JEMBE JIPYA YANGA KUANZA KAZI NA WANAJESHI
KOCHA Mkuu wa Yanga Mkongoman, Mwinyi Zahera amemjumuisha kiungo wake mkabaji, Mohamed Issa ‘Banka’ kwenye orodha ya wachezaji waliongia kambini katika kujiandaa na michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Yanga imeingia kambini juzi Jumatano kwenye Hoteli ya Nefaland iliyopo Manzese jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza mazoezi ya mwishoni kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la FA uliotarajiwa kupigwa jana dhidi ya Biashara United.
Banka ambaye anasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa Yanga akiwa uwanjani, ni baada ya kifungo chake cha mwaka mmoja kuelekea ukingoni alichokuwa anakitumikia kutoka Fifa baada ya kubainika alikuwa akitumia kilevi chenye asilimia 150.
Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema kiungo huyo adhabu yake inatarajiwa kumalizika Februari 8, mwaka huu, hivyo ataanza kucheza katika mchezo wa ligi dhidi ya JKT Tanzania inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) utakaopigwa Februari 10, mwaka huu.
Saleh alisema kiungo huyo ni kati ya wachezaji waliongia kambini katika kujiandaa na mchezo wa Kombe la FA waliotarajia kucheza nao jana, licha ya yeye kutokuwa sehemu ya wachezaji watakaocheza mechi hiyo kutokana na adhabu yake kumalizika wiki ijayo.
Aliongeza kuwa, kiungo huyo tayari ameingizwa kwenye mipango ya Zahera katika michezo ijayo ya ligi ukiwemo wa Simba na Yanga utakaopigwa Februari 16, mwaka huu kutokana na mazoezi anayompa.
“Baada ya mechi ya Biashara tutasafiri naye kesho (leo) kuelekea Tanga kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Coastal Union na baadaye tutakwenda naye tena Singida kucheza na Singida United, Februari 6.
“Mchezo huo wa Singida ndiyo utakuwa wa mwisho kutumikia adhabu na baada ya hapo atakuwa huru na kuanza kucheza katika mechi inayofuatia ya ligi dhidi ya JKT Tanzania kabla ya kukutana na Simba,” alisema Saleh.
0 COMMENTS:
Post a Comment