LEO uwanja
wa Uhuru, Simba akiwa na hasira zake za kutolewa kwenye michuano ya
kimataifa na UD do Songo kwa faida ya bao la ugenini anaanza hesabu zake kutetea
kombe la Ligi Kuu Bara mbele ya JKT Tanzania.
Rekodi
zinaonyesha kuwa msimu uliopita, JKT Tanzania ambayo ilikuwa imepanda Daraja
iliacha pointi zote sita mikononi mwa Simba.
Mchezo wa
kwanza uliochezwa uwanja wa Mkwakwani, Tanga, JKT Tanzania ilikubali kupoteza
kwa jumla ya mabao 2-0 huku mfungaji akiwa ni Meddie Kagere na mchezo wa pili
uwanja wa Uhuru ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Ripoti za
daktari wa JKT Tanzania iliyo chini ya Mohamed Abdallah ‘Bares’ ambao waliweka
kambi visiwani Zanzibar zinaonyesha kwamba mpaka sasa hakuna majeruhi hata
mmoja na wote wapo na morali ya kufuta gundu la msimu uliopita.
Bares
amesema kuwa wachezaji wana morali kubwa ya kupambana na amewapa
majukumu maalumu kwenye mchezo huu muhimu na mgumu.
Kwa upande
wa Simba iliyo chini ya Mbelgiji, Patrick Aussems yeye atawakosa wachezaji wake
muhimu ambao ni John Bocco, Wilker Henrique ambao wanasumbuliwa na goti pamoja
na Jonas Mkude ambaye anahoma.
Aussems amesema wapo tayari na wamejipanga kuanza kufanya vema mbele ya JKT Tanzania leo.
0 COMMENTS:
Post a Comment