Na Saleh Ally
MIAKA mitatu iliyopita wakati kikosi cha Taifa Stars kambini nchini Uturuki, Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa alilalamika kuhusiana na wachezaji wavivu wa mazoezi. Kati ya aliowataja alikuwa ni Ibrahim Ajibu na Abdi Banda.
Mkwasa alimueleza Banda mbele yetu tuliokuwa mazoezini katika kambi katika Mji wa Kartepe, Uturuki kwamba kama atamuita tena akaumia wakati wa mazoezi ya kupima utimamu wa mwili, basi hatamuita tena kwa kuwa kuumia kwenye mazoezi hayo ya mwanzo ya kambi ni ishara tosha ya uvivu.
Tukiwa Uturuki nilipata bahati ya kuzungumza na Banda ambaye alilalamika kiasi fulani lakini kuna ambayo alikubaliana nayo. Kuanzia hapo, nikawa na ukaribu na Banda kama mdogo wangu tukikumbushana masuala kadhaa.
Banda alibadilika na huenda kati ya wachezaji wanaoaminika ni makini na kazi, wanaopenda na kutimiza haki ya mazoezi ni Banda. Wakati nikiwa Afrika Kusini kumfanyia mahojiano, nilibahatika kuzungumza na kocha wake, Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi la Baroka FC, Dokta Khumalo ambao wote walimsifia na kunieleza kumteua kuwa mmoja wa manahodha wa timu hiyo.
Wakati Banda akiwa amebadilika, mara zote tumesikia kuhusiana na suala la uvivu wa mazoezi wa wachezaji kadhaa nyota mfano Ajibu, Jonas Mkude na wengine. Kila mmoja anakubaliana na kipaji walichonacho lakini tatizo kubwa limekuwa ni suala la uvivu au nidhamu.
Kawaida, unapokuwa mvivu wa mazoezi, maana yake huna nidhamu. Kama utekelezaji wako wa mazoezi utakuwa wa kiwango cha chini, maana yake husikilizi kile ambacho unaelezwa na kocha au makocha wengine.
Nidhamu ya chini imewaangusha sana wachezaji wengi nchini ambao baadhi yao wamekuwa kipenzi cha mashabiki wa soka ambao hawajui undani wa wachezaji hao.
Jana, Kocha Mkuu wa Taifa Stars ametangaza kikosi cha wachezaji walioondoka kwenda Cairo kwa ajili ya kambi akiwa amewatema wachezaji saba wakiwemo Ajibu na Mkude ambao wamezua gumzo kubwa.
Ajibu amecheza Simba na Yanga, Mkude amekuwa Simba tu na wote wamekuwa vipenzi vya mashabiki wa timu hizo mbili na hasa Simba kwa kuwa ni vijana waliokulia katika timu yao ya vijana.
Hakuna ubishi, Ajibu na Mkude wamekuwa kati ya wachezaji wanaozungumzwa katika masuala ya nidhamu na mara kadhaa wamekuwa wakiingia katika msigano na baadhi ya makocha na sote tunalijua hili.
Mkude na Ajibu wana vipaji, lakini adui mkubwa wa vipaji vyao ni ukosefu wa juhudi sahihi, nidhamu ya kutosha kuwafanya waviendeshe vipaji vyao. Ni sawa na kusema gari yenye uwezo wa kubeba tani 10 lakini matairi yake ni yale yenye uwezo wa tani tatu hadi tano.
Kuna tatizo kubwa kwa Ajibu na Mkude na wengine wa aina yao. Tumesikia matatizo mengi sana lakini ushabiki umewafunga macho wadau wengi wa soka, wameendelea kuwaunga mkono wachezaji hao kwa kuwa wana uwezo wa kutoa pasi nyingi za mabao au kupiga pasi wanapokuwa uwanjani.
Ushabiki umewafanya wachezaji waendelee kuwa na hisia za kifalme, ambazo zinawainua kwa maana ya hisia lakini uhalisia unawaangusha. Kila wanachoambiwa si sahihi, wanaona wanaonewa kwa kuwa jamii inayowazunguka imekuwa na unafiki badala ya urafiki kwao.
Unafiki kwa kuwa wanaowatetea wanajali furaha wanayoipata kutoka kwa wachezaji hao kutokana na ushabiki lakini uhalisia ni kweli hawako sahihi na lazima wajipime kwa kuwa haiwezekani makocha wazalendo, wageni wote wawe wanawaona wachezaji hao wana tatizo.
Katika maendeleo ya mpira, umahiri kutokana na kipaji pekee haumfanyi mchezaji kuwa bora zaidi. Sote tunajua kuhusiana na kipaji cha Mbwana Samatta lakini sote tunafahamu ubora wa nidhamu yake ambayo kwa jumla, leo anakuwa mfano namba moja wa kuigwa.
Sote tunajua, kwa asilimia kubwa Ajibu anaweza kuwa na kipaji cha juu hata kuliko Simon Msuva, lakini angalia hatua na maendeleo ya Msuva na Ajibu, ni mbingu na ardhi na bahati mbaya wenye mapenzi na wachezaji hao tunashindwa kuwasaidia kwa visingizio tofauti lakini kikuu ni madai kuwa wanaonewa.
Ajibu na Mkude, pia wengine wenye tabia kama zao lazima wajipange na kubadilika kwa kuwa dunia imebadilika kwa kuwa wachezaji wasio na vipaji vya kutisha, wamekuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri kutokana na kiwango kikubwa cha nidhamu wanachokuwa nacho.
Wachezaji wenye vipaji ndiyo wamekuwa wakihangaika, wakipata nafasi ya kutamba kwa muda mfupi sana kwa kuwa nidhamu ni msingi mkuu wa maendeleo na mafanikio kwa wachezaji na si kipaji pekee.
Endeleeni kuwatetea Ajibu na Mkude, wao pia wandelee kufanya wanachoamini ni sahihi licha ya kwamba ni sahihi, mwisho wake wataendelea kushuhudia wale ambao wanaamini ni wa kawaida wakisonga mbele na kucheza Ulaya kwingineko kwenye mafanikio zaidi.
Angalia, leo Ajibu anabaki lakini Miraji Athuman wa Lipuli FC anakwenda Afcon, tafakari hili au Mkude anabaki halafu Mudathir Yahaya, kinda zaidi kwake au Fred Tangalu wa Lipuli FC wanakwenda Afcon.
Unaweza kuchukulia kawaida lakini kwa uhalisia katika hili, mpongezeni Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike kwa kuwa uchaguzi wake unaonyesha umeangalia vigezo sahihi badala ya majina tu, kama ambavyo kocha wa Simba anaweza akasumbuliwa na Mkude lakini akaamua kukaa kimya kwa hofu ya mashabiki au baadhi ya viongozi wanaompenda Mkude.
Kuna kitu cha kujifunza na Mkude na Ajibu kwa walipofikia, si jambo sahihi wao kushindwa kwenda Afcon.
Lakini aliyewafanya washindwe kwenda ni wao wenyewe na wadau tukitaka tuwe sehemu ya kusaidia, basi tunapaswa kuwa wakweli kwao badala ya kuishi nao kinafiki tukiwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa mwisho wao ndiyo unakuwa huu wa kuishia Dar es Salaam na Cairo kuishuhudia runingani.
Makala ni mazuri Sana na natamani watajwa wayaone na kuysoma Kwa Makini na iwe fundisho Tosha. Anayekunasihi anakuthamini na kukupenda na kukutakia maisha katika maisha yako
ReplyDeleteKwani kocha wa Simba anaishi vipi na Mkude licha ya matatizo yake ya nidhamu lakini anabaki kuwa msaada kwa Simba?
ReplyDeleteVipi Zahera aliwezaje kuishi na Ibrahimu Ajibu Yanga hadi kumkabidhi ukapteni? Vipi Juuko anaedaiwa kuwa mkosefu wa nidhamu lakini kunako uahai subiri atakavyokinukisha kule Misri. Kwa maoni yangu tayari benchi la ufundi la taifa stars limeshakuwa na kasumba hiyo yakwamba wachezaji fulani hawana nidhamu kwa hivyo hawafai na wanachotafuta ni kajikasababu fulani hivi. kwanini wasiwape second chance wakawaangalia ufanisi wao ndani ya timu ya Taifa kwani kwa hakika ndani ya Taifa stars ukifuatilia ndani ya stars ya Amunike akina Ajibu hawakuwahi kupewa hata first chance ya kuonesha uwezo wao. Kuna wachezaji hata wanaocheza nje hawapo vizuri kulinganisha na Ajibu na Mkude. Hasa Jonasi mkude amekuwa moja ya wachezaji wa Simba waliochangaia kwa kiasi kikubwa kuisaidia Simba kufika ilipofikia kwenye klabu bingwa Africa. Na hii leo hakuna ubishi tena kwa soka la Tanzania linepiga hatua moja mbele kwa msaada wa Simba na sio timu ya Taifa.Hata vilabu vya kwao Amunike vilishia mapema tu kwenye klabu bingwa Africa na kuwaacha akina Mkude wakipambana na waalgeria,wakongo,wazambia,wamisri na kipi hasa kitakacho mzubaisha mkude kule Afcon kwa sasa? Pale stars kuna kiungo gani wa kusema mkude hana nidhamu tunamchukuwa huyu? Kweli wapo wachezaji wenye vipaji ila suala la uzoefu ni moja ya kitu muhimu kwa mchezaji hasa mashindano makubwa kama AFCON.
lakini leo wachezaji wale wale waliliongezea thamani soka letu tunakwenda kuwavunja moyo kwa maneno mepesi kuyatamka lakini ni mazito katika kuichafua taswira ya mtu kuwa "hana nidhamu" kwani kazi ya ualimu ni nini hasa? Niltarajia mtu kama Amunike angekuwa mweledi zaidi kuishi na wachezaji watukutu na kwa kutumia taaluma na uzoefu wake katika maisha ya mpira kuweza kuwabadisha hawa wachezaji kuwa msaada zaidi kwa timu ya Taifa badala ya kuwafukuza kwani anachokifanya kwa Mkude na Ajibu sio kwamba ana nia ya kuwasidia ili wajirekebishe hapana,anachokifanya ni kuwavuruga kabisa hawa vijana kisaikolojia badala ya kuwajenga. Ni kuwakatisha tamaa. Kwa wenzetu kijana au mchezaji anapoonekana kuwa na uwezo au kipaji huwa wanatumia njia za busara zaidi na jitihada za ziada katika kuwaongoza katika misingi sahihi ya kazi yao kwani binaadamu wote hawawezi kuwa sawa. Tumekuwa tukishindwa kuyaanika wazi Mapungufu ya Amunike katika taaluma yake na kuwasakama zaidi wachezaji kana kwamba yeye ni malaika ila asipojirekebisha basi tutavuna tulichokipanda kwa taifa stars muda si mrefu kule Misri .
Practically Ausems anamwamini zaidi Kotei kuliko Mkude na hata mashabiki wa simba licha ya kumpenda Mkude wamethibitisha wanamkubali zaidi Kotei....rejea Mo simba awards.Kwaiyo hawa makocha wote waliopita simba na stars wanamchukia na mkude/Ajibu. Kwann Ausems anataka asajiliwe kiungo mwingine mkabaji kama mkude ambaye anazidiwa na Kotei ni wa kuaminika.Mkude sio bora lkn ni mchezaji mzuri na hapa duniani hakuna kocha mwendawazimu anaweza kumwacha mchezaji bora.Subiri simba wasajili halafu uone kama Mkude atavyosubiri.Ajibu ni mchazi mzuri tena kwa mechi ndogondogo....lkn msimu huu ulioisha kwenye mechi kubwakubwa eg.dhidi ya Azam, simba, mtibwa alipotei kabisa.Kama isivyowezekana kila mmoja kuwa daktari ndio isivyowezekan kila mtu akawa kocha....tujifunze kuheshimu taaluma na Ajibu na Mkude tuwaambie ukweli kama tunawathamini.Wasipodilika basi wayasubiri yale ya Boban na Chuji ambao licha ya kuwa na vipaji vikubwa kuliko Ajibu na mkude lkn kwao mpira haujawa na faida.
DeleteUmeongea point kazi ya MWL no kujenga psychologia ya wachezaji na kupandisha nidhamu iweje huyu amunike? Yetu macho pia ajifunze ugerman walicho Fanya kombe LA dunia ndo yatatukuta haraf Dauda mkosowe amunike kwa kutokua baba bora kwa wachezaji hawa wawili aslay alsema mtoto akinyea mkono usiukate uoshe iweje yy awachukie kiasi hicho amunike sio BABA
ReplyDeleteHUYU COACH NI PROFESSIONAL NA UKIANGALIA WACHEZAJI ALIOWACHAGUA UTAGUNDUA KUA
ReplyDeleteIBRAHIM AJIB NA MKUDE HAWANA NAFASI PALE NA HASA UKIANGALIA STYLE YA UCHEZAJI WAO
WA KUCHEZA NA JUKWAA KWA MADOIDO HAKUTATUSAIDIA KULE MISRY MAANA TUNAKUTANA NA TIM
NGUMU INAHITAJI TUFIGHT HADI DAKIKA YA MWISHO . COACH AACHWE HADI ATAKAPOSHINDWA KISHA MUWALETE HAO WANAOCHEZA KWA MARINGO TURUDI KUA KICHWA CHA MWENDAWAZIMU NA MKUMBUKE HAO KINA AJIBU HAWAJATUINGIZA AFCON HADI TUSHADIDIE UWEPO WAO - CIAOOOOO
Wakati mwengine kusoma sio kuelemika unaweza kusoma ukabakia kuwa mpumbavu.Rudi nyuma kaangalie Simba vs Nkana vipi Simba waliweza kurudi mchezoni baada ya kuwaruhusu Nkana kupata bao la ugenini. Halafu ikiwezekana kaa chini kidogo angalia Simba vs Ahly pale kwa mkapa. Kuongea vitu bila ya ushuhuda ni majungu.
ReplyDeletetimu nzuri inacheza vizuri popote pale na udhaifu wa simba unaonekana pale wanapocheza ugenini angalia mechi ya nusu fainali mazembe alishindwa kuwafunga waarab pale pale kwao Congo !!
ReplyDeleteMazembe kwa Simba wawahukuru Yanga na Zahera wao kwa kuiwangia Simba zidi ya Mazembe. Na ukiangia kwa undani utakugundua kuwa kwenye bongo za baadhi ya wabongo ndani yake mna kinyesi badala ya akili kwani Yanga povu lilikuwa linawatoka kwa hasira kila wakati Simba ilipokuwa ikisonga mbele hadi kuonesha juhudi zao za kuzisapoti timu pinzani za Simba lakiki matokeo yake kumbe juhudi za Simba ni kwa manufaa ya Yanga. Sawa na msafiri anaemfurahia mtu anaetoboa jahazi anayosafiria kisa tu kwa sababu anaetoboa jahazi hatoboi upande aliokaa yeye?
ReplyDeleteAJIB NA MKUDE WAKUBALIANE NA HALI HALISI NA WAJIFUNZE
ReplyDeletemwalimu amunike nae ana kasumba yake,nae tuache unazi anapenda kusujudiwa ,kwa soka la kileo halipo hivyo .
ReplyDeleteNaomba kuuliza kwenye mechi za kufuzu Afcon AJIBU NA MKUDE Walishiriki????
ReplyDeleteHapana hawakushiriki na ndio maana tunasema sio suala na nidhamu pekee bali kuna namn.
ReplyDeleteKocha ni kama mzazi.. Huwezi kuwatimua watoto wako muhimu wenye msaada adhimu kwenye safari muhimu kisa wamekushinda "tabia".. Kama mzazi kukubali kushindwa na watoto ni ishara ya mapungufu ya moja kwa moja..
ReplyDeleteAnyway haya tuyaache..
Muhimu ni kufahamu kuwa tulikuwa timu ya kwanza kuripoti Misri..
Je, tumejipanga vipi kisaikolojia ikitokea sisi ndo tuwe timu ya kwanza kuyaaga mashindano?