MZUNGU AFANYIWA 'SAPRAIZI' MISRI
KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems amefunguka kuwa licha ya kuwa na baridi kali lakini bado wachezaji wake wameonyesha morali ya juu katika kufanya mazoezi kuhakikisha wako tayari kupambana dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Simba, kesho itakuwa ugenini dhidi ya Al Ahly katika mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Makundi ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab.
Simba itakuwa ikitupa karata yake ya tatu katika hatua ya makundi baada ya kuivaa, JS Saoura na AS Vita Club na kuwa nafasi ya tatu katika kundi hilo.
Akizungumza kutoka Misri, kocha huyo alisema kama timu wanaendelea vizuri kufanya maandalizi yao ya mwisho licha ya kukabiliwa na hali ya baridi ambayo ni tofauti na ile ya Tanzania.
“Japo kuna baridi kali lakini vijana wanaonyesha ari ya kupambana, wanafanya mazoezi kwa bidii na sisi tumefanya mazoezi usiku hivyo tunaendelea kujiweka sawa na wachezaji wote ambao wamekuja huku wote wako fiti.
“Kurejea kwa John Bocco kwenye kikosi nako kumeleta hamasa kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wachezaji, ninaamini mpaka kufika Jumamosi kila kitu kitakuwa sawa na lengo ni ushindi kama ni hali ya hewa tutaendelea kupambana nayo,” alisema Mbelgiji.
0 COMMENTS:
Post a Comment