December 19, 2018



Na Saleh Ally
KOCHA Mwinyi Zahera amejijengea sifa mbele ya mashabiki wa soka nchini kwamba ni mkweli na asiyependa kupindisha maneno hata chembe.

Tokea Zahera raia wa DR Congo ametua nchini, amezidi kubeba umaarufu akionekana ni mmoja wa makocha ambao kama kuna tatizo, basi angependa kusema ukweli na mwisho utatuzi upatikane.

Sote tumeona Zahera akieleza wazi kuhisiana na makosa ya wachezaji wake, akiwataka hadharani kubadilika na kuweka msimamo hadharani kuhusiana na masuala kadhaa.

Zahera amekuwa akionekana hana siri tena hasa baada ya kuanza kuzungumza kuhusiana na viongozi wake wanaohusika na masuala ya usajili kwamba walimdanganya kuhusiana na suala la wachezaji kadhaa ambao waliahidi kwamba wangewasajili na baadaye wakawa hawakufanya hivyo.

Zahera alieleza wazi kuhusiana na Kamati ya Usajili ya Yanga inayoongozwa na Hussein Nyika kwamba walimueleza walishamsajili mshambuliaji kutoka Uganda lakini pia kipa kutoka Kenya na wakamhakikishia kila kitu kimekwenda vizuri.

Kocha huyo alisema kilichomshangaza mwishoni ni kuelezwa kwamba kipa huyo hatasaini na Nyika akawa kimya kuhusiana na mshambuliaji huyo aliyemtaka na baadaye anasema aliona Yanga wakiwa wamemsajili kipa kutoka Zanzibar ambaye hamfahamu, hajawahi kumuona wala hakumpendekeza!

Kutokana na hali hiyo, mbele ya waandishi wa habari, Zahera akaweka mambo hadharani kwamba, kama litatokea suala la kukosa ubingwa. Basi yeye asilaumiwe kwa kuwa kila alichokitaka hakikufanyika na vilivyofanyika havikuwa kwa ridhaa yake na moja kwa moja amesukuma mzigo kwenye kamati ya usajili ya Nyika.

 Baada ya hapo, imefuatia ishu ya Zahera kuondoka kwenda Ufaransa. Ndani ya safari hiyo kumekuwa na mkanganyiko mkubwa, kila mmoja akisema kivyake. Nyika amesema tofauti na Msemaji wa Yanga, Dismas Ten na Zahera pia akaeleza tofauti kuhusiana na safari hiyo moja ya kwenda Ufaransa.

Nyika amesema kocha ana matatizo ya kifamilia kuhusiana na ndoa yake anatakiwa kwenda kusaini karatasi kadhaa. Lakini Dismas yeye amesema kocha huyo anakwenda kwa ajili ya matibabu wakati kocha mwenyewe amesema ni masuala ya biashara na atarejea nchini ni uhakika.

  

Sasa hii ni sehemu tosha ya kuonyesha kuwa kuna tatizo sehemu fulani hata kama kocha atarejea kuna tatizo ambalo linaanza kujenga nyufa kati ya kocha na viongozi hao.

Kama viongozi wamesema jambo wanaonekana wanatofautiana naye basi kuna suala la mawasiliano duni ambayo mara nyingi yanakuwa chanzo cha matatizo mengi hasa katika sehemu zinazihusisha watu wanaofanya mambo fulani sahihi.



Angalia Kocha Zahera anaonyesha kwamba amefanyiwa “mchezo” ambao haikuwa sahihi kulingana na hai ilivyo. Zahera amesisitiza kwamba hajafurahishwa kwa kuwa amedanganywa kwa kuhakikishiwa usajili utafanyika wa wachezaji fulani, haukufanyika lakini akadanganywa kwa kuletewa mchezaji ambaye hamjui au hakumpendekeza.

Kwa kocha makini kuona mchezaji ambaye hamjui, hajawahi kumsikia akisajiliwa katika kikosi chake ni kesi ambayo inaweza kusababisha mmomonyoko ndani ya kikosi kwa maana ya kocha na mchezaji husika wakati mwingine kutoelewana.

Tayari Zahera amejiwekea kinga, kwamba akikosa ubingwa asilaumiwe. Anaamini mwendo wake ulikuwa sahihi na alitaka wachezaji aliowataja, akahakikishiwa watasajiliwa na aliamini kupitia hao angeweza kuweka njia au malengo yake katika msitari. Sasa anaona kama amesalitiwa.

Kuanzia hapo unaweza kujiuliza. Je, baada ya Zahera kusema mambo hadharani akieleza kuhusiana na namna viongozi wa Yanga walivyomfanyia, unafikiri siku akikosea yeye wao watanyamaza?
  

Unafikiri viongozi hao wamefurahia? Kama hawakufurahi au kujisikia vizuri watachukulia vipi na watakuwa watu watakaokubali kwa nia ya kujifunza au watapanga kujibu siku yao ikifika ya kufanya hivyo!

Kwa mbali unaona kwamba kuna tatizo linakuja ndani ya Yanga lakini hata kama litatokea Zahera hawezi kuwa wa kulaumiwa kwa kuwa amechagua aina ya mtu ambaye anapenda kuwa wazi kwa lengo la kumaliza tatizo.

Tatizo hili ambalo kwa sasa linaonekana ni dogo leo, lazima kuwe na tahadhari kwa kuwa baadaye hili linaweza kuwa tatizo la kumyumbisha au kumuondoa Zahera Yanga.

Mliokosea kama kweli, basi mkubali na kuyafanyia kazi badala ya kutengeneza ukuta wa kujilinda na badala yake kutengeneza ufa. Ingawa kwa Zahera naye kama mzazi, inapendeza kuwa na staha na kuficha mambo ya ndani lakini kwa hili la usajili, ilikuwa vizuri kuwa wazi kwa kuwa wakati mwingine Wanayanga wanatembea wakiwa wamefungwa kitambaa cheusi ambacho wao hawakioni.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic