April 15, 2019



Na Saleh Ally, Liverpool
EVERTON ni klabu kongwe katika soka la England, ni moja ya klabu 12 zilizoshiriki kuanzishwa kwa Ligi Kuu England mwaka1888. Pamoja na Everton FC, nyingine ni Accrington, Aston Villa, Blackburn Rovers, Bolton Wanderers, Burnley, Derby County, Notts County na Preston North End, wakati huo ikijulikana kwa jina la Football League First Division. 

Klabu hiyo ndiyo chanzo cha kuanzishwa kwa FC Liverpool ambayo ilikuwa sehemu yake hadi pale walipoamua kujitenga na kuanzisha klabu yao na huo ndiyo ukawa mwanzo wa Merseyside Derby moja ya Derby maarufu ya mchezo wa soka duniani.

Pamoja na wao kuwa wakubwa, Everton ndiyo waliamua kuondoka Anfield na kuanzisha Everton FC na jina la uwanja wao ukawa Goodison Park.

Wakati wa ligi hiyo kabla haijaanza kujulikana kama Premier League mwanzoni mwaka miaka ya 1990, Everton FC walibeba ubingwa mara mbili. Hata hivyo imekuwa miaka mingi na nguvu ya kuwa mabingwa, kidogo haijakaa sawa.

Pamoja na hivyo, wanataka kushiriki michuano ya kimataifa ili kuendelea kujiimarisha na kuongeza nguvu ya moja ya klabu zenye nguvu England kwa kuwa wao wanabaki kuwa na historia lakini mafanikio makubwa ya makombe na michuano ya kimataifa, haijakaa sawa.
Kocha Mkuu Marco Silva raia wa Ureno anaamini wakati wa mabadiliko katika kikosi cha Everton ambacho kwa sasa kinadhaminiwa na kampuni maarufu ya michezo ya kubeti ya SportPesa.

Silva anasema wanachotaka kupambana na kuingia katika timu saba za juu na mwisho kushiriki michuano ya Europa League kwa ushindani mkubwa na wa juu kabisa. Lakini mwisho anasisitiza, kama wataikosa nafasi hiyo, bado hatakuwa na shida yoyote!

Katika mahojiano maalum ambayo Gazeti hili la Championi la Tanzania lilifanya na kocha huyo pamoja na runinga za Sky Sports na BT Sports kwenye Viwanja vya Mazoezi vya Everton FC katika eneo la Finch Park nje kidogo ya Jiji la Liverpool, Silva amesema ushiriki wa michuano ya kimataifa utasaidia kurudisha hadhi ya klabu hiyo kongwe na yenye heshima katika soka la England.

“Kwa maana ya historia, Everton ina historia kubwa na soka la England. Ni klabu inayopaswa kupewa heshima, lakini bado nafasi ya kufanya vizuri zaidi inatakiwa kupiganiwa na ndiyo jambo ambalo tumekuwa tukilifanya kwa nguvu sana.

“Tunataka kufanya vizuri zaidi na zaidi kwa kuwa tunaona mwelekeo mzuri wa kuimarika kwa kikosi chetu, unaona mwishoni mwa ligi tumeanza kucheza kwa kujiamini zaidi na mwendo wetu umekuwa mzuri.

“Tunataka kushinda mechi zote zilizobaki lakini katika Premier League hili haliweza kuwa jambo rahisi, angalia kama unakutana na Fulham ambayo imeishateremka daraja, haina presha hata kidogo na timu kama hii inakuwa hatari zaidi kwetu (kweli Fulham imewafunga 2-0).

“Baada ya hapo itakuwa ni Manchester United na sisi tutatakiwa kuanza na Fulham, kama itashindikana Manchester United itafuatia na iwe kama fainali kwetu. Tunatakiwa kupata pointi tatu kwa kuwa tunakwenda ukiongoni, chini ya mechi tano tutakuwa tumemaliza ligi na sisi tunataka nafasi saba za juu,” anasema Silva akiwema msisitizo.

“Kushiriki michuano ya kimataifa ni jambo zuri na tunapaswa kulipa kipaumbele ndiyo maana tunataka kupambana vilivyo. Lakini ikitokea mambo yakawa magumu pia, hatutaona tumekwama badala yake tutajipanga kwa ajili ya msimu ujao huku tukirekebisha mambo ambayo tunaamini yatakuwa mazuri.

“Kama unakwama jambo na mwisho unaona bila ya hilo kila kitu kimefeli, hii inaweza kuwa hatari ya kukufelisha mambo mengine. Ndiyo maana nasema tutapambana hadi mwisho, ikishindikana basi tunaangalia kinachofuatia kwa ufasaha,” anasema.

Everton iko katika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 46 na imecheza mechi 34, maana yake imebakiza mechi nne tu za Ligi Kuu England, moja ikiwa dhidi ya Manchester United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Goodison Park jijini hapa wikiedi ijayo.

Msimu huu ulikuwa mzuri kwa Everton ingawa bado inatakiwa imalize vizuri. Kikosi hicho za Silva kilionekana kuwa hatari au kiboko cha vigogo baada ya kuzitwanga Chelsea na Arsenal, sare na Tottenham, Liverpool, Arsenal kwake Emirates na Man City kwake Itihadi.

Katika mechi zake 34, imeshinda 13 ikionekana kuwa moja ya timu zinazopata mabadiliko makubwa pamoja na ushindani mkubwa sana wa Ligi Kuu England.

Mjue Marco Silva
Jina lake kamili ni Marco Alexandre Saraiva da Silva, umri wake ni miaka 41, ni Mreno ambaye enzi anacheza soka alikuwa beki wa kulia.

Silva alistaafu akiwa na umri wa miaka 34 baada ya kucheza mechi 152 na kufunga mabao nane katika timu tatu za juu.

Alitua Everton, mwaka jana baada ya kuonyesha kuwa ana uwezo mzuri wa kupambana na timu za England alipokuwa akiifundisha Watford.

Wakati anacheza alizitumikia timu kadhaa za Ureno lakini zaidi ni Estoril alikodumu kwa miaka sita. Baada ya hapo alistaafu na kuanza kuitumikia timu hiyo kwa miaka mitatu.

Baada ya hapo maisha yake ya ukocha yaliendelea katika timu ya Sporting CP kisha akatoka nje ya Ureno akifanya kazi katika timu za Olympiacos ya Ugiriki, baadaye akaenda England alikotua Hull City, Watford na sasa ni Everton

Baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa Everton, Mei, mwaka jana akichukua nafasi ya Sam Allardyce, hiyo ilikuwa ni timu yake ya tatu katika Premier League, hizi ni takwimu zake kwa jumla tangu aanze kuwa bosi katika ligi hiyo: 

Takwimu za Silva (Premier League)
Mechi 76
Kushinda 26
Sare 15
Kupoteza 35
Mabao ya kufunga 99
Mabao ya kufungwa 124


Marco Silva
Alikozaliwa: Lisbon, Ureno
Urefu: Futi 5 inchi 11

Alikocheza 
1996–1997: Belenenses
1997–1998: Atlético
1998–2001: Trofense
1999–2000:  Campomaiorense (mkopo)
2001: Rio Ave
2002–2003: Braga B
2003–2004: Salgueiros
2004–2005: Odivelas
2005–2011: Estoril

Alikofundisha
2011: Estoril (Mkurugenzi wa Soka)
2011-2014: Estoril
2014-2015: Sporting CP
2015-2016: Olympiacos
2017: Hull City
2017-2018: Watford
2018-sasa: Everton

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic