KOCHA YANGA AFANYA MAMBO 10 MAKUBWA, HAYA HAPA
Kuna mambo 10 ambayo Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amefanya mpaka mashabiki wanashangaa. Hebu angalia mambo ambayo Kocha huyo mwenye uraia wa DR Congo na Ufaransa amefanya;
KUTOPOTEZA MCHEZO
Yanga ya Zahera imecheza michezo 14 kwenye ligi kuu mpaka sasa ambapo wameshinda michezo 12 na kutoa sare michezo 2. Ni rekodi nzuri kwa aina ya kikosi Yanga ilichonacho.
Wamekusanya pointi 38 kwa sasa wana mabao 27 na ni vinara wa kupachika mabao wakiongozwa na Heritier Makambo mwenye mabao 7.
KUBADILI MATOKEO
Amekuwa na bahati sana kwenye eneo hili. Ni mtu wa mipango mingi hasa ya kutaka kufunga bao la mapema ili awaweke sawa wachezaji wake na kama ikitokea wameanza kufungwa bado amekuwa na mbinu muafaka za kuwarudisha mchezoni.
Alifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Ndanda ambapo walifungwa mapema baadae wakapata faulo wakasawazisha na kutoa sare, pia katika mchezo dhidi ya Mwadui baada ya kusawazishiwa bao kipindi cha pili alimtoa Klaus Kindoki na kumpa nafasi Ramadhani Kabwili, akafanikiwa kushinda kwa mabao 2-1.
Kwenye mechi na Prisons mambo yalikuwa magumu hasa kutokana na mchezo kuwa na tafrani nyingi mpaka dakika ya 70 walikuwa nyuma kwa bao 1 ndipo alipoamua kufanya mabadiliko kwa kumtoa beki Juma Abdul nafasi yake ikachukuliwa na Amissi Tambwe ambaye alibadili matokeo kwa kusababisha penati na kufunga mabao 2.
KUMUAMINI MCHEZAJI
Ni ngumu sana kuwaaminisha mashabiki wa Yanga kwamba Pappy Tshishimbi anarukaruka tu uwanjani wakati wao wanaamini kwamba ndio jembe. Lakini Zahera amewaambia ukweli. Tshishimbi siyo staa tena Yanga.
Zahera hatazami jina la mchezaji anaangalia juhudi na uwezo wa mchezaji. Juma Abdul alipoumia alimuanzisha Paul Godfrey ambaye ni kinda aliyewashangaza mashabiki kwenye mechi ya Simba na Yanga.
Mchezaji mwingine ni Mohammed Jaffary ambaye yupo kikosi cha vijana naye amekuwa akimpa nafasi ya kucheza bila kuangalia ni nani atakuwa benchi. Akimuamini mtu haangalii pembeni.
Ramadhani Kabwili amechukua nafasi ya Beno Kakolanya ambaye alikuwa golikipa namba moja kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kudai stahiki zake na Klaus Kindoki amekuwa benchi. Mashabiki wanamkejeli Kindoki lakini yeye anaamini bado ana kitu cha kuifanyia Yanga, hajaja bure.
KUSHINDA MIKOANI
Baada ya kuweza kufanikiwa kucheza michezo 11 jijini Dar es Salaam wengi walifikiria kwamba itakuwa ngumu kwake kupata matokeo nje ya Dar kutokana na ubovu wa viwanja.
Kashinda mechi zake zote tatu alizocheza nje ya Dar kwa ushindi wa mabao zaidi ya 2 ambapo mechi yake dhidi ya Prisons ilivuna jumla ya mabao 3-1.
MAAMUZI MAGUMU
Amekuwa ni mwepesi kufanya maamuzi ambayo wengi wamekuwa wakiyashangaa na amekuwa akiyasimamia mpaka apate matokeo.
Kwa mfano kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu ambaye amekuwa ni msaada ndani ya timu aliposhindwa kuhudhuria mazoezi muda ambao hakuwepo hakumjumuisha kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Mwadui na akapata matokeo bila ya kuwa na wachezaji wake kama Kelvin Yondani na Beno Kakolanya. Inahitaji ujasiri kufanya uamuzi kama huu haswa kwa kocha Mwafrika.
MSEMA UKWELI
Viongozi wamekuwa wakificha matatizo yaliyoko ndani ya Yanga lakini yeye wala haogopi anafunguka tu akiamini kwamba ndiyo njia sahihi ya kupata suluhisho na mashabiki wajue kinachoendelea.
Kwa sasa msisitizo wake ni kwamba hawezi kufanya usajili wa wachezaji wapya kwa muda huu kwa kuwa kuna wachezaji zaidi ya 10 ambao wamemfuata na kumueleza kuwa hawajalipwa stahiki zao hali ambayo inamfanya ashindwe kuruhusu kusajili wachezaji wengine.
Pointi yake ya msingi ni kwamba wachezaji hao wapya atakaozungumza nao atawaambia nini, hata akiwasajili atawapa nini ilihali wapo ambao wapo ndani ya timu wanadai stahiki zao? Jambo hili linamfanya azidi kuwa tofauti na makocha wengine kwa kuzungumza masuala yanayohusu uongozi ili kuweka usawa.
ANAWAPONDA WACHEZAJI
Ni mara chache sana kwa ardhi ya Bongo kocha kuwaponda wachezaji wake hata kama amepata matokeo, tofauti kwa Zahera amekuwa akiwaponda hata kama wamepata matokeo katika mchezo wao hali ambayo imezidi kumfanya awashangaze wengi wakiamini kuwa anatengeneza chuki kwa wachezaji.
Ibrahim Ajibu ni miongoni mwa wachezaji ambao walikumbwa na suala hili na alisema wazi kuwa licha ya wengi kuamini Ajibu anafanya vizuri bado amekuwa haonyeshi juhudi akiwa uwanjani hivyo anawakati mgumu kupata namba Taifa Stars.
Amissi Tambwe naye kocha alisema kuwa anapenda kula ugali hali inayomfanya aongezeke uzito na kushuka kiwango chake akiwa uwanjani, ajabu hata Herieter Makambo ambaye ana mabao 7 kocha alisema kuwa hana umakini na anafikiria kumleta Mama yake(Mama Zahera) ili awe mshambuliaji kutokana na uzembe wa mchezaji huyo.
KUWEKA KAMBI MOROGORO
Yanga hawakufanya maandalizi siriazi, walikuwa na kambi ya kuungaunga mjini Morogoro huku wakubwa wenzao Simba na Azam wakienda nje.
Simba ilikuwa Uturuki na Azam ikaweka kambi Uganda.
Hali ya uchumi wa Yanga ilikuwa ni duni, hivyo maandalizi ya kambi hiyo yaliwapa wasiwasi mkubwa mashabiki ambao hawaamini matokeo wanayoyaona kwa sasa Jangwani.
KUVAA KOFIA
Tabia hii amekuwa nayo kwa muda mrefu kwani kila akiwa benchi hawezi kukosa kuvaa kofia hali ambayo imewafanya baadhi ya wachezaji wake kuiga mtindo huo kwa kuvaa kofia mara kwa mara.
Zahera hapendi makuu hasa kwa upande wa mavaz. Anatupia kawaida sana saa nyingine hata kipensi na tisheti anapiga anatinga uwanjani.Ni mpenzi sana wa kofia anapokuwa kwenye benchi la ufundi.
MTU WA MAGAZETI NA TV
Anatoa ushirikiano sana kwa vyombo vya habari na hatafuni maneno. Amekuwa akijibu kwa ufasaha majibu mengi anayoulizwa na waandishi muda wote.
Anajitahidi kuongea lugha ya kiswahili chenye lafudhi ya kikongo ili aweze kwenda sawa na waandishi wa habari akiwa anawaelezea jambo ambao anahitaji waweze kulitambua.
Ni mwalimu ambaye amekuwa akieleza mambo mengi yanayohusu wachezaji na kuwakosoa wachezaji wake mbele ya vyombo vya habari bila ya kupepesa macho akiwa mbele ya kamera. Anapenda sana kutumia magazeti kuwasiliana na mashabiki wake.
Muandishi ungemalizia na kutaka kumpiga referee pia. Na kupaki basi katika mechi ya simba.
ReplyDeleteIla kupaki basi mbinu ya mchezo. By the way imekuwa faida kwa yanga.
Delete...Assume yanga ishinde mechi zake zote , itoke droo na simba, na simba ashinde mechi zote zingine. Nani atakuwa bingwa hapo?. Acha zahera awe kocha bora.
Kooo kupaki basi mlishindwa kulitoa acheni uzembe bwana
ReplyDeleteZahera anajua
Maswala ya kumpiga refa Antony hayakuhusu, waachie tff hiyo yote Ni mbinu ya kimchezo,
ReplyDeleteMh! Mbinu ya kimchezo! kumpiga refa!
ReplyDelete