March 29, 2019


WIKIENDI iliyopita, bondia wa ngumi za kulipwa Tanzania, Hassan Mwakinyo, aliendelea kupaa kimataifa kufuatia kumtwanga kwa TKO, Sergio Eduardo Gonzalez kutoka nchini Argentina.

Mwakinyo alishinda pambao hilo la raundi nane ambalo halikuwa na ubingwa na lilifanyika nchini Kenya kwenye Jiji la Nairobi likisimamiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportPesa ambayo inamdhamini Mwakinyo.

Bondia huyo ana rekodi ya kucheza mapambano 16 akishinda 14 na 10 kati ya hayo ikiwa ni kwa KO, huku akipigwa mara mbili na kati hayo moja ni kwa KO.

Jumanne ya wiki hii bondia huyo alitembelea ofisi za gazeti hili zilizopo Sinza Mori jijini Dar na kufanya mahojiano mafupi juu ya pambano lake la Kenya.

Katika maojiano, Mwakinyo alianza kueleza juu ya maneno mengi ya watu wanaodai amempiga bondia mzee.

“Kiukweli kama mpinzani wangu angekuwa mzee au mgonjwa asingepanda ndege kuja kupigana na wala asingeweza kupewa kibali kwao cha kuja kupigana.

“Nilishinda Botswana mechi yangu ya kwanza watu hawakusema kitu kizuri, walisema nimebahatisha ikatokea tena kwa Sam, wakasema nimempiga mlevi mara hana afya.

“Wao wanasema lakini mimi nasogea, napiga hatua kwa kuwa SportPesa wameniwezesha mpaka leo hii nipo hapa.

Ulitamba kumaliza pambano hilo ndani ya raundi ya pili, lakini ikawa tofauti, kwa nini?

“Tofauti hakuna isipokuwa wale makocha niliokuwa nao walinieleza kitu kwamba natakiwa nichukue muda wa kucheza na mabondia wazoefu.

“Halafu nisitake kushinda raundi za kwanza kwa sababu mabondia wakubwa wanapopelekewa rekodi ya mtu huwa wanaangalia unachezaje na wakigundua unamaliza kazi katika raundi ya 1 au 2 basi wao watakukimbiza hadi ya saba.

“Lakini nilikuwa na uwezo wa kumaliza mapema ila nilifanye vile kwa sababu hiyo na kama angetaka kuendelea basi bado alikuwa anapigika tu.

Ni kweli ulipita kwenye mikono ya Rashid Matumla?

“Matumla hakuhusika kunitengeneza kabisa ila nilikuwa na mechi na mtu ambaye Matumla alimpiga KO, akatumika Matumla ili kunipa njia za kucheza naye.

“Lakini matokeo yake nikaona sioni anachokifanya kwangu kwa sababu mimi nilishazoea kufanya mazoezi raundi moja kwa dakika nane halafu yeye alikuwa anatumia dakika tatu kwa hiyo nikaona nashuka badala ya kupanda.

“Nikamueleza promota kwa  kuwa alilipwa kuja kunifundisha nilimueleza kwamba mafunzo yake hayanitoshelezi, hivyo asiseme kama amechangia kitu kwangu, Mungu ndiyo ana msaada kwangu na siyo yeye.

“Lakini yeye alitumia taaluma yake na akalipwa kutoa msaada kwangu ambao sikuona faida yake.

Kwa nini unatumia mbinu ya southpaw na orthodox kwa pamoja?

“Nashukuru kwamba umerudi kwenye swali langu kwamba utofauti wangu na wao umeanzia hapo.

“Popote pale nitakaposimama nitaweza kushinda na zamani nilikuwa nikifanya mazoezi, shida inakuwa kwenye msosi ila sasa hata nikitaka kula mara nane nakula.

“Nimefanya kitu kikubwa sana, serikali imenipongeza, nimepata kiwanja ambacho ni cha pili, siyo kitu kidogo, natamani kuja kufanya makubwa zaidi.

“Sasa hao wasiotaka waache wabaki na ujinga wao kutokana na siyo wote ambao watakaokuwa wakiniunga mkono na hata wewe siyo wote wanaokubali kazi yako.

Tanzania sasa hivi bondia gani unaweza kupigana naye?

“Kiukweli sijaona ingawa wengi wanasema wanataka kucheza na mimi ili waweze kuandikwa ila kwangu sioni kama kuna mtu wa kucheza naye hapa nchini.

Kuna wakati ulikuwa unamataka Amir Khan, vipi kwa sasa?

“Khan ni bondia mzuri, simtaji kwamba mimi ni bora zaidi yake lakini Khan ana matatizo kwa hiyo nataka kumpiga kupitia matatizo yake.

“Kwanza miguu yake mibovu halafu ana matatizo ya kidevu na kichwa chake kama cha bata yaani kikiguswa tu kazi imeisha sasa nikicheza naye nitakuwa sipigani ila nitamvizia ajae nimalize kazi yangu.

“Kitu ambacho Watanzania wengi hawawezi, wanaongea sana wana mataji mangapi hadi sasa yaani sawasawa umesafirisha mabondia 20 kwa mwaka ambao wote wanakuwa wanashindana kwa kupigwa.

Jambo gani ambalo huwezi kusahau?

“Kila kitu katika maisha tunasahau lakini kuna wakati mama yangu alipata matatizo ikanibidi kuongeza hasira zaidi katika mazoezi ili nifanye vizuri kwenye mechi kwa ajili ya kumsaidia yeye.

“Tena ilikuwa wakati nakwenda Uingereza kucheza na Sam ilikuwa lazima nishinde kwa hali yoyote, aligongwa na bodaboda na aliyemgonga hakuwa na kitu, hivyo mambo yakawa magumu ingawa mwenyewe aliniombea ndiyo maana ikatokea vile.

Tofauti ya mazoezi ya Wazungu na kwetu ni kitu gani?

“Kikubwa ni ufundishaji ndiyo kilichonifanya nivutiwe na watu wa kule lakini naona kama nikichukua mbinu zao na zangu nakuhakikishia hakuna bondia atakayeweza kumaliza na mimi raundi nane.

“Unajua ushindi unaanza na mimi kutoka moyoni nimesema bondia atakayekuja kunipiga labda awe ametoka mbinguni au Mungu mwenyewe awe amepanga riziki yangu imekwisha kwenye ngumi ila siyo jambo rahisi kupigika.

“Ngoja nikwambie kuna Mtanzania ametengeza rekodi yake vizuri sana akawa ameenda Ulaya kucheza lakini alitaka dola elfu 50 lakini akambiwa Tanzania bondia tunayemjua ni Mwakinyo.

“Lakini alieleza ana rekodi nzuri ila hajapiga watu wakubwa, hivyo siyo rahisi kupewa pesa anayotaka, mimi nimesimamisha dunia, nimekaa kwenye kurasa za mbele katika gazeti kubwa Uingereza kwa wiki nzima.

“Niseme siyo rahisi kucheza na mimi, kikubwa tuelewane nataka kiasi gani watoe, nitakuwa tayari kucheza hata sebuleni kwake na bado nitampiga vizuri tu ila kwa sasa hakuna wa kiwango changu.



Ratiba yako ya msosi unapokuwa na pambano inakuaje?

“Kwanza sina chakula maalum ila ninapokuwa na mechi huwa nakula zaidi kwa kuwa nafanya mazoezi zaidi lakini kama sina mechi nakula kawaida tu.

“Unajua nikiwa na mechi asubuhi nikitoka mazoezini huwa kuna uji nakunywa majagi mawili, huo uji huwa unaongeza nguvu.



“Uji huo unakuwa na karanga, mtama, mahindi, ngano na ulezi ambao nakunywa halafu nakwenda kuoga, mazoezi yakiisha inakuja chai na chapati zisizopungua sita zikiwa na maharage.

“Jioni nikirejea nikikuta chochote nakula hata kama ikiwa ni viganja vya mtu, hivyo sina chakula maalum ila nakula kutokana hali na ukubwa wa kazi ninayoifanya.



Katika ratiba yako ya kula tofauti yake ipo wapi wakati upo mwenyewe na sasa wapo SportPesa?

“Nikisema leo nafanya mazoezi halafu nikatamani supu basi nakunywa supu kweli, siyo nafanya mazoezi kisha nakwenda kula vipande vya miwa, yaani kifupi kwa sasa nina uhakika wa kula na nina uhakika wa kushinda mechi yoyote labda Mungu aniambie riziki yangu imekwisha kwenye huu mchezo,” anasema Mwakinyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic