August 21, 2019



MOTO wa Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na ule wa Kombe la Shirikisho umeanza kuwaka kwenye viwanja tofauti ambapo wawakilishi wetu wanapambana kupeperusha Bendera ya Taifa.

Tanzania imepata fursa ya kuwa na timu sita ambazo zinapeperusha Bendera kimataifa hivyo ni fursa nzuri kwa wachezaji pamoja na timu kuandaa mambo mazuri kwa ajili ya mashabiki wao.

Tumeona Timu ya Taifa ya Wanawake ‘Tanzanite’ wametwaa Kombe la COSAFA, wanastahili pongezi kwa hilo.

Hii inamaanisha kwamba kila kitu kikipangwa kinawezekana kutokea vile ambavyo tunafikiria, uwe mwanzo na mwendelezo kwenye michuano mingine.

Kwa upande wa Tanzania kuna Simba, Yanga ambazo hizi zipo upande wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam FC na KMC wao wakipeperusha Bendera kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Visiwani Zanzibar ni KMKM ambao hawa wanawakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Malindi kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Tumeona mechi za mwanzo timu zote zimeonyesha jitihada ya kupambana kusaka matokeo ambapo Simba, KMC, na Malindi walikuwa ugenini na wamelazimisha sare ya bila kufungana.

Simba wao walikuwa nchini Msumbiji walimenyana na UD Songo ya Msumbiji, KMC ilikuwa Rwanda ilimenyana na AS Kigali huku Malindi ya Zanzibar ilikuwa Somalia ikicheza na Mogadishu City.

Hili ni fungu la kwanza ambalo kazi yake sio ya mchezo kwani wengi wanajipa nafasi ya kupata matokeo na kusahau kwamba kwenye mpira kila timu inatafuta matokeo chanya.

Kwa sare walizopata hawa wawakilishi wetu kimataifa kazi yao kubwa ni kupanga mikakati imara na sio kujipa matumaini kwamba watapenya wasipojipanga wataangukia pua.

Mechi za marudio zitakuwa nyumbani hivyo kazi yao kubwa ni kutumia vema fursa ambayo wapinzani wao wameshindwa kutumia mwanzo kwani kwa sasa kila timu inapambana kupata matokeo.

KMKM ina kumbukumbu  ya kupoteza kwa kufungwa mabao 2-0 na de Agosto ya Angola wana kazi ya kwenda kupindua meza ugenini na inawezekana kukiwa na nia ya kutafuta ushindi.

Kwa upande wa Azam FC ambao walipoteza mbele ya Fasil Kenema naona bado ina nafasi ya kupenya hatua hii ya awali ya michuano ya kombe la Shirikisho.

Watanzania katika hili tunatakiwa kuungana na kuzipa matumaini timu zetu kuelekea kwenye michezo ya marudio ili wapate matokeo, Azam wanautambua vema uwanja wao wa Chamazi kazi yao itakuwa moja tu kuwafunga wapinzani wao.

Naona wengi kama wameanza kuipotezea ramani Yanga na kuipa kiburi Simba kwamba itapata matokeo hakuna wepesi katika michuano ya kimataifa hasa kwenye mechi za awali.

Hivyo nina amini Yanga inakwenda kufanya kitu cha kipekee kwenye mchezo wa marudio dhidi ya Townshp Rollers ya Botswana na wengi hawataamini.

Kitu pekee ambacho Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera anapaswa kukifanya kwa sasa ni kurekebisha makosa madogo ambayo yameonekana kwenye mchezo wa kwanza.

Kwa namna ambavyo wachezaji wamecheza mchezo wa kwanza kuna kitu ambacho kimejificha hasa kiuwezo hicho ndicho ambacho kinapaswa kitumike mchezo wa marudio.

Kuruhusu kufungwa kwenye michuano ya kimataifa hatua ya awali sio matokeo mazuri ila kwa kuwa nao wamefunga bao basi safu ya ushambuliaji ina mzigo wa kufanya vema mchezo wa marudio.

Safu ya ulinzi inatakiwa iongeze umakini na kufanya maboresho madogo ambayo walikuwa wameshindwa kuyafanya wakati walipocheza Uwanja wa Taifa.

Imani yangu ni kwamba ukubwa wa Taifa na michuano ilivyo kila timu ina nafasi ya kupenya jumla endapo itapambana na mikakati ikiwa makini.

Zile ambazo zinajipa nafasi ya kushinda zinapaswa ziwe makini zisijiamini kupita kiasi zitapoteana uwanjani na habari yao itaishia hapo, mpira ni mchezo unaohitaji nidhamu na umakini.

Mashabiki kwa michezo ambayo itakuwa nyumbani ni wajibu kujitokeza kuzisapoti timu zetu zikiwa uwanjani kuzipa sapoti.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic