June 23, 2019


MSIBA wa bibi harusi, Diana Jackson aliyefariki dunia kwa ajali wakati akienda kwenye ‘Send Off’ yake Dar es Salaam, umemvuruga mchumba wake hadi kutaka kujiua.  Habari kutoka chanzo chetu zinasema kuwa Elisante Edward ambaye alikuwa mume mtarajiwa wa Diana, alishindwa kuipokea taarifa ya kifo cha mtarajiwa wake na kujikuta akipoteza fahamu.

HABARI KAMILI

“Baada ya ile ajali (iliyotokea Jumatano wiki hii eneo la Mlomboji, wilayani Mbarali mkoani Mbeya na kuua watu wanne akiwemo Diana) kutokea tulipata tabu sana jinsi ya kumfikishia Elisante taarifa. “Maana na yeye alikuwa safari kwenda Dar kwenye Send Off ya mtarajiwa wake, lakini kwa kuwa hakukuwa na taarifa nyingine zaidi ya kifo ilibidi tumwambie.

“Kusema kweli ilikuwa taharuki kubwa, alipoteza fahamu kwa muda, alipozinduka tuliendelea kumfariji,” alisema mtoa habari wetu ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini kwa sababu yeye ni rafiki wa Elisante na si msemaji wa familia.

ELISANTE ASIMULIA

Baada ya kuzungumza na rafiki huyo wa karibu, mwandishi wetu alimtafuta kwa njia ya simu bwana harusi mtarajiwa (juzi Alhamisi) kwa lengo la kumpa pole ambapo alisimulia jinsi alivyoipokea taarifa ya kifo cha mkewe mtarajiwa.

“Baada ya kuambiwa kuwa mchumba wangu amekufa sijui kilichoendelea, nilijiona sipo duniani kwa kuwa nilipoteza fahamu. “Nilipozinduka na kukutana na taarifa ileile ya kifo niliishiwa nguvu, nikawa natamani isiwe kweli lakini haikuwezekana.

“Kila nilipokaa na kufikiria uhusiano wetu, mipango yetu ya maisha nilikosa sababu ya kuendelea kuishi. “Nikawaza kujimaliza na mimi ili uchungu niliokuwa nao umalizwe kwa njia hiyo na si vinginevyo,” alisema Elisente kwa huzuni.

SIMU YAOKOA MAISHA YAKE

Elisante aliongeza kuwa, kila alichokuwa akikiwaza wakati huo wa huzuni kali hakikuwa hitaji la moyo zaidi sana alitamani kufa. “Nilisimamisha kila kitu, nikafunga na mitandao yangu yote ya kijamii ikabaki wazi simu ya mkononi tu.

“Kilichonisaidia sana kutoka kwenye mawazo makali ni simu, ilipokuwa wazi watu wengi wakawa wananipigia na kunipa pole. “Kwa hiyo nikajikuta niko bize kupokea pole na maneno ya faraja kutoka kwa watu mbalimbali kama hivi na wewe umenipigia.

“Basi taratibu ile hali ya kukata tamaa ikaanza kupotea hadi leo niko sawa, yote nimeyapokea na nimemwachia Mungu, ingawa naumia sana,” alisema Elisante.

MANENO YA MWISHO YA DIANA

Mwandishi wetu alipomuuliza aliyekuwa bwana harusi mtarajiwa juu ya maneno ya mwisho waliyozungumza na marehemu kabla ya ajali alisema:

“Kwa kuwa safari yao ilikuwa ni asubuhi nilimpigia simu tukasalimiana na akaniambia wameshaanza safari. “Tukatakiana safari njema na kuahidiana kuwa tutawasiliana baadaye, basi hayo ndiyo yalikuwa mazungumzo na kusema kweli ilikuwa sauti ya mwisho ya Diana kwangu.”

NDUGU WA DIANA KATIKA MAOMBOLEZO MAZITO

Chanzo kutoka ndani ya familia kililiambia Risasi Jumamosi kuwa, maombolezo ni mazito kutokana na kupoteza ndugu wanne kwa mpigo. Katika ajali hiyo iliyohusisha gari dogo namba T 251 DGK aina ya TOYOTA RAUMU aliyokuwa wamepanda bi harusi na nduguze na gari T 213 APW aina ya MITSUBISHI FUSO, watu wanne walipoteza maisha.

Mbali na Diana ndugu zake wengine ambao ni Faraja Jackson, James Jackson na Jocktam Baraka nao walikufa na kuifanya familia hiyo kuwa na msiba wa watu wanne. Kutokana na simanzi hiyo mwandishi wetu hakuweza kufanya mahojiano yoyote na mmoja kati ya wanafamilia hao wa marehemu Diana.

Hata hivyo, tangu ajali hiyo itokee na kuondoka na roho ya bibi harusi mtarajiwa kumekuwa na maombolezo ya aina yake kwenye mitandao ya kijamii ambayo watu mbalimbali wameonesha kuguswa na msiba huo.

“Tukio kama hili ulisikie tu, yaani kufiwa mke katika hali kama hii, sitaki hata kuwaza; Mungu aniepushe na balaa hili, pumzika kwa amani Diana,” aliandika msichana mmoja kwenye ukurasa wake wa Facebook akiambatanisha na picha ya Diana akikata keki siku ya Send Off yake aliyofanyiwa mkoani Mbeya.

TUJIKUMBUSHE

Diana alikuwa katika mipango ya ndoa yake na kwamba amefanya sherehe ya kuvikwa pete ya uchumba, na alikuwa akitarajiwa kufanyiwa Send Off jijini Dar es Salaam kabla ya kufunga ndoa yake na Elisante, Juni 29, mwaka huu.

Lakini kama wasemavyo Waswahili, kazi ya Mungu haina makosa na lolote apangalo yeye huwa; tumuombe Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Diana – Amina

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic