April 15, 2019





NA SALEH ALLY
TULIZA akili kama kweli unaupenda mpira wa Tanzania, nataka tujadili jambo kwa faida ya mpira wa nchi yetu badala ya utani tu wa Simba na Yanga ambao faida yake ni kuchekeshana na mwisho inakuwa basi.

Utani wa jadi maana yake nini, msingi wa neno lenyewe ni utani. Je, utani tu kila kukicha unaweza ukawa ndio faida ya maendeleo ya mpira wetu.

Hata kama hatuukatai utani basi ifikie wakati tuwe tunabadilika kimawazo na kuwa watu tofauti kidogo badala ya utani tu, basi tunaangalia mambo ya msingi.

Kila mmoja wetu anaamini tofauti ingawa binafsi nimekuwa nikitofautiana na watu wengi sana kwa kuwa naona ushabiki wa timu zetu hasa Yanga na Simba kwa watu wengi wanaojiita mashabiki umekuwa ni wa kuingiza, kupenda kuonekana, kutafutia sifa na kadhalika, lakini si mapenzi ya dhati kutoka katika mioyo yao.

Wanaoshabikia wengi wanaamini kumuudhi wa upande mwingine, kumkera au kumuona anaumia ndio ushabiki pekee. Ushabiki wa kutukanana na kuumizana, kutakiana mabaya, ndio ushabiki jambo ambalo kwa miaka mingi nimekuwa nikiamini limeziangusha klabu hizi ndio maana eti hata kujenga uwanja wa mazoezi peke yake, inaonekana ni jambo kubwa lililoshindikana leo kwa zaidi ya miaka 80.

Hebu jiulize, uwanja kwa maana ya udongo, halafu inatakiwa kuwekwa nyasi na kuzikuza chini ya uangalizi maalum na baada ya hapo inabaki kumwagilizia na kutengenezea magoli! Klabu kama hizo zinashindwa?

Kuna mambo mengi Simba na Yanga zingeweza kushirikiana, lakini imeshindikana kwa visingizo au vigezo visivyokuwa sahihi kwa madai ya rangi, upenzi na sifa za hovyo kabisa.

Leo angalia Simba ilipofikia, hatua ya robo fainali, ni robo fainali kweli achana na zile hadithi za miaka ile za Yanga au haohao Simba. Tunajua sasa soka lilivyopiga hatua, lakini ajabu muda mwingi wapinzani wao Yanga wako wanapiga kelele na kucheza Kikongo, kushangilia kila timu ya kila taifa linalocheza na Simba.

Simba iliyoifunga Mbabane Swallows, ikasonga mbele, ikaitwanga Nkana FC ya Zambia na kusonga tena. Imekutana na Al Ahly imeshinda Uwanja wa Taifa kama ilivyofanya kwa AS Vita Club, timu hizi ziliifunga Simba mabao 5-0 kwao, kila moja. Kabla Simba iliitwanga JS Saoura ya Algeria kwa mabao 3-0, Taifa.

Nakukumbusha TP Mazembe imechukua ubingwa mara tano na Ahly, ndio inaongoza kwa Afrika. Lakini angalia Dar es Salaam, TP Mazembe walilazimika kupoteza muda wakipata sare ya bila kufungana.

Maana yake kuna mabadiliko katika mpira wa Tanzania, jambo lililopaswa kuwa mjadala sasa. Simba imetolewa kwa kufungwa jumla ya mabao 4-1 katika hatua ya robo fainali.

Kumbuka katika mechi nane zote ambazo zimezaa jumla ya mechi nne za robo fainali, idadi ya mabao 4-1 ndio ndogo zaidi kwa kuwa Constantine ya Algeria, imetolewa kwa mabao 6-3 dhidi ya Esperance, Horoya ya Guinea imechapwa jumla ya 5-0 dhidi ya Waydad na vigogo Al Ahly wametoka kwa jumla ya 5-1 dhidi ya Mamelodi ya Afrika Kusini.

Simba wanapaswa kuzomewa? Shabiki wa timu anayeizomea Simba yake imecheza hatua gani? Au michuano ipi? Faida ya ushabiki hata kama yako inafanya hovyo unashangilia za wengine tu na unaita ni ushabiki?

Kama hiyo kweli ndio furaha ya mpira Kitanzania, nafikiri vema kuibadilisha na sasa mjadala uwe namna walipofikia Simba, timu nyingine za Tanzania zifanye nini, maana ndio tunainuka na tunahitaji kuwa na timu zitakazofikia hapo.

Kama ni Simba itashiriki mwakani ivuke, ikienda Yanga basi ifanye vizuri kwa kiwango hiki au zaidi. Kama ni Azam FC au nyingine, kuwe na mwendelezo huu wa Simba, Tanzania itakuwa bora na mwisho tutainuka na kuondoka kwenye kuwa wasindikizaji wakchuano ya Caf.

Bado nafasi ya kuchagua pia tunayo, kama tunaona kuchekacheka na kuchekana ndio furaha ya mpira, basi tutaishia hivi tu, kuchekana na kuchekelea.

4 COMMENTS:

  1. Uandishi wako tu unaonesha we ni mnazi wa Simba... Labda nikupe changamoto kwani kipindi Yanga inacheza shirikisho hata kama haikufika popote kama unavyodai, Mashabiki wa mikia kama wewe si ndo mlikuwa kimbelembele kushabikia timu za nje?

    ReplyDelete
  2. Mi nashangaa huo uzalendo wanaounadi kila siku ufanywe na Yanga wakati miaka 5 iliyopita simba akiwa kakaa kando Yanga ikicheza kimataifa wao waliisapot kila timu ngeni ilipofika nchini. Unakumbuka 2016 Yanga ilipocheza Taifa na TP Mazembe na Manji alitoa free chance kila shabiki aingie uwanjan bure na Kiingilio ni jez ya Yanga/njano au kijani? Simba walivaa mashati ya wapinzan ndani na nje walivaa jez za yanga na kuingia uwanjani. Waliporuhusiwa kuingia wakazichana chana na kuzitupa jez za yanga na kubak na za wagen au zao kisha kuwasapot mazembe.

    Leo mnaandika kuilaum yanga. Uandish wenu hamna weledi kabisa kwa sababu mlipaswa kuliandika lile na kulikemea kwanza na mngehamasisha simba waache ujinga wao ili leo cmba wapo kimataifa wapate nguvu kutoka Yanga kwa reference kwamba yanga alipokuwa kimataifa cmba ilimpa sapot.

    Saleh Jembe kaka na waandish wenzako andikeni mambo ya soka bila kuegemea kwenye ushabiki ambao sasa mnaudhihirisha mpaka kipofu anauona!

    ReplyDelete
  3. sawa endeleeni kuchekacheka na kutembeza bakuli club yenu itakuwa bora

    ReplyDelete
  4. Kama ni makabila basi hakuna makabila mabaya kama Simba na Yanga. Mwenye mada kama nimemuelewa vizuri, anasema tutathmini hatua waliyofikia Simba. Hata Young Africans wakituwakilisha mwakani na wafanye hivyo kwa kujua mpira wa Tanzania sio wa kubeza sana sasa hivi. Ndo maana tunakwenda Afcon na Inshallah vijana wetu wa U-17 wanaweza kutupaisha Brazil. Ushabiki usifunike mafanikio au madhaifu. Wingi wa mashabiki wa Simba au Young Africans ungekuwa na tija klabu hizi zisingekosa viwanja hata vya mazoezi tu. Ifike mahala tutofautishe kati ya ushabiki na udau wa mchezo wa mpira.
    Tulipo sio pabaya. Sasa tusirudi nyuma. Bila ya Young Africans, Simba , Azam, Alliance na wengineo kuwa imara tusitarajie mafanikio ya kudumu labda ya kuviziavizia tu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic