September 25, 2019








Na Saleh Ally
INAWEZA kuwa vigumu sana kukubaliana na mimi lakini uhalisia unaweza kukuonyesha kile ambacho ninakiamini mimi kwamba wasemaji maarufu zaidi wa klabu hapa nyumbani Tanzania, zaidi ni watatu, Haji Manara wa Simba, Masau Bwire wa Ruvu Shooting na Thobias Kifaru wa Mtibwa Sugar.


Kifaru ndiye amekuwa maarufu kwa muda mrefu zaidi ya wenzake, amekuwepo akiendelea kufanya mambo yake na ndiye mtu aliyetafutwa na watu wengi sana wakitaka waijue sura yake. Kama unakumbuka, redio ndio ilikuwa ina nguvu zaidi, anaonekanaje sasa? Mwisho walifanikiwa kumuona na sasa ni maarufu hata kwa sura kutokana na kizazi cha sasa, video imekuwa ina nguvu zaidi ingawa magazeti ndiyo yalianza kuitambulisha sura yake baadaye redio kuitambulisha sauti yake.


Baada ya hapo, tumekwenda na Masau akiendelea kutamba licha ya kwamba timu yake haina mashabiki wengi hadi alipoibuka Haji Manara. Huyu ni mwanasiasa, mtu ambaye amesomea propaganda, lakini ameifanya kazi yake vizuri katika suala la usemaji, ingawa wakati anaanza pia alikuwa ana makosa mengi.


Kwa sasa, Manara ni mtu tofauti kwa kuwa wakati anaanza naye aliboronga katika sehemu kadhaa, baadaye akatulia na kuanza kunyoosha mambo hadi kufikia kuwa msemaji maarufu kuliko wote kwa kipindi hiki.


Kutaka kulazimisha kuwa Manara si alivyo sasa ni kujiumiza kichwa. Vizuri kukubali kile anachokifanya mwenzako na hasa kama amefanikiwa.


Kulazimisha hajafanikiwa wakati uhalisia unaonyesha amepiga hatua au kufanya vizuri ni upotezaji wa muda.
Nasema hivi kwa kuwa hivi karibuni, Yanga imewatangaza watendaji wengine wawili wa majukumu yao kwa maana ya kuboresha utendaji.



Msemaji mpya ambaye ni Hassan Bumbuli, huyu kijana kwangu si mtu mgeni kwa kuwa tumekua pamoja kitaaluma.
Nilimfahamu mwaka 1999, nilipomkaribisha Habari Corporation Ltd ambako tulipikwa kikazi na amekuwa ni rafiki yangu kwa miaka mingi sana. Katika utendaji sina wasi naye lakini siwezi kuweka dhamana ya asilimia mia, naye ni mwanadamu.

Wazi niseme ninaamini anaweza kutekeleza majukumu yake. Mwingine ni Antonio Nugaz ambaye imeelezwa kwamba atakuwa ni Mhamasishaji wa Wanachama wa klabu hiyo.
Yanga inaonekana wametengeneza mfumo wa kuwatumia watu hao wawili, kwamba Bumbuli atakuwa akisimamia utoaji wa habari na Nugaz ni mzungumzaji. Vizuri kwa kuwa ninaamini Yanga wanajua wanachokifanya.


Pamoja na hivyo, vizuri wakakumbuka jambo moja, Yanga ipo kwa lengo la kufanya mambo yao vizuri, hili litakuwa zuri zaidi kwao na itaisaidia klabu.


Nasema hivi mapema kwa kuwa nimeona “mguu” wa Bumbuli na Nugaz, kama umekuwa na “mwendo mbaya wa mwanzo”. Wameingia kichwani mwao akiwa amejaa Manara zaidi ya Yanga yenyewe, hii haitakuwa sawa.


Tayari Bumbuli amemkosoa Manara katika siku za mwanzo tu, akisisitiza ni mropokaji na kadhalika. Anaweza kuwa na hoja lakini muhimu kwake ni Yanga na si Manara.


Anaweza kuwa na hoja lakini anapaswa kuwa makini na trick za maswali, kwa kuwa huenda akawa anafanya mambo yasiyo sahihi kujikuta unamzungumzia Manara kutaka kuonyesha si sahihi wakati kupitia hayo, ana mafanikio makubwa.


Kama unakumbuka nilianza kuzungumzia Masau na Kifaru, hawa wana aina yao tofauti kabisa. Ndio maana wamedumu na Manara pia amefika mbali kwa kuwa aliibuka na aina yake. Huu ndio maana ya ubunifu, hata kama usemaji nao unahitaji ubunifu.


Kwa upande wa Nugaz, yeye namuona kabisa analenga kushindana na Manara, anataka kuzungumza utafikiri “amekasirishwa”, huyu ni yule Manara wa zamani. Anataka kuzungumza kwa sauti ya juu, kusema harakaharaka, jambo ambalo Bumbuli anaonekana kutokubaliana nalo.


Vizuri Nugaz aingie kama Nugaz, awe mbunifu wa aina yake na kuweza kutimiza kazi yake vizuri kwa aina tofauti isiyofanana na Manara.


Maofisa habari wa klabu nyingi tu, huenda mmewasahau. Kutokana na kutokuwa wabunifu walishindwa, mwisho wakahamia vyeo vingine na leo hawapo kabisa na ndio maana wamesahaulika.

Jiulize kama kweli wewe ni mpenda mpira, utachukua muda gani kuwasahau Masau, Kifaru au Manara? Lazima itakuwa miaka nenda rudi.

Hivyo Nugaz naye asitake kuwa Manara, asitake kushindana na Manara kwa kuwa kazi yake ni kuzungumza kwa ajili ya Yanga. Kwenda kama Manara au kuzungumza kwa sababu ya Manara, mwisho atakayebaki atakuwa Manara.

2 COMMENTS:

  1. Brother Saleh unazungumza vizuri sana,umefanya la maana sana kumshtua huyo muhamasishaji mpya wa Manara

    ReplyDelete
  2. Katika dunia Mwenyezi mungu kamuumba binadamu mmmoja mmoja huwezi kufanana na mwingine hata kama mmezaliwa familia moja

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic