July 12, 2019

DIRISHA la usajili linaendelea kwa sasa ambapo timu nyingi zinajipanga kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 23.

Kuna umuhimu mkubwa kwa kila timu kuanza maandalizi mapema kwani matokeo chanya uwanjani yanatengenezwa na maandalizi ya awali ambayo timu huwa zinafanya.

Muda wa kufanya haya yote ni sasa kwa kuanza na usajili makini pamoja na kambi bora zitakazofanya kila timu kupambana kikamilifu msimu ujao.

Kwa timu zote bila kujali zinashiriki Ligi Kuu Bara ama Ligi Daraja la kwanza ni muhimu kujipanga vema.

Wale ambao wamekuwa wakifanya usajili kwa mapezi yao ama kutumia nafasi zao za uongozi si sawa kwani anayejua uhitaji wa wachezaji ni kocha mwenyewe.

Itapendeza endapo viongozi watafuata ripoti ya kocha kwenye kufanya usajil jambo liakaloepusha lawama na malalamiko kwa benchi la ufundi kwani wao ndio wanahusika kwenye suala la kupanga timu.

Kwa kupitia yale mapungufu ambayo benchi la ufundi limeyaona hapo ndipo kazi inabidi ifanyike na sio kusajili kwa kufuata mkumbo.

Kila mmoja amekuwa ana mamlaka hasa linapofika suala la usajili kulingana na mapenzi ambayo anayo kwa mchezaji ama wengine ni wale ambao wanaona kwamba watapata faida endapo watamsajili mchezaji fulani.

Sasa suala la kutazama faida huwa linakuwa kwa muda tu tofauti na yule ambaye atasajili kwa kufuata mapendekezo ya mwalimu itasaidia kujenga kikosi imara.

Ikumbukwe kuwa wakati timu ikiboronga anayepewa mzigo wa lawama siku zote huwa ni mwalimu hivyo itakuwa vizuri endapo ripoti itafanya kazi lawama zitakuwa haziepukiki kwake.

Naona timu nyingi zinapambana kutafuta wachezaji ambao wanaona kwamba wanawafaa kwenye kikosi chao kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao.

Tukiachana na suala la usajili wa ligi ambao unaendelea kwa sasa ngoja tuzungumzie pia suala la maandalizi ya michuano ya CHAN ambayo inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Muda mzuri kwa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya timu yetu ya Taifa ili ifanye vema na kuwatoa kimasomaso mashabiki.

Ikumbukwe kwamba timu imefanya vibaya kwenye michuano ya Afcon ambayo inaendelea nchini Misri huku timu yetu ya Taifa ikitolewa kwenye hatua za awali.

Kwa sasa itakuwa vema wachezaji wakitumia michuano hii kufanya ushindani wa kweli na kupata matokeo chanya kwenye michuano ambayo inatajia Kuanza hivi karibuni.

Kama wachezaji watatumia vema michuano hii ya CHAN itarudisha ile imani ambayo ilikuwa imeanza kupotea kwa mashabiki na kuwafanya wawe kitu kimoja.

Mashabiki wanapenda mpira hii ipo wazi na haiwezi kufichika kwani ukirudisha kumbukumbu kwenye mchezo wa mwisho ambao ulichezwa uwanja wa Taifa mashabiki walionyesha mapenzi yao wakati timu ilipocheza na Uganda.

Wachezaji wanapaswa watambue kwamba wana kazi ya kufanya kurejesha imani kwa mashabiki na kazi yao ni moja tu kupata matokeo chanya.

Maandalizi mazuri kwa timu ya Taifa yanapaswa yaanze kufanyika sasa kabla ya kuanza kujutia hapo baadaye ikitokea tukaboronga tena.

Kila kitu kwenye soka kinawezekana na ipo wazi kwa muda huu malipo ya wachezaji yawe wazi na wajitoe kwa moyo mmoja kufanya kazi na kutafuta matokeo.

Benchi la ufundi litazame namna bora ya kufanya kuongoza kikosi kiwe na ushindani na morali bora kwenye michuano hii ya ndani.

Nidhamu inapaswa ipewe kipaumbele na wachezaji waingie kazini kwa juhudi kubwa bila kutafuta matokeo wakiwa ndani ya uwanja.

Mashabiki pia tusiwe nyuma katika hili kazi ya kutoa sapoti ni muhimu kwani uwepo wa mashabiki unaongeza morali na hamasa kwa wachezaji wakiwa uwanjani.

Bado tuna imani na timu yetu hasa ukizingatia kwamba wachezaji wengi wameanza kutambua thamani ya kucheza ndani ya timu ya Taifa.

Wale watakaochaguliwa kuitumikia timu ya Taifa wafanye kazi kwa moyo kupeperusha Bendera ya Taifa kwani watakuwa wameaminiwa kiasi kikubwa.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic