March 24, 2019

KIKOSI cha Taifa Stars leo saa 12:00 Jioni kitakuwa kazini kumenyana na timu ya Uganda kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Afcon 2019 zitakazofanyika nchini Misri mwezi Juni huku mchezo wao wa leo ukiwa ni wa lazima kushinda wa Stars kwani hawana mchezo mwingine tena.

Uganda wao hawana cha kupoteza leo kutokana na kufuzu hatua hii baada ya kufikisha pointi 13 kwenye kundi L ambalo mpaka sasa timu tatu zina nafasi ya kufuzu kwa leo kutokana na kila mmoja kuwa na pointi ambazo zinampa nafasi mpinzani wake kupenya endapo mmoja kati yao atapoteza.

Wakati Stars ikimenyana na Uganda leo saa 12:00 Jioni wapinzani wao ambao nao wanagombea nafasi ya kufuzu hatua ya kufuzu Cape Verde na Lesotho nao pia watakuwa Uwanjani kutafuta tiketi ya kuwania kufuzu Afcon.

Kundi L kwa sasa lipo wazi kwa kila mmoja aliye nafasi ya pili, tatu na ya nne kutokana na kila mmoja kuwa na pointi ambazo zinategemea mchezo wao mmoja mkononi huku kila atakayeshinda itamlazimu kutazama matokeo ya mchezo wa jrani yake amepata nini na hesabu zinakaaje.

Lesotho yupo nafasi ya pili akiwa ana pointi 5 anacheza na Cape Verde ambaye ana pointi nne hivyo kama Lesotho atashinda atafikisha pointi nane na kumdidimiza Cape Verde mwenye pointi nne nafasi ya mwisho.

Endapo Cape Verde atashinda atafikisha pointi saba na kumdidimiza mazima Lesotho mwenye pointi tano huku naye atatakiwa atazame matokeo ya Stars ajue hatma yake.

Endapo watatoka sare hapo nafuu kidogo kwa Stars kwani Lesotho atafikisha pointi sita na Cape Verde pointi tano hivyo Stars akishinda safari inakuwa imeiva.

Stars akishinda mchezo wake dhidi ya Uganda atageuka kutazama nani ameshinda kama Lesotho akishinda safari yake inayeyukia Taifa kutokana na kuwa sawa na pointi na Lesotho huku akiwa amezidiwa mabao ya mechi walipokutana na Lesotho.

Lesotho ameshinda mabao 2 huku Stars akiwa ana bao moja tu mkononi walipokutana kwenye mechi za awali kuwania kufuzu Afcon.

Picha itatisha kama Lesotho akapigwa na Cape Verde, halafu kwa Mkapa ngoma ikawa sare ama Emmanuel Okwi akafanya yake ngoma itapinduka na kuwapa nafasi Cape Verde kufuzu Afcon kiulani.

Hivyo leo wachezaji wa Stars wanatakiwa waingie Uwanjani wakitambua kwamba wanacheza fainali na kila mtanzania anaamini watapenya mbele ya Uganda ambao mpaka sasa hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa hata mchezo mmoja kwenye kundi L.

 Mchambuzi wa masuala ya michezo, Mwalimu Kashasha amesema kuwa mashabiki wamekuwa na mwamko mkubwa kutokana na Serikali na Shirikisho a Soka Tanzania (TFF) kutoa sapoti ya kutosha hali inayowapa wachezaji deni. 

"Wachezaji wana deni kubwa leo kupata matokeo hasa kutokana na nguvu ambayo imewekezwa hasa tangu mwanzo na watanzania wameitikia kwa hamasa kubwa.

Kwa sasa ushindi upo miguuni mwa wachezaji ambao watakuwa na kazi huku mashabiki wakitoa sapoti yao,kila kitu kinawezekana," amesema Kashasha.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic