May 27, 2019


AFRIKA Mashariki Alhamisi ya wiki iliyopita usiku ilikuwa kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. Mabingwa wa Tanzania, Simba walicheza na Sevilla ya Hispania mida hiyo katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyokuwa na umuhimu mkubwa kwa soka la Tanzania.

Mechi hiyo iliandaliwa na kampuni ya michezo ya kubeti ya SportPesa kwa ushirikiano na Laliga na TFF. Ni mchezo mzuri ambao mashabiki wengi wa Tanzania na Afrika wameinjoyi soka.

Licha ya matokeo ya mwisho lakini Simba ilicheza soka na kuonyesha kweli wao ni mabingwa wa nchi na ni timu iliyoundwa kushindana.

Spoti Xtra tunatoa pongezi kubwa kwa soka la ushindani lililoonyeshwa na Simba na kuwaduwaza Sevilla ambao hawakutarajia kama mchezo ule ungekuwa na mabao mengi kiasi kile.
Hawakutarajia kama Simba ingeweza kuwafunga mabao manne, lakini ndiyo maajabu ya soka yalivyo. Lolote linaweza kutokea Uwanjani na ndilo lililotokea.

Maoni yetu ni kwamba mchezo ule na kila kitu walichokiona Simba kiwe kama funzo kwao na kuona jinsi wanaweza kufanya ili kuimarika zaidi kisoka ndani na nje ya Uwanja.

Katika mchezo ule lazima uongozi utakuwa na mambo mawili matatu ya kujifunza kuhusiana na mambo ya utendaji, maandalizi ya mambo ndani na nje ya uwanja pamoja na uendeshwaji mzima wa mambo ya soka kwenye ngazi ya klabu.

Ni rai yetu kwamba kwa levo yetu Tanzania na aina ya mabadiliko ambayo Simba wamekuwa wakiyapigia upatu, watakuwa wamejifunza kitu cha kuboresha.

Sevilla imewazidi Simba kwa mambo mengi kwavile ni klabu kubwa na ya miaka mingi Hispania, hivyo wachezaji wetu wajifunze kitu kutokana na kile walichokiona uwanjani. Miongoni mwa mambo ambayo tunamaanisha hapa ni pamoja na ari ya mapambano uwanjani bila kukata tama, kucheza kitimu pamoja na utulivu wa mchezaji mmoja mmoja.

Kwavile Simba ilianza kupata mabao ya haraka katika mchezo huo lakini wenzao wakatulia na hawakuwa na papara huku wakicheza na muda na malengo yao mpaka dakika ya mwisho wakapindua matokeo na kuondoka na ushindi.

Kuna jambo kubwa la kujifunza hapo kwamba kama mchezaji usikate tamaa pambania timu yako mpaka dakika ya mwisho kwavile kwenye soka sekunde moja ni muda mwingi sana kwani kibao kinaweza kubadilika kama walivyofanya Sevilla.

Lakini kilichotokea ni muafaka kwavile kimefanyika kwenye mechi kubwa ya kirafiki ambao lengo lake ni kujifunza na kujipima. Ni imani yetu kwamba Simba watakuwa wameona udhaifu wao.

Tunapenda pia kuwapongeza SportPesa kwa kuileta Sevilla kwani ni gharama kubwa wametumia lakini yenye nia chanya ya kuendeleza soka la Tanzania na Afrika.

Ni jambo zuri ambalo tunalipongeza na kuwasihi kutokata tamaa kwani soka la Tanzania bado lina changamoto nyingi na linahitaji misaada ya kila namna ndani na nje ya Uwanja.

Itakumbukwa kwamba SportPesa wamewekeza fedha zao kwa Simba, Yanga na klabu zingine za Bara jambo ambalo ni zuri na la kuigwa na makampuni mengine kwa faida ya soka letu. Asanteni SportPesa, hongereni Simba kwa kiwango kizuri.

2 COMMENTS:

  1. Pongezi kutoka ndani na nje zazidi kumiminika Kwa Simba kutokana na kiwango cha kupigiwa mfano kutoka Kwa mabingwa WA soka, jee haijafika wakati Zahera kuona aibu kutokana na msimamo wake WA pekee usioungwa mkono na yeyote pale anapoendelea kuihujumu Simba na TFF kuwa inapendelewa na haistahiki ubingwa?

    ReplyDelete
  2. Simba walicheza vizuri tena sana. Na kitu kilichowaduwaza Sevilla kwa maoni yangu ni soka la Africa. Siku zote huwa sio tulivu ni la kasi ila wazungu wakipata muda kidogo wa kuisoma timu ya Africa utashangaa licha ya soka lao la kasi huishia kufungwa kirahisi sana. Moja ya kitu kikubwa Simba ambao wanatakiwa kujifunza katika mechi na sevilla iwe kwa uongozi,kocha,wachezaji na hata mashabiki wa Simba ni jinsi wachezaji wa sevila walivyokuwa imara katika umilikaji wa mpira wanapoupata kutoka kwa wachezaji wa Simba. Wachezaji wa sevila walitulia na kukaa na mpira kwa umahiri mkubwa badala ya kuupokonya kutoka kwa wachezaji wa Simba na nadhani ni moja ya jambo ambalo timu na wachezaji wetu wanapaswa kujifunza.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic