September 23, 2019


HUWEZI kutaja orodha ya wasanii waliokubalika katika Muziki wa Bongo Fleva mwanzoni mwa miaka ya 2,000 bila kulitaja jina la Lawrence Malima Madole ‘Marlaw’.

Marlaw alikuwa jamaa mmoja hivi kutokea Iringa ambaye alitikisa vilivyo na ngoma kibao kama Rita, Daima Milele, Bembeleza, Mbayuwayu, Busu la Pinki, Pi Pii (Missing My baby) na nyingine kibao.

Nyuma ya mkali huyu alikuwepo prodyuza Tudd Thomas aliyemsukia kuanzia ngoma zake za kwanzakwanza kama vile Bembeleza na Rita.
Kwa muda mrefu, Marlaw amekuwa kimya kwenye gemu, kuna kipindi aliachia ngoma haikuwa kali kivile, akapotea na kuendelea na shughuli nyingine za kijamii.

Over Ze Weekend limemuibua tena mkali huyu anayekimbiza na Ngoma ya Taa na katika mahojiano haya anafunguka zaidi;
Over Ze Weekend: Mambo vipi Marlaw?
Marlaw: Poapoa niambie.
Over Ze Weekend: Ulipotea ghafla kwenye gemu, hebu tuambie ilikuwaje na kwa nini uliamua kuwa kimya hivyo?

Marlaw: Kweli nilipotea kwa kipindi kirefu, lakini lengo lilikuwa ni kutaka kujifunza mambo mbalimbali katika sanaa ya muziki ninaoufanya, nashukuru Mungu awali nilikuwa siwezi kuandika nyimbo na kuprodyuzi, lakini sasa hivi naweza kufanya kila kitu hivyo hiyo ndiyo sababu kubwa iliyonifanya nipotee kwenye gemu.

Over Ze Weekend: Nimesikia una ujio mpya, wimbo wako unaitwaje na uliutoa lini?
Marlaw: Wimbo unaitwa Taa, nimeutoa tangu siku tano zilizopita hivyo ndiyo maana leo nipo hapa kwa sababu nimeamua kurudi rasmi kwenye gemu.
Over Ze Weekend: Kwa hiyo sasa hivi umerudi rasmi au ndiyo kama kawaida yako kutoa wimbo kisha unakaa baada ya miaka miwili au mitatu unatoa mwingine?

Marlaw: Hapana, sasa hivi nimerudi rasmi, watu wakae mkao wa kula, sasa hivi ni mwendo wa hit kwa hit hivyo ukimya wangu haukuwa wa bure.
Over Ze Weekend: Unaionaje gemu ya muziki kwa sasa? Je, kuna tofauti yoyote kati ya kipindi kile na sasa?

Marlaw: Gemu ya muziki iko vizuri kwa kwa kweli siwezi nikasema uongo, pia kuhusu tofauti upo kwa sababu sasa hivi wanamuziki wamekuwa wengi na wanazidi kuuboresha muziki wetu, kifupi wanafanya vizuri sana na ninawapongeza kwa hilo.
Over Ze Weekend: Kuna msemo unasemwa sana siku hizi kwamba msanii akishaoa, basi anapotea kwenye gemu wewe unazungumziaje hilo?

Marlaw: Siyo kweli kabisa, mimi nadhani ni juhudi zako tu binafsi ndiyo zinakufanya uendelee kuwa bora kila siku, japo ndoa nayo huwa ina changamoto, lakini ukipangilia ratiba zako vizuri kila kitu kinakuwa sawa.

Over Ze Weekend: Maisha ya ndoa unayaonaje kwa upande wako?
Marlaw: Yako vizuri, nashukuru Mungu mke wangu ananielewa na kunisikiliza pia.
Over Ze Weekend: Ulivyopotea wewe na Besta (mke wake) naye akapotea kwenye gemu, vipi ulimkataza kuendelea na muziki?

Marlaw: Hapana, sijawahi kumkataza Besta asiendelee kufanya muziki na kama unavyojua mimi nilimkuta mke wangu akiwa kwenye fani hiyo ndiyo nikamuoa kwa hiyo siwezi kabisa kumkataza nadhani yeye mwenyewe pia aliona ni bora tupumzike kwanza halafu tukiamua kurudi, turudi rasmi.
Over Ze Weekend: Vipi akihitaji kurudi kwenye muziki tena utamkubalia?
Marlaw: Ndiyo, tena nitamkubalia kabisa kwa sababu kwanza yeye ndiye amekuwa akinisukuma mimi kuja kwenye interview, sasa hivi na yeye yupo tayari kufanya muziki.
Over Ze Weekend: Kuna kolabo yeyote mliyoifanya pamoja kwa kipindi hiki?

Marlaw: Ndiyo, tayari tuna ngoma nyingi sana bado muda wa kuzitoa tu, kwa kweli tumejipanga inavyotakiwa!
Over Ze Weekend: Unaamini katika kiki?
Marlaw: Ndiyo!
Over Ze Weekend: Unahisi ni sahihi msanii kutanguliza kiki halafu ndiyo baadaye aje atoe ngoma?

Marlaw: Inategemea na aina ya kiki unayoifanya, unajua siku hizi watu wengi wapo bize na maisha yao, kwa hiyo huwa inakuwa ngumu kumfanya mtu awe makini kukusikiliza wewe aache kufanya shughuli zake, hivyo ambacho wasanii wengi wanakifanya nikuwapa watu attention, yaani ili mtu akuzingatie na kukusikiliza ni lazima kwanza ufanye kitu kitakachomfanya akuangalie kwa makini kisha baada ya hapo ndiyo unaachia ngoma yako.

Kwa hiyo nahisi ndiyo maana unaona wasanii wengi wanafanya sana kiki, lakini niwasihi tu ziwe kiki nzuri zenye kujenga siyo kubomoa au kuvunja maadili ya nchi yetu.
Over Ze Weekend: Lakini huoni kama ni hali ya kutojiamini kwa msanii?
Marlaw: Sidhani kama ni hali ya kutojiamini ila ninachokiamini mimi ni kwamba huwa wanafanya hivyo ili wazingatiwe that’s it.

Over Ze Weekend: Kati ya nyimbo zako zote ni wimbo gani uliokuletea mafanikio makubwa na hautausahau?
Marlaw: Nyimbo zangu zote naweza kusema kwa sababu asilimia kubwa ya watu wanazipenda nyimbo zangu zote.
Over Ze Weekend: Mondi na Kiba unamkubali nani?
Marlaw: Wote kwa kweli, wanajua kuimba na kila mmoja ana ladha yake.

Over Ze Weekend: Umeshawahi kufikiria kufanya nao kolabo kwa siku za hivi karibuni?
Marlaw: Nimeshawahi kufikiria nadhani ipo siku tutafanya, kwa sababu wale ni washkaji zangu, tumekuwa pamoja kwenye mambo mengi.
Over Ze Weekend: Kitendo cha Harmonize kuondoka WCB na kwenda kuanzisha lebo yake mwenyewe ya Konde Gang ni sahihi au kazingua?

Marlaw: Mimi naona kafanya jambo zuri tu, kama kila mmoja kwenye nafsi yake anaamani na ameridhia why not? Japo mimi siamini kama amejitoa, naona Harmonize bado yupo WCB.
Over Ze Weekend: Kwa nini uliamua kuishi Arusha?
Marlaw: Mimi na mke wangu tuna makazi mengi kiukweli, kuna kipindi tunaishi Arusha na siku zingine tunaishi hapa Dar, lakini kwa sasa tupo hapa Dar.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic