Aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amelitaka benchi la ufundi ndani ya timu hiyo chini ya Kocha Mbelgiji, Patrick Aussems, kumpanga Aishi Manula katika mechi ya leo dhidi ya Kagera Sugar itakayopigwa uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.
Simba itakuwa na kibarua kizito ambacho kitakuwa cha kulipiza kisasi katika mechi ya Ligi Kuu Bara baada ya kufungwa mechi zote mbili na walima miwa hao wa Kagera msimu uliopita.
Kihwelo ameamua kutoa ushauri huo kutokana na kauli aliyoitoa Kocha wa Kagera, Mecky Maxime siku chache zilizopita, kuwa endapo Manula atapangwa watakuwa na urahisi wa kupata matokeo sababu wanajua udhaifu wake.
Kihwelo ameeleza kauli ya Maxime waitumie kwa kuendelea kumchezesha Manula kwani itawasaidia kisaikolojoia kwani Kagera wayaingia na lengo la kumfunga kirahisi.
Amesisitiza si vema wakamtumia kipa namba mbili ambaye ni Beno Kakolanya na badala yake wamtumie yuleyule Manula maana anaamini ataweza kusahihisha makosa yake.
"Kocha anapaswa kumtumia Manula langoni sababu ndiye atawaharibu kisaikolojia Kagera Sugar, hiyo kauli ya Maxime itakuwa imewasaidia mno na wanaweza kupata matokeo.
"Naamini Manula akipewa nafasi hiyo atakuwa anaingia uwanjani tayari akiwa anafahamu kipi Kagera wanahitaji hivyo lazima ajipange kuwaonesha kuwa hayupo tayari lango lake kuguzwa.
Kwa upande mwingine, Julio ambaye aliwahi pia kucheza Simba, amewataka wachezaji wa timu hiyo kuingia uwanjani wakiwa hawana presha ili kucheza vizuri, lasi sivyo historia ya Kagera Sugar kuendelea kupata matokeo mbele yao itazidi kuendelea.
Katika mchezo wa mwisho msimu uliopita, Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0 ambalo alijifunga beki Mohammed Hussein na kuipa Kagera alama tatu muhimu kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
0 COMMENTS:
Post a Comment