May 13, 2019


MCHEZO wa kwanza kuteleza kwa Simba ilikuwa mbele ya Mbao FC ambapo walifungwa uwanja wa CCM Kirumba bao 1-0 lililopachikwa na Said Khamis kwa mkwaju wa penalti, kwenye mchezo wa marudio uliochezwa uwanja wa Jamhuri ililipa kisasi kwa ushindi wa mabao 3-0.

Ngoma nzito ilikuwa kwa Kagera Sugar ambao mchezo wa kwanza uwanja wa Kaitaba, Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 wakajipa matumaini watalipa kisasi uwanja wa Uhuru, ngoma ikawa nzito wakawazawadia bao 1 kupitia kwa nahodha msaidizi Mohamed Hussein na kufanya Simba kupoteza jumla ya pointi sita.

Nyuma ya mafanikio ya Kagera Sugar, yupo kocha mzawa mwenye maneno mengi akiwa nje ila kwa wachezaji ni mwenye nidhamu, Mecky Maxime, huyu hapa anafunguka namna alivyoweza kuibana Simba nje ndani huyu hapa:-

"Msimu mzima sikuanza kufanya vizuri, wengi wakawa wananicheka na kunibeza hali iliyonifanya nipate hasira ya kupambana kwani nilijua ni kipindi cha mpito tu niliendelea kuwaandaa vijana wangu kwa ajili ya michezo yetu yote na sio mmoja tu.

Unadhani kwa nini mlikuwa hampati matokeo?

"Tulianza vizuri kwa kupata ushindi mwanzo ila wachezaji walipoanza kujisahau kutimiza majukumu yao ikawa rahisi kwetu kupoteza michezo mingi, nilikaa nao na nikawaambia mwenendo wetu sio mzuri tunapaswa tuzinduke ili tufanye vema.

"Waliniskia ila bado ikawa kuna tatizo kwenye kupata matokeo hasa ukizingatia kwamba kila mchezaji alikuwa ana mfumo wake ambao ameuzoea na anakutana na vitu vipya ndani ya kikosi changu nikajipa matumaini kwamba ni lazima nifanye jambo kuleta mabadiliko.

Tatizo kubwa lilikuwa wapi?

"Safu ya ushambuliaji ilikuwa inaniangusha mwanzo kutokana na kushindwa kutumia nafasi ambazo tunazitengeneza, ilikuwa ni uzito wao pamoja na kutokujiamini ambako kulikuwa kunawasumbua maana kucheza walikuwa wanacheza.

Ulichukua maamuzi gani?

"Kwangu mimi haikuwa tatizo kwa sababu kama timu inacheza na haipati matokeo hauwezi kulaumu, mpira ni kitu ambacho hakifichiki na muda wote kila kitu kipo wazi hivyo hawakunipa taabu nilipokuwa sipati matokeo.

Uliwezaje kuibana Simba?

"Unajua weng wanashindwa kuelewa kwamba mpira ni sayansi na unanjia zake ambazo unapita, ukizizuia inakuwa ngumu kupenya, niliisoma namna Simba inavyocheza na nikajua kwamba ili nishinde ni lazima nami nizibe njia zao.

"Mbinu za Simba ni ngumu licha ya kubadilika mara kwa mara ila aina ya wachezaji inabaki ileile, hivyo hawakuweza kunipa tabu nilipokutana nao na dawa yao nilianza kuiandaa mapema tukiwa Kagera kwenye mchezo wetu wa kwanza, niliwapa majukumu wachezaji wangu na kila mmoja alitimiza jukumu lake.

Ubora wa Simba upo wapi?

"Kikosi cha Simba ni imara hasa ukizingatia wametinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ni hatua nzuri waliyofikia ila haimaanishi kwamba hawawezi kufungika ni mipango tu, kwa timu iliyojipanga inapata matokeo.

"Wanatumia viungo wengi sana hali inayofanya mashambulizi yao yaanzie katikati kuliko pembeni, hivyo kama utawadhibiti kwenye viungo umemaliza nusu ya kazi licha ya kuwa na wachezaji wenye uwezo ila uwanjani hachezi mchezaji mmoja ni timu nzima ndiyo inapambana.

Mwenendo wa ligi unauonaje?

"Kwa sasa ligi ipo lala salama na kila timu inapambana kupata matokeo hasa kwenye mechi hizi za lala salama kwa kuwa timu nyingi hazipo salama.

"Ukitazama namna ambavyo kila timu imepishana pointi na yule ambaye yupo juu utagundua ni kwa alama chache tu moja ama mbili hivyo timu yoyote ambayo itashinda na kupata pointi tatu ni rahisi kupanda na kuwa kwenye kumi bora hivyo hii ni changamoto.

Hali ya Ukata kwako ipoje?

"Janga la timu nyingi hasa zile ambazo hazina wadhamini, kwetu sisi  gharama zote zipo chini ya kampuni sasa tatizo kwa timu nyingine ambazo zinajiendesha zenyewe, gharama ni kubwa kutokana na kutokuwa na mdhamini.

"Ni wakati muafaka kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Kufanya mpango mzuri msimu ujao kuwe na wadhamini ambao watapunguza makali ya gharama kwa timu nyingi ambazo hazina hata mdhamini.

Huwa unawaambia nini wachezaji wako kabla ya mechi?

"Tunakwenda kucheza mchezo mgumu, mechi ipo mkononi mwetu ni lazima tupambane kupata matokeo ninawaamini na mnaweza, hakuna neno lingine la kuwaambia zaidi ya hili vijana wangu.

Kama mkipoteza je?

"Haikuwa bahati yetu, bado tuna nafasi ya kufanya vizuri mchezo wetu unaofuata, mmepambana kwa uwezo wenu ila haikuwa bahati yetu, mnaweza kufanya vizuri mchezo ujao.

Unawaambia nini mashabiki zako?

"Ushirikiano wao ni kitu muhimu kwa kuwa uwepo wao kwenye michezo yetu unatupa hamasa ya kupambana tukiwa uwanjani ili kupata matokeo, shukrani za kutosha kwao kwa kuwa wapo bega kwa bega nasi," anamalizia Maxime.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic