LIGI Kuu Bara inazidi kupasua anga huku kila timu ikonyesha namna ambavyo imejipanga kubeba pointi tatu mbele ya mpinzani wake ndani ya Uwanja.
Kuna wachezaji ambao ni 'wachawi' kuzifumania nyavu usiku kabisa kwenye mchezo kwa kuwa wanapindua meza kibabe na kufanya matokeo kuwa tofauti na wengi wanavyofikiria.
Dakika moja kwa kila timu imekuwa na umuhimu kutokana na kubadili matokeo hasa kwa timu ambayo ilianza kupoteza ama hakukuwa na nafasi ya kushinda.
Hii hapa michezo ambayo washambuliaji walitumia muda wa jioni kabisa kutupia mabao kambani na kusaidia timu yao kubeba pointi tatu mazima ama kugawana pointi tatu na kila mmoja kuambulia moja kama ifuatavyo:-
Lipuli 2-2 Sindida United, Samora
Uwanja wa Samora, Singida United wakati wanapiga hesabu za kukomba pointi tatu mbele ya Lipuli ya Matola, mambo yalibadilika. Godfrey Mwashiuya alianza kufunga dakika ya 46 bao lilisawazishwa na Haruna Shamte dakika ya 61.
Dakika za lala salama, Boniface Maganga alizama kambani na kuwafanya waamini wanabeba pointi zote kufumba na kufumbua Miraj Athuman 'Shevchenko' alizama kambani dakika ya 90+2 na kufanya wagawane pointi moja.
Azam 2-1 Lyon, Azam
Mchezo huu ulichezwa Chamazi ambapo Lyon walianza kuzama kambani dakika ya 8 kupitia kwa Hood Mayanja, dakika ya 13 Yahya Zayd wa Azam FC alisawazisha bao huku Lyon wakiamini ngoma ni sare, dakika ya 89 Abdallah Kheri alizama kambani na kufanya Lyon waishie kuzisikia pointi tatu kwenye bomba.
KMC 0-1 Yanga, Taifa
Mlinda mlango mkongwe, Juma Kaseja hakuamini macho yake baada ya kijana, Feisal Abdallah 'Fei Toto' kumtungua dakika ya 89 ambapo mashabiki waliamini ngoma ni suluhu kutokana na dakika kuyoyoma bila timu kuwa na matumanini ya kushinda.
Dakika ya 88 beki wa KMC, Ally Ally 'Mwarabu' alicheza rafu kwa mchezaji wa Yanga hapo ndipo Fei Toto alionyesha maana halisi ya kusajiliwa Yanga kwa kupiga faulo kiufundi na kuzaa bao lililobeba pointi tatu kwa Yanga.
Mbao 2-2 Mbeya City, Kirumba
Mbeya City walifunga dakika ya 12 kupitia kwa Iddy Seleman na Eliud Ambokile dakika ya 49 iliwafanya waamini wanabeba pointi tatu mkoani Mwanza, Uwanja wa CCM Kirumba, wakati huo kocha Amri Said kabla hajajiunga na Alliance alikuwa anamuandaa mchezaji wake Evarigestus Mujwahuki ambaye aliingia akitokea benchi alipachika mabao mawili akianza dakika ya 83 na dakika ya 90 yote kwa kichwa na kuwafanya Mbeya City wabaki midomo wazi.
Alliance 1-0 Singida, Nyamagana
Mchezo wa kwanza kwa Alliance ikiwa nyumbani iliwapiga kimoja tu wapinzani wao Singida United kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Nyamagana, dakika za lala salama.
Dakika 89 zilikamilika kwa timu zote kutoshana nguvu, wakati huo ilikuwa chini ya Hemed Moroco ndipo dakika ya 90+3 Martin Kiggi alifunga bao la ushindi kwa Alliance.
KMC 1-1 Mbao, Uhuru
Mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Uhuru, Mbao walikuwa nyuma kwa muda baada ya Emmanuel Mvuyekure kuitanguliza KMC kuongoza dakika ya 45+2, wakijiandaa kubeba pointi tatu nyumbani ndipo David Mwasa alipotibua mipango kwa kufunga bao la kusawazisha dakika ya 90.
Stand 1-1 Alliance, Kambarage
Bao la mshambuliaji, Dickson Ambundo dakika ya 24 halikuwapa faida wao kubeba pointi tatu ugenini, mipango ilitibuliwa na Hafidh Mussa wa Stand United dakika ya 90 na kuwafanya wote wagawane pointi mojamoja.
Biashara 2-1 Mbeya, Karume
Mbeya City waliukumbuka ule msemo wa wahenga kwamba kutangulia siyo kufika, baada ya kufunga bao la kuongoza dakika ya 17 bao ambalo lilidumu kipindi cha kwanza mbele ya Biashara, kipindi cha pili meza ilipinduliwa.
Daniel Manyenye alifungulia mlango dakika ya 63 kabla ya msumari wa mwisho wa ushindi kuwekwa na Juma Mpakala dakika ya 90+6.
Biashara 1-0 Stand, Karume
Wazir Rashid wa Biashara United aliipa ushindi timu yake baada ya kufunga bao mida ya lala salama baaada ya dakika 89 kukamilika kwa timu zote kutoona lango la mpinzani.
Dakika ya 90 bao la ushindi kwa Biashara lilipachikwa kambani na Rashidi hali iliyowafanya wabebe pointi tatu ugenini.
Stand 1-0 Yanga, Kambarage
Mchezo wa kwanza kwa Yanga kupoteza msimu wa 2018/19 ulikuwa ni wa mzunguko wa pili ambapo walikuwa mkoani Shinyanga.
Hadi dakika ya 87 timu zote ilikuwa zimetosha nguvu zikiwa zimebaki dakika 2 kukamilika, Jacob Masawe alipachika bao la ushindi dakika ya 88 lililodumu mpaka mwisho wa mchezo.
Azam 1-1 Alliance, Azam
Huenda mkosi kwa Mholanzi, Hans Pluijm ulianzia kwenye uwanja wake wa nyumbani, Chamazi baada ya kulazimishwa sare mbele ya Alliance, kwani walitawala mchezo kwa kiasi kubwa na bao lao la kuongoza lilifungwa dakika ya 79.
Dakika ya 90+5, Alliance walipata faulo karibu na eneo la hatari hali iliyozaa matunda na Dickson Ambundo kupachika bao dakika ya 90.
0 COMMENTS:
Post a Comment