatu za England ziko katika wakati mgumu zaidi huenda hata kuliko Man United kwa kuwa zote zitakwenda kucheza katika nchi moja, yaani Ujerumani.

Timu za Ujerumani zinajulikana, ni imara, zina uvumilivu na zile zenye malengo ya kupambana kutaka kushinda. Wajerumani wanafuata weledi katika vitu vyao vingi, hivyo mechi zitakazochezwa Ujerumani kamwe haziwezi kuwa laini na kuwarahisishia England.

England wanapaswa kuwa makini kwa kuwa kwa mpangilio huo dhidi ya Wajerumani unaweza kuwafanya katika hatua ya robo fainali wakamaliza wakiwa na timu moja tu au hawana kabisa timu.

Schalke 04 Vs Man City:
Ukiiangalia kwa namna ilivyo unaweza ukajua ni njia ya mkato kwa Man City lakini si hivyo. Pep Guardiola atakuwa anarejea Ujerumani na anajua namna alivyokuwa akisumbuka kuwafunga Schalke wakati akiinoa Bayern Munich katika Bundesliga.

Kweli hii ni timu nyingine, lakini ubora kwenye timu nyingine ni utamaduni. Msimu huu si mzuri kwa Schalke katika Bundesliga lakini uzoefu wake kimataifa na lazima wataweka nguvu nyingi katika Ligi ya Mabingwa ili kupata mkate sahihi.

Ukiangalia msimamo wa Bundesliga wako nafasi ya 14. Hizi ndizo timu za kuchungwa hasa zinapokutana na timu zenye mwendo mzuri kwa wakati husika.

Tottenham Vs Dortmund:
Usisahau Borussia Dortmund ndiyo vinara wa Bundesliga. Mwendo wao unatishia nguvu ya Bayern Munich. Sasa wako kileleni kwa tofauti ya pointi 9 dhidi ya Munich. Katika mechi 15 za ligi, wameshinda 12, sare tatu na wamekusanya pointi 39 zinazowafanya kuwa timu bora zaidi Ujerumani.

Angalia uwezo wa kufunga mabao, wamepiga 41 katika mechi 15 na wameruhusu mabao 15. Lazima Tottenham waende wamejipanga.

Liverpool Vs Bayern Munich:
Kocha Jurgen Klopp atakuwa anarejea nyumbani kwao Ujerumani, lakini atakuwa anarejea Allianz Arena, uwanja ambao kwake si sahemu ya kujidai.

Lazima unakumbuka ushindani mkali kati ya Bayern Munich dhidi ya Dortmund iliyokuwa inanolewa na Klopp. Ushindani wao ulikuwa ni zaidi ya gumzo na wakati huo alibatizwa kuwa kiboko ya Bayern. Sasa nafasi nyingine ya kuonyesha ubora huo.

Kwa Bayern pamoja na kutaka kusonga mbele kutaka kwenda kucheza hatua ya robo fainali, lakini suala la kumfunga Klopp litakuwa faraja kubwa kwao na hili linaifanya mechi hiyo kuchukuliwa kwa uzito mkubwa zaidi.

Ukiangalia katika msimamo wa Bundesliga, utaona Bayern hawana mwendo mzuri sana kama ilivyozoeleka kwa kuwa wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 30 sawa na Monchengladbach.

Inajulikana Bayern mara nyingi wanakuwa vinara, sasa wana pengo la pointi tisa dhidi ya Dortmund ambalo kiuhalisia haliondoi ubora wao na linaweza kuwa sehemu ya wao kuendelea kupambana zaidi ili kuwaonyesha mashabiki wao wana sehemu ya kushinda.

Timu za Ujerumani haziwezi kuwa laini kwa England. Si vibaya kusema kwamba England wamepata njia ngumu ya kwenda robo fainali na watalazimika kufanya kazi ya ziada kwa kuwa hakuna kisichoshindana.

Kikubwa wanachoweza kukitumia ni nafasi ya kuanza mechi zao nyumbani kama ilivyo kwa Tottenham, Liverpool na hata Manchester United itakayokuwa Ufaransa.

Kwa Manchester City, kazi ni ngumu pia kwa kuwa wataanzia ugenini ingawa kuna wakati kuanzia ugenini kunakuwa na faida zaidi kwa kuwa soka limebadilika. Kama ukifanikiwa kuanza kwa kushinda ugenini, basi unakuwa umeilainisha njia katika mechi ya pili.


ENGLAND VS UJERUMANI

Schalke 04 Vs Man City
Tottenham Vs Dortmund
Liverpool Vs Bayern Munich

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic