ZIMESALIA siku tatu kabla ya kuanza kwa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17, Afcon itakayofanyika hapa Tanzania kwa mara ya kwanza.
Pazia la michuano hiyo, litafunguliwa Jumapili hii ambapo mashindano hayo yataunguruma kuanzia Aprili 14-28 kwenye ardhi hii ya Tanzania.
Ikumbukwe kuwa, michezo hiyo ya Afcon imepangwa kuchezwa kwenye viwanja viwili tu ambavyo ni Benjamin Mkapa (Taifa) na mwingine ni Azam Complex, ule wa Uhuru ukitumika kama uwanja wa mazoezi kwa timu shiriki.
Wakati Tanzania ikiwa ndiyo wenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza, macho ya Watanzania yanawatizama vijana wa Serengeti Boys juu ya kuandika historia kwa kutwaa ubingwa.
Iko hivi, endapo Serengeti Boys itafanya vyema kwenye michuano hiyo, basi itakuwa na nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Vijana ambalo litafanyika mwaka huu nchini Brazil.
Mbali na kila nchi kujiandaa ipasavyo, Serengeti Boys wana kila sababu ya kujituma ili wavune matokeo chanya katika kila mechi yatakayowafungulia njia ya kutinga fainali na hatimaye kuchukuwa ubingwa.
Katika kundi la Serengeti Boys, zipo nchi ambazo Tanzania ziliwahi kukutana kwenye michuano tofauti ambazo ni Uganda na Angola. Serengeti Boys imekutana na timu hizo kwenye ile michuano ya Cosafa na Cecafa ambako timu hiyo ilifanikiwa kutwaa ubingwa mwaka jana
Kwa kufahamiana huko, ni wazi kuwa jukumu kubwa wanabeba Serengeti Boys katika kuhakikisha wanaitoa kimasomaso Tanzania dhidi ya wapinzani.
Kimaandalizi, Serengeti wamekwiva, kilichobaki ni kuitumia ipasavyo miguu yao uwanjani kwa kupeana pasi zilizokwenda chuo kikuu na kutua moja kwa moja kwenye lango la timu pinzani.
Nini tunamaanisha hapa! Hakuna kingine zaidi ya wachezaji wa Serengeti kucheza kwa nidhamu, kujituma, kushirikiana ili wafikie lengo la kufuzu kushiriki mashindano ya Dunia.
Maandalizi yanaendelea lakini Watanzania tunatakiwa kufahamu Serengeti Boys ni yetu wote hivyo tujitokeze kwa wingi kuiunga mkono timu yetu iweze kufanya vyema katika michuano hiyo.
Sapoti kubwa inatakiwa kutoka kwetu Watanzania katika michuano hiyo, wale vijana wakiwezeshwa na Watanzania ni wazi kuwa, hamasa itaongezeka na mwishowe watacheza huku wakijua kwamba, wana deni kubwa katika nchi hii.
Serengeti ambayo inafundishwa na kocha, Oscar Mirambo, imekuwa na rekodi ya kufanya vyema katika michezo yake tofauti hivi karibuni. Hivyo tumuunge mkono Mirambo pamoja na vijana wake kuhakikisha wanaitendea haki Afcon ili watinge kwenye michuano ya Kombe la Dunia na kuweka historia.
Kila la kheri Serengeti Boys katika maandalizi yenu ya mwisho, imani ya Watanzania ni nyinyi kuiperushe vema bendera ya nchi yenye rangi nne lakini msisahau kuwa hii ni zamu yetu kwenda Brazil kuiwakilisha Afrika.
0 COMMENTS:
Post a Comment