INAUMA!!! MTOTO MBEYA AIBWA KIMAFIA
MBEYA: INAUMA sana! Ni maneno ambayo mtu yeyote anayejua uchungu wa mtoto anaweza kuyatamka kutokana na mtoto Herieth Ismail mwenye umri wa miezi sita kuibwa kimafia, Ijumaa Wikienda linakupa habari kamili.
Akielezea kwa masikitiko mama wa mtoto huyo, Elizabeth Mgina(22) ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mwenge Kata ya Ruanda jijini Mbeya alisema tukio hilo lilitokea Agosti 29, mwaka huu majira ya jioni eneo la Soko la Soweto.
Aliendelea kusema yeye ni mfanyabiashara wa vitunguu katika soko hilo ambapo alifuatwa na mwanamke mmoja aliyechukua vitunguu vyenye thamani ya shilingi elfu moja lakini akawa hana fedha akamwambia waongozane kwenda kwake kwa ajili ya kuchukua fedha yake aliyokuwa akimdai.
Walipofika njiani uelekeo wa Hospitali ya Uhai Baptist mwanamke huyo aliomba kumpokea mtoto aliyekuwa amebebwa kwa nia njema hivyo Elizabeth alimpatia mtoto wakaendelea na safari.
Wakafika eneo la Sekondari ya Ihanga umbali wa mita mia moja hamsini kutoka Soweto, mwanamke huyo alimwambia amsubirie nje amchukulie pesa anayodaiwa huku akiwa amembeba mtoto Herieth.
Baada ya dakika tano alimfuata alipoingilia mwanamke huyo akagundua kuna vichochoro viwili ambavyo alihisi kupita mwanamke huyo na kutokomea kusikojulikana.
Hata hivyo baada ya kubaini kuibiwa mtoto, Elizabeth alitoa taarifa kwa mjumbe ambaye alishirikiana na wananchi kumtafuta mwanamke huyo bila mafanikio.
Aidha alimpigia simu muwewe aliyefahamika kwa jina la Ismail Sinjelwa(25) ambapo walisaidiana kutafuta hatimaye kutoa taarifa kituo cha Polisi Ilomba ambapo waliambiwa waendelee kumtafuta na baada ya saa ishirini na nne warudi tena.
Elizabeth alisema mwanaye ni mweupe hivyo yeyote atakayemuona mwanamke mwenye mtoto anayemtilia shaka atoe taarifa kwenye kituo chochote cha polisi kilicho karibu.
Kwa upande wa Mjumbe wa Mtaa wa Mwenge, Eliah Tuja alisema baada ya kupata taarifa walisaidiana kutafuta pia kuwashauri kutoa taarifa polisi.
Mjumbe huyo alitoa wito kwa wazazi kutowapatia watoto watu wasiowafahamu kwani ni hatari.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwenge, Anna Ndimbwa alisema hili ni tukio la kwanza kutokea mtaani kwake na ni kitendo cha kikatili kwani umri wa mtoto ni mdogo na bado ananyonya na anahisi mama huyo aliyemwiba mtoto huyo huenda siyo mkazi wa mtaa hu.
Hata hivyo alitoa wito kwa yeyote anayemtilia shaka mwanamke mtoto asiye wa kwake atoe taarifa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi, Jerome Ngowi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linafanya msako ili kumbaini mtu aliyehusika na tukio hilo.
Matukio ya wizi wa watoto yamekuwa yakitokea mara kwa mara Mkoani Mbeya ambapo Jeshi la Polisi limekuwa likifanikiwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahusika wa uhalifu huo.
Kwa yeyote atakayemuona mtoto huyu anaomba atoe taarifa kwa simu namba; 0737903847.
0 COMMENTS:
Post a Comment