July 12, 2019


TAYARI muda unazidi kukimbia kwa kasi ambayo haiwezi kuzuilika hivyo ni muda mwafaka kwa kila timu kuanza kujipanga kwa ajili ya msimu unaofuata.

Kwa sasa ni usajili tu ndio umepamba moto hili haliepukiki ni lazima kila timu ifanye usajili kwa kuboresha kikosi na kukifanya kiwe cha ushindani msimu ujao.

Ambao bado hawajaanza kufanya maandalizi kwa ajili ya msimu ujao hata kwa kuaandaa mipango kazi wanajiweka kwenye mazingira magumu ligi ikianza.

Viongozi wa timu pamoja na benchi la ufundi ni muda wa kukaa na kufanya mipango makini kwa ajili ya msimu mpya unaofuata.

Wengi wanajisahaulisha baada ya ligi kuisha wanadhani wamemaliza kila kitu kumbe kuna mambo ambayo yanapaswa yafanyiwe kazi.

Kuangalia mapungufu ambayo msimu uliopita yalisumbua na kuanza kuyafanyia kazi ni vitu vya muhimu kwa muda huu kabla ligi haijaanza.

Kufanya maandalizi ya awali na kukaa na timu ni jambo ambalo haliwezi kuepukika hasa ukizingatia kwamba wengi wanafanya usajili.

Muda wa maandalizi ya awali utakuwa muda wakuwafanya wachezaji wawe kitu kimoja na benchi la ufundi kutambua aina ya kikosi walichonacho.

Pia wale ambao wanapuzia kufanya maandalizi ya awali ni muda wao kushtuka kwamba kama hawatafanya wakati huu wakati ujao watavuna kile walichokipanda.

Isiwe maandalizi yapo kwenye timu ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara pekee bali iwe na kwa zile ambazo zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza nazo ni lazima zifanye maandalizi.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mipango yao iwe wazi na itazame makosa ambayo yalitokea msimu uliomalizika kwa sasa yasijirudie.

Kwa kuwakumbusha tu kama watakuwa wamesahau suala kubwa la viporo kwa msimu uliopita lilivuruga na kuua kabisa utamu wa ligi.

Ilifika wakati timu zimemaliza mzunguko wa kwanza nyingine bado zilikuwa hazijacheza mechi nyingi hii ilikuwa inavuruga na kuua kabisa ushindani wa ligi.

Hapa kuna jambo la msingi ambalo linatakiwa kufanyika hasa msimu mpya ambao unatarajiwa kuanza Agosti 23.

Ratiba iliyopangwa na kuwekwa wazi na Bodi ya Ligi Tanzania ni lazima ifuatwe na izingatie kanuni ambazo zimewekwa.

Kwa kufanya hivyo kutafanya ligi iwe bora na yenye ushindani hali itakayoongeza mvuto wa ligi msimu mpya.

Ligi isivurugwe bali ipewe thamani kubwa itakayofanya kila mmoja apende kuitazama na kuifuatilia bila kujali timu gani inacheza.

Kwa upande mwingine suala la viwanja limekuwa tatizo kubwa hasa kwa timu nyingi kutokuwa na viwanja vyao vya kudumu.

Viwanja vingi ambavyo msimu ulipota vilitumika viwango vilikuwa vya chini jambo lililofanya matokeo kuwa ya shida kupatikana kutokana na ubora wa viwanja.

Mfano ukitazama hali halisi ya viwanja vyenye ubora bado ni vichache sana na vinahesabika tofauti na idadi za timu ambazo zipo.

Vuta picha uwanja wa Mkwakwani ambao unatumika na timu ya Coastal Union ya Tanga namna ulivyo timu inacheza kwenye mazingira magumu.

Pia ukienda Namfua pale Singida ni shida kupata matokeo chanya kwa timu ambayo haijauzoea uwanja na hata wenyeji wakati mwingine wamekuwa na taabu kupata matokeo.

Ni muhimu kwa TFF kuweka masharti magumu kwa kila timu ambazo zinashiriki ligi kuwa na viwanja bora na kuvikagua kabla ya ligi kuanza ili kuepusha sababu ambazo zinaweza kuepukika.

Bora kuwa na viwanja vichache ambavyo vinakidhi viwango kuliko kuwa na viwanja vingi ambavyo havikidhi viwango kwa ajili ya kuchezea.

Uwanja kama ule wa Samora upo vizuri na unaleta raha kwa timu kucheza michezo yao pale kwani ni sehemu bora na inapendeza.

Ukigusa na Azam Compex nao pia wamewekeza na wanapaswa kuwa mfano kwa timu zote hapa Bongo hasa kwa uwekezaji na namna ambavyo wanaendesha timu zao.

Napenda kutoa rai kwa TFF msimu huu waongeze zaidi umakini na kufanya kazi kwa weledi ili kuiboresha ligi yetu iwe na msisimko tofauti na muda mwingine.

2 COMMENTS:

  1. Hivi unaanzaje kuwashauri au kuwakosoa TFF japokuwa wana mapungufu wakati wewe mwenyewe na timu yako ya waandishi wa blog ni majanga.Nakushauri kabla hujawanyooshea kidole TFF ungeanza wewe kurekebisha mapungufu makubwa katika uandishi wenu wa habari usio na mwelekeo na wenye kukera wengi.Habari nyingi ni za kupika kiasi kwamba inafikia vichwa vya habari na habari yenyewe ni tofauti kabisa na ukisoma kwa makini unagundua ni habari za kutunga.ANZA WEWE KWANZA KUJIREKEBISHA ILI TUKUUNGE MKONO UNAPOKOSOA WENGINE...

    ReplyDelete
  2. Unawashauri nini hao tff wapo hapo kwa maslahi yao na kujaza matumbo yao tu viporo vingi vilifanywa kwa malengo maalum na wewe mwandishi unalielewa hilo sasa hivi unajifanya msahuri kwa jinsi unavyojitoa fahamu na nyinyi tff ni wakati wa kukaa pembeni mshathibitisha mmefeli kabisa tena wala hamna weledi wa uongozi wa mpira na huyo Wambura wenu hamana kitu kabisa debe tupu kwa ufupi muondoke msingoje aibu,mmeshindwa hata kwenda kwenye mkutano na Waziri wa michezo.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic